
Juu ni muandishi wa makala hii Bw. Jenerali Ulimwengu!
SIMULIZI yangu kuhusu
Balozi Steffler ililenga kushadidia dhana ya kujitambua na kujiheshimu. Bila
mtu au jamii kujiheshimu hawawezi kuheshimika. Ukijiheshimu utaheshimiwa kwa
kuwa unaheshimika na ukijidharaulisha utadharauliwa kwa kuwa unadharaulika.
Hali ya kuheshimika ni hatua moja kabla ya kuheshimiwa. Ina maana unazo sifa ambazo zinawafanya wengine wakuheshimu, na kwa hiyo, pindi watakapokufahamu, watakuheshimu. Hali ya kudharaulika nayo vivyo hivyo: Ni kwamba unazo sifa zitakazowafanya wengine wakudharau, na hivyo, pindi watapokufahamu, watakudharau kutokana na sifa watakazoziona ndani yako.
Katika mambo mengi tuliyoyapata katika historia yetu kama Waafrika – nikijadili bara la Afrika kwa ujumla – mojawapo ni dharau kubwa ambayo dunia iliyobaki imekuwa nayo juu yetu.
Matendo haya yote yalitendwa na watu kutoka nje dhidi ya Waafrika. Kwa hiyo haya ni matendo ya watu wengine. Lakini matendo haya yasingetendwa dhidi yetu bila sisi wenyewe kushiriki kwa kuwasaidia wageni hao katika matendo hayo dhidi yetu.
Katika hili kuna dhana mbili: Mosi ni pale ambapo, kwa jamii zetu nyingi, tuliposhindwa kukataa dharau ya viwango vile. Ingekuwa watu wetu waliondoka wakaenda Ulaya au Marekani, na huko wakajikuta wakinyanyaswa, tungekuwa na haki ya kulalamika dhidi ya manyanyaso hayo, lakini kwa kiasi kikubwa tungeelewa kwamba tunafanyiwa hivyo kwa sababu tumejipeleka wenyewe katika nchi za watu. Kukubali kwamba wageni waje nyumbani kwetu halafu watunyanyase hapa hapa, ni jambo jingine kabisa.
Udhalili huo ndio uliowapa wageni hawa ujasiri wa kutufanyia kila walilolitaka, ikiwa ni pamoja na kututeka na kutupeleka kama watumwa, tukauzwa kama ng’ombe. Udhalili huo haujatoweka, na dharau hiyo tunaishi nayo hadi leo.
Pili ni pale baadhi yetu waliposhiriki moja kwa moja katika kuwasaka, kuwapiga na kuwateka ndugu zao, na kisha kuwakabidhi kwa wageni kama watumwa, bidhaa za kusafirishwa ughaibuni. Baadhi ya wasaliti hawa waliotengeneza faida ya fedha na mali kwa kuwauza ndugu zao walikuwa si wengine ila watawala wetu waliokuwa na dhamana ya kuwalinda na kuwahami watu wao. Hali hii pia haijaondoka, hali ya watawala kushiriki kikamilifu katika kuwauza watu walio chini ya mamlaka yao.
Ni kweli kwamba walikuwapo watawala wa baadhi ya jamii katika bara letu waliokataa dharau hii, na wakasimama kidete na wakapigana. Historia zao zimeandikwa. Lakini walikuwa wachache ; wengi walikubali kuwa vibaraka wa wageni katika kila jambo walilotaka wageni hao. Kwa maana hiyo walikuwa ni maadui wa watu wao. Na hivyo ndivyo ilivyo hadi leo.
Haya si makovu; ni vidonda vinavyoendelea kutiririka damu na usaha. Dharau tuliyoikubali karne tano zilizopita bado inatufuata hadi leo, na sisi bado tunaiendeleza kwa njia nyingi. Waafrika hatujipendi, hatujithamini, hatujiheshimu, na msingi wake mkuu ni kwamba hatujijui, hatujielewi, hatujifahamu.
Angalia tunavyothamini kila kitu kutoka nje na kudharau kilicho chetu. Ikitokea raia wa nchi hii akatoa mawazo ya kuisaidia nchi, lakini mawazo hayo yakiwa ni tofauti na watawala wanavyofikiri, mawazo hayo yatakataliwa na kubezwa. Mawazo hayo hayo yakija kusemwa na kijana mdogo kutoka Uropa au Marekani watwala wetu watayadandia na kuyaona ni kama aya zilizoteremshwa na malaika.
Nimewahi kuwasikia watawala wetu wakishangaa kwamba sisi tunalalamika kuhusu mambo wanayoyafanya wakati Wazungu wanawasifu, utadhani Wazungu ndio waliowachagua! Kashfa zilizoibuliwa na vyombo vyetu wenyewe hazifanyiwi kazi mpaka Wazungu waseme kwamba tusipozishughulikia hawatatupatia misaada.
Dharau ya kujidharau wenyewe imekwenda mbali zaidi kiasi kwamba hatupendi kuonekana kama Waafrika. Tunauchukia Uafrika, na ingekuwa inawezekana tukaumbwa upya katika muonekano mwingine, bila shaka tungeteua kuwa Wazungu au Waasia, au Waeskimo, kwa jinsi tunavyoona dada zetu – wakati mwingine hata wanaume – wakijichubua ili wawe na ngozi nyeupe.
Leo hii, zaidi ya nusu ya wanawake unaokutana nao wamefunga manyoya kichwani yanayofanana na nywele za Kizungu au Kiasia. Nimeona kibao jijini Dar es Saalam kinachotangaza kwamba nywele mpya zimewasili kutoka Peru! Manyoya haya, ambayo ni ya gharama kubwa, yananunuliwa hata na wanawake ambao hawajui mlo ujao utatoka wapi, lakini fasheni ni kuwa Mzungu bandia, na hilo ni muhimu kuliko chakula.
