Lowassa aliyasema hayo nyumbani kwake jana mjini hapa, kufuatia baadhi ya vyombo vya habari, kumnukuu Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais, akisema baadhi ya watu wanatumia vibaya umaskini wa Watanzania kwa kuwakusanya na kuwapa fedha ili waseme wanawashawishi wawanie urais.
Akizungumza mbele ya wachungaji 110 wa makanisa ya Kipentekoste kutoka sehemu mbalimbali nchini jana, Lowassa alisema hana uwezo wala sababu ya kuwagharimia watu wanaofika nyumbani kwake kumshawishi na kwamba wengi wanafanya hivyo kwa mapenzi yao na Mungu wao.“Najiunga na mwenzangu (Mwenyekiti wa CCM Shinyanga, Khamis Mgeja) kusema leo (jana) kuna mtu kwenye magazeti amesema maneno ya hovyo hovyo kidogo, ambaye nikimjibu nitakuwa nampa heshima kwa hiyo nampuuza, sina uwezo wa kuwagharamia watu wote hawa waje nyumbani kwangu na wala sina sababu,” alisema.
Alisema makundi yanayomshawishi awanie nafasi hiyo wanafanya hivyo kwa utashi wao, mapenzi yao kwa taifa na Mungu wao na kwamba ‘lugha nyingine tofauti ni upuuzi tu na uongo.’
Awali, Mgeja alisema watu wanaosema kuwa wanaofika nyumbani kwa Lowassa wanalipwa, ni walioishiwa hoja, wamefilisika na sasa wanatapatapa na kwamba kuwajibu watu hao ni kuwapa sifa wasizostahili kwani baadhi yao wanahitaji muda mrefu wa kujifunza siasa.
“Nimekaa muda mrefu kwenye siasa, wengine bado wanahitaji wapate muda wa kujifunza na katika siasa hatuwajui ni wapi walipotokea, wakipata muda mzuri wajifunze, wawe na adabu, watulie kuliko kuzusha maneno ambayo huna uhakika nayo, ambayo ni dhambi kubwa sana,” alisema Mgeja. Alisema wakati wa sherehe za miaka 38 ya CCM mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete alitoa rai kuomba wananchi na wana CCM wakiona mtu anayefaa kuwa kiongozi wamshawishi, hivyo wanachokifanya siyo makosa.
“Tusihukumiane kwenye hili, Mgeja na wengine wamefika nyumbani kumshawishi, ndivyo tulivyoombwa kwamba tukiona ana uwezo tumshawishi, mpeni nguvu, mjengeni suala hili ni kubwa linahitaji dua na maombi. Kama viongozi tumeona kwa maana tunafahamiana, nani anafaa kupokea kijiti na kutupeleka mbele, niungane na Watanzania wenzangu na mimi kusema tunaona kwamba hakuna mwingine zaidi ila Mheshimiwa Lowasa,” alisema Mgeja.
Aidha, Lowassa alizungumzia ujio wa wachungaji hao nyumbani kwake jana, akieleza kuwa umeandika historia katika maisha yake kwani hakutegemea kupokea kundi kubwa kama hilo la watumishi wa Mungu.
Alisema watu ambao wamemfuata kumshawishi amewaambia kuwa nafasi ya urais ni kubwa na inahitaji maombi.
“Ninachoomba wachungaji mmekuja nawashukuruni sana, mkapige magoti mpaka yachubuke, hatimaye niweze kusema nayaweza yote katika yeye anitiaye nguvu,” alisema.
Mapema, Mratibu wa ujio wa Wachungaji hao, Mchungaji Benedickto Kamzee, kutoka Kanisa la Glory of Christ la Katavi, alisema wamefikia uamuzi huo bila kushinikizwa wala kushawishiwa na mtu yeyote.
“Hakuna aliyetushawishi, hata siyo maaskofu wetu, hili suala halina msukumo wowote zaidi ya msukumo wa Mungu,” alisema.
Kamzee alisema wachungaji hao wanatoka kwenye madhehebu ya EAGT, TAG, PEFA na KLPT kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Wachungaji hao waliingia nyumbani kwa Lowassa wakiwa na mabango yaliyoonyesha maeneo waliyotoka.
Maeneo hayo ni pamoja na Meatu, Makete, Karatu, Busega, Bariadi, Bukombe, Igunga, Chakechake, Mafia, Karagwe, Nachingwea, Temeke, Kinondoni, Rombo, Monduli, Kilwa, Mkuranga Kasulu na Bunda.
Wengine wanatoka Handeni, Ngara, Iramba, Mpanda, Bagamoyo, Same, Masasi, Kibondo, Kilombero, Rungwe, Mwibara, Kisarawe, Nachingwea na Kilolo.
