KWA UFUPI: Katika utumishi wangu nimefanya operesheni kubwa zaidi ya 7,000 zikiwamo za viongozi wakuu wa nchi hii lakini leo baada ya kustaafu napigwa danadana sina thamani tena kwa Serikali
Moshi. Daktari bingwa wa zamani wa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Dk Fulgence Mosha anasotea mafao yake ya kiinua mgongo na pensheni kwa miaka 10 mfululizo bila mafanikio.
Akizungumza juzi, Dk Mosha alisema licha ya kulifikisha suala hilo kwenye vyombo husika, ikiwamo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, bado mafao yake ni kitendawili.
Dk Mosha aliajiriwa na Serikali mwaka 1983 kabla ya Januari 1,1995 kupelekwa KCMC kwa barua ya Desemba 29, 1994 yenye kumb HE/MP ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Desemba 11, 2004, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ikauandikia barua uongozi wa KCMC kutoa kibali cha Dk Mosha kustaafu rasmi baada ya kufikisha umri wa miaka 60 wa kustaafu kisheria.
Alisema baada ya kustaafu, alilipwa Sh10 milioni na Shirika la Hifadhi za Jamii (NSSF), ikiwa ni michango yake na ya mwajiri ambaye ni Shirika la Msamaria Mwema (GSF) linalomiliki KCMC.
“Katika utumishi wangu nimefanya operesheni kubwa zaidi ya 7,000 zikiwamo za viongozi wakuu wa nchi hii lakini leo baada ya kustaafu napigwa danadana sina thamani tena kwa Serikali,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Mosha, utata wa mafao yake ikiwamo kulipwa pensheni kila mwezi, unatokana na Hazina kutopeleka mchango wowote katika Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF).
Dk Mosha alisema baada ya kustaafu, alichukua malipo yake ya NSSF na kuyapeleka PSPF ili yajumlishwe na michango ya Serikali katika kipindi alichokuwa mtumishi wa Umma (1983-1994).
“Zile fedha zilikaa kule, PSPF wakaamua kunirudishia maana Serikali haikupeleka ile michango yake ambayo walitakiwa wailipe kati ya 1983 na 1994 nilipokuwa serikalini,” alisema.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu malalamiko ya Dk Mosha alionyesha kushtushwa na kusema, huenda daktari huyo hakutumia njia sahihi kudai haki yake.
“Simfahamu huyo daktari lakini ni jambo linaloshtua. Naomba mwelekeze aje ofisini na nyaraka zake zote nimpeleke SSRA (Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii),” alisema Kabaka.
Kwa mujibu wa Kabaka, kwa sasa zipo kanuni zinazounganisha mafao kama mfanyakazi alifanya kazi katika maeneo mawili yanayohudumiwa na mifuko miwili tofauti ya hifadhi ya jamii.
“Kwa jinsi ulivyonieleza isingewezekana kulipwa pensheni. Ni lazima mifuko hii miwili (PSPF na NSSF) ilitakiwa ikae na kuoanisha michango na mamlaka inayowakutanisha ni SSRA,” alisema.
Dk Mosha alipoelezwa kwamba Waziri amemuomba aende Dar es Salaam kumuona, alisema kwa sasa hana hata nauli kwa vile kwa miaka yote 10 tangu amestaafu amekuwa akiishi maisha ya shida.
“Nitapata wapi nauli? Dar nimekanyagia mpaka nimechoka sasa hivi nina miaka 70 hiyo nguvu iko wapi? Miaka 10 nimeishi bila pensheni na kumbukumbu zangu zipo. Kabaka naomba nisaidie,”alisema.
No comments :
Post a Comment