Tumeambiwa mara kwa mara kwamba kuchubua ngozi ni hatari kwa afya yako kwani kunasababisha ngozi iathirike na mionzi ya jua, na hilo linaweza kusababisha saratani, lakini hatusikii, kwa kuwa labda ni bora uwe Mzungu kwa muda mfupi halafu ufe kuliko kuishi miaka mingi bila kuwa Mzungu walau kidogo.
Manyoya yanayovaliwa na akina mama wakati mwingine huja yakiwa yamebeba chawa na minyoo, na ni rahisi kwa wadudu hawa kuwaumiza wavaaji wa manyoya hayo. Tunaponzwa na uzungu feki wakati nywele za Kiafrika zinaweza kutengenezwa na zikapendeza. Sababu kubwa ni kwamba hatujipendi, na tunajidharau na kujichukia.
Aidha, tunajua kwamba tunazo rasilimali nyingi na kubwa, lakini akili zetu hazitumiki kuzichukulia kama nyenzo za ukombozi wetu kama tukiamua kuzifanyia kazi kwa juhudi na akili; tunaona ni rahisi zaidi kwenda kuombaomba na kujidhalilisha mbele ya Wazungu.
Kila mtu anaelewa ni kwa nini watawala wetu wanasema kwamba wanasifiwa na Wazungu. Ulitaka Wazungu waseme nini wakati wanazungumza na wewe ukiwapo? Watakusifu tu kwa sababu wewe ni mradi wao, kuna vitu wanataka kutoka kwako na wakijua kwamba sifa zitakuvimbisha kichwa, watakusifu tu, tena sana.
Lakini sisi binadamu wa kawaida tunazungumza nao katika mazingira tofauti, na tunasikia mambo ambayo watawala hawatapata nafasi ya kuyasikia, labda baada ya kuondoka madarakani. Hao hao wafadhili wanaowasifu watawala wetu ndio hao hao wanaotuambia katika mazingira tofauti kwamba wanachoshwa na tabia za ombaomba za watawala wetu. Isitoshe, kinachozidi kuwaudhi ni tabia ya ombaomba inayoambatana na ubadhirifu wa kutisha.
Hawaelei ni jinsi gani nchi inaweza kutembea kote duniani ikiombaomba kwa kusafiri daraja la kwanza wakati wafadhili wenyewe wanasafiri daraja la kawaida. Ni kama ombaomba uliyemtupia shilingi mia tano hapo mapema umkute hotelini anafurahia ‘lobster’ na mvinyo. Hivyo ndivyo wanavyotuona, kama watu tusio na maana wala mantiki.
Wazungu wanatuangalia na wanatufuatilia katika kila tunalofanya, na kwa kuwa wanajua kwamba tunajidharau, nao hawana la kufanya ila kutudharau. Wanatuona kama tumbili wanaoongea. Ndiyo maana vijana wetu wanaocheza soka Ulaya kila siku wanatukanwa kwa kulinganishwa na tumbili. Wanafanyiwa hivyo kwa sababu bara walikotoka linaendeshwa kama himaya inayoendeshwa na tumbili kutokana na matendo yetu, na hasa ya watawala wetu.
Naapa kwamba siku itawadia, na nchi zetu zitakuwa na watawala wanaoendesha nchi zao katika misingi ya akili na mantiki, zikiwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa badala ya kuuza mali-ghafi. Tutaacha kusafirisha ajira za vijana wetu kwenda China na mali-ghafi zetu zitatumika kuzalisha ajira hapa hapa Afrika kwa ajili ya vijana wetu. Tutakuwa bara la viwanda, utafiti, uvumbuzi, usomi uliotukuka, falsafa ya kina, na ushairi.
Tutaondokana na njaa, maradhi na umasikini katikati ya neema kubwa. Watu wetu wataishi maisha ya staha na furaha. Watoto wetu, wanawake wazazi na wazee watakuwa na siha bora maisha yao yote. Likitokea janga duniani tutakuwa miongoni mwa mataifa yanayoepeleka misaada. Tutawapelekea misaada masikini wa Uropa na Marekani kwa sababu tutakuwa tunayo ziada ya kutosha.
Tukifikia hatua hiyo, hata kelele za nyani katika michezo ya soka Ulaya zitapungua. Vijana wa Kizungu watatuheshimu kwa sababu tutajulikana kama watu makini, watu wa mantiki, siyo ombaomba. Watakuja kujifunza kutoka kwetu kwa sababu tutakuwa tunafanya maajabu.
Ili kufikia hatua hiyo, hatuna budi, angalau kwa nchi kama yetu, kuanza kwa kutambua kwamba huwezi kumfundisha mtu jambo lo lote kupitia lugha asiyoielewa; mbaya zaidi mwalimu aisyeelewa lugha anayofundishia ni mtu hatari kwa maendeleo ya motto. Niliwahi kusema kwamba ingewezekana watoto wa Kisukuma wangefundishwa Kisukuma wangelewa zaidi wanachofundishwa, na watoto wa Kihaya, na wa Kimakonde pia. Labda hili ni gumu zaidi kuliko Kiswahili kwa nchi nzima, na kwa ngazi zote.
Itaendelea - See more at: http://www.raiamwema.co.tz/tunadharauliwa-kwa-sababu-unadharaulika-tunajidharau#sthash.3CpAwSHt.dpuf
No comments :
Post a Comment