WANAFUNZI, WAFANYABIASHARA WANENA
Wakati huo huo, wanafunzi wa vyuo vikuu na wafanyabiashara mjini hapa waliokwenda kwa Lowassa juzi kumshawishi agombee, wamesema kwa Lowassa hakukuwa na ubwabwa wala soda na kwamba kauli ya Makamba inaonyesha kuwa Lowassa ni kiongozi anayefaa ndio maana watu wanampinga.
Rais wa Kitivo cha Imformative katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Goodluck Philip, alisema wanafunzi walikwenda kwa Lowassa kwa utashi binafsi na bila shinikizo na kwamba kauli ya kuhongwa imewadhalilisha.
Alisema kauli hizo zinalenga kuwatisha watu wakati msingi wa kufanya hivyo ni wa kidemokrasia.
Naye mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Dodoma, Norbati Pangaselo, alisema wapinzani wa Lowassa wanatakiwa kujenga hoja badala ya kuzusha uongo kwa nia ya kumchafua.
WAZAZI WAJA JUU
Mbio za uchaguzi wa urais zimeanza kukichanganya CCM, kufuatia Jumuiya ya Wazazi kutoa tamko kali la kutaka kuwachukulia hatua wenyeviti na makatibu wa mikoa wa jumuiya hiyo na wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya waliokwenda nyumbani kwa Lowassa kumshawishi agombee urais mwaka huu na kumpatia Sh. 600,000 wakidai ni kwa niaba ya baraza hilo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, alisema CCM ina maadili na taratibu zake kwa wanachama wanaotaka kugombea urais mwaka huu.
"Viongozi 20 wa jumuiya waliokwenda kwa mgombea mmoja (Lowassa), wakae kwenye vyombo vya habari wakanushe hawakwenda kwa niaba ya Jumuiya ya Wazazi ndani ya mwezi huu na kwamba kukanusha huko hakuzii kuwahoji kwenye kikao cha maadili” alisema Bulembo.
Alisema vikao vya maadili vya jumuiya hiyo vitakaa kuwajadili na wakibainika kufanya makosa wanaweza kuchukuliwa hatua ambao ni pamoja na kufungiwa uanachama miezi sita, 12 na 18 au kufukuzwa kabisa uanachama.
Kwa mujibu wa kanuni ya Jumuiya ya Wazazi toleo la Mwaka 2008 kifungu cha 83 Ibara ndogo ya 11, Baraza la Wazazi Taifa litakuwa na uwezo wa kumfukuza au kumsimamisha uongozi kiongozi yeyote ambaye uongozi wake huteuliwa na Umoja wa Wazazi.
Bulembo alisema viongozi watakaojadiliwa na ikibainika wamekiuka kanuni watakumbwa na adhabu hiyo ni wenyeviti wa wazazi mkoa wa Kilimanjaro, Simiyu, Mwanza, Mbeya , Morogoro, Shinyanga, Kusini Unguja na Mkoa wa Mara. Wajumbe wa Baraza Kuu watakaojadiliwa ni kutoka mkoa wa Tanga, Mbeya, Dodoma, Ruvuma na mkoa wa Njombe wakati Makatibu wa Jumuiya wanatoka mikoa ya Kusini Unguja, Morogoro na Shinyanga.
Alisema siyo kosa kwa kiongozi au mwanachama yeyote kuonyesha mapenzi kwa mtu yeyote anayetaka kugombea urais, lakini taasisi ya chama haiwezi kuwa na mgombea wake itakuwa imekosa sifa.
"CCM ina jumuiya tatu, Jumuiya ya Vijana, Wazazi na Wanawake, jumuiya mojawapo inaposema ina muunga mkono mgombea fulani haifai kubaki tena katika CCM kwa sababu kazi ya jumuiya hizi ni kufanya kazi za chama kutegemeana na maelekezo," alisema.
Alisema unapozungumzia taasisi ambayo ni Jumuiya ya Wazazi yenye wanachama zaidi ya 2,300,000 Tanzania nzima, hivyo anapotokea kiongozi mmoja anasema anazungumza kwa niaba ya wanachama hao ni hatari na anavunja maadili ya chama ambacho hakiruhusu taasisi kujihusisha na mgombea yeyote.
Bulembo alisema CCM itatoa mgombea wake baada ya mkutano mkuu kwa kazingatia vikao vya chama, hivyo wale wote waliokwenda kwa Lowassa watachukuliwa hatua kwa kuitumia jumuiya kwa matakwa yao .
"Lakini hawa wagombea urais napenda niwaase, kama wanataka kugombea ndani ya CCM wafuate taratibu za chama na kusoma vitabu vinavyoelezea miiko ya chama, lakini unakuta mgombea anakusanya watu Mbeya na maeneo mbalimbali jamani anataka nini?” alihoji.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment