Mnyika katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema wananchi wanapaswa kumuita Chenge ‘nyoka wa ufisadi’ badala ya kujisifia kuwa ni ‘nyoka mwenye makengeza’ kwa kuwa amehusika katika kutafuna mali ya umma.
“Kauli ya Chenge kama ilivyokuwa kwa ile ya ‘vijisenti’, ni kiburi cha kifisadi,” alisema Mnyika.
Chenge alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Mahaha kata ya Vunamala, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, akiwaeleza wananchi wa jimbo lake kuwa aitwe nyoka kwa kuwa ni mjanja wa kutafuta fedha kwa ajili ya wananchi wake.Mnyika alisema udhaifu wa serikali na vyombo vyenye mamlaka ya kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya tuhuma za ufisadi unaodaiwa kufanywa na Chenge na watuhumiwa wengine wa ufisadi ndiyo unaowalinda nyoka wa ufisadi na sasa wanajigamba kuwa ni wajanja wa kutafuta fedha kifisadi.
“Chenge anadai kwamba yeye ni mjanja wa kutafuta fedha za wananchi wa jimbo lake ili hali yeye na wenzake wamesababisha wananchi wa jimbo lake na mengine nchini kukosa fedha nyingi zaidi za miradi ya maendeleo mpaka hivi sasa kutokana na ufisadi wa Tegeta-Escrow,” alisema Mnyika.
Alisema Rais Jakaya Kikwete anapaswa kujitokeza tena kulihutubia taifa kueleza hatua, ambazo ameendelea kuzichukua kukamilisha kutekeleza maazimio ya Bunge.
Mnyika alisema taarifa alizonazo hadi sasa wapo washirika wa maendeleo, ambao wameacha kutoa fedha kwa kutoridhika juu ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusiana na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow.
Aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupamana na Rushwa (Takukuru) kuweka wazi kwa umma matokeo ya uchunguzi wake na hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya wahusika.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment