Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, March 4, 2015

NANI KAMA NYERERE????

Image result for julius nyerere

Hajatokea kama Mwalimu Nyerere

KWA UFUPI
Hotuba yake nzuri iliyovuta wengi, ilikuwa kama mbegu iliyopandwa moyoni mwangu, siyo siri kwamba tangu kipindi hicho, nilivutiwa kuingia katika harakati na hasa suala zima la haki za wanyonge.
Nilikutana na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa mara ya kwanza mwaka 1978. Mimi nilikuwa Seminari ya Likonde wilayani Mbinga. Mwalimu alikuja kutembelea Kijiji cha Amani Makoro.
Hotuba yake nzuri iliyovuta wengi, ilikuwa kama mbegu iliyopandwa moyoni mwangu, siyo siri kwamba tangu kipindi hicho, nilivutiwa kuingia katika harakati na hasa suala zima la haki za wanyonge.
Mara ya mwisho, nilikutana naye huko Musoma mwaka 1998, wakati wa sherehe za Jubilei ya miaka 25 ya upadri wa Askofu wa Jimbo la Musoma, Mhashamu Justin Samba. Nilