Ahoji mbona wezi wa kuku wanafungwa?
Alitoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kibakwe ikiwa ni sehemu ya ziara zake za kuimarisha chama na kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, mkoani Dodoma.
“Ili chama kiendelee kuaminiwa na watanzania ni lazima wana CCM wenzangu kuwa wakali, cha kwanza kinachowaudhi watanzania na watu wa Kibakwe ni wizi, na kinachowaudhi zaidi mtu akichukua halafu tunaanza kupiga maneno," alisema.
Alisema kinachowashangaza watu ni pale mtu kuiba halafu anaulizwa anaonaje akiondoka.
“Lakini mwingine akiiba kuku, inakuwaje, anafungwa, siyo sawa lazima tukatae, kweli si kweli ndugu wananchi? Mtu wa kwanza anatakiwa kukasirika kuchukua hatua, siyo upinzani ni CCM, nataka niwaombe wana CCM nchi nzima kuweni wakali acheni kulinda na kutetea watu wasio na uadilifu,” alisema.Alisema kuna tabia siku hizi imezuka mtu anaiba na akishaiba wanajitokeza wana CCM wenzake kumtetea.
"Nikikutuma kazi na nikakuamini fanya ninavyotaka na si kufanya unavyotaka wewe, nataka niwaahidi wananchi, CCM tutakuwa wakali naelewa humo humo ndani kuna wengine watasema ngoja kwanza..., subiri kwanza..., unajua.. na siku hizi kuna kitu kimekuja na nyinyi ni mashahidi kinaitwa utawala bora..."
Alisema wakati mtu anaiba, hafuati utawala bora, lakini akishaiba wanaambiwa wafuate utawala bora kumshughulikia.
“Hakikisheni bwana huyu anachunguzwa lakini ameshaiba, tafuteni ushahidi keshaiba, mpeni muda wa kujieleza, keshaiba, utawala bora na ukiwa na fedha mambo yako mazuri sana kwasababu gani? Utaweka mawakili wanne, mwizi wa kuku anaweka mawakili wangapi?”alihoji.
Alisema utawala bora nao uangaliwe kwani umeegemea upande mmoja, mtu akiiba mahala pake ni jela na si maneno.
Aliwataka wana-CCM wachukuliane hatua kwa kuadhibiana na kuwajibishana, kama ilivyokuwa utamaduni ulioasisiwa na hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere.
“Baba wa Taifa anasema ukikosea usiuguse moto, kwani ukiugusa moto unakuchoma pale pale na ukifanya kosa adhabu pale pale, zamani kulikuwa kuna kitu kinaitwa kustaafishwa kwa manufaa ya umma, sasa imeondolewa...Mimi ninakijua chama kinachosimamia misingi,”alisema Kinana.
“Lakini mkikaa mnafanya vitu vyenu mnalindana hatari sana, wana CCM wenzangu Iyena...Iyena...tuwe wakali, tumepewa dhamana tumeaminiwa na sisi tuwe wakali, tusilindane, mnakaa kwenye vikao anakuja mtu ananyoosha kidole eti kwanza tumuache tumchunguze, tunamchunguza nini tukitaka kuchunguza akae nje kwanza atoke, siyo unamwambia abaki ndani unamchunguza".
Alisema wana-CCM wengi ni masikini, wanaosingiziwa wala rushwa, wezi wachache hata mkono hawajai, wengi ni maskini wa kawaida wanakaa vijijini lakini wanabeba dhambi ya watu walio mbinguni walaji.
Alisema wananchi wamekichagua chama kwa ilani na kwa ahadi, hivyo chama kinapoona kimeshindwa kutekeleza baadhi ya ahadi kiite wananchi kuwaeleza kwanini kimeshindwa, kama kilivyowaita wakati wa kuomba kura.
Naye Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye alivitaka vyama vya upinzani kuacha kukumbatia vurugu na kuwagawa wananchi kutokana na siasa za majitaka.
“Mnajua lengo la kuanzishwa kwa upinzani ni kuleta hoja za ushindani kwa ajili ya kuchochea maendeleo lakini vyama hivi ni sawa na hadithi ya fisi aliyelazimisha kuhudhuria mkutano wa wanyama wenye pembe huku akijua hana pembe,”alisema. Alisema wajiulize vyama gani vinajengwa kwa damu za wananchi, ni laana na kazi moja kwa mwaka huu ni kumfukuza kichaa na makopo yake.
“Kichaa afukuzwe na makopo yake kwa sababu hata akikaa miaka mingapi atayarudia, ukisikia mtu anasema ‘peoples’ mwambie tunafukuza vichaa, akisema tena ‘peoples’mwambie tunafukuza kichaa na makopo yake, ukisikia ‘Haaakii’ mwambie tunaondoa vichaa.
“Njia za kuwafukuza ni kuwanyima kura hata moja, kwa sababu wapinzani hata wakipata kura tatu au moja, watarudia makopo yao na watajua wana watu wao watarudi tena uchaguzi ujao,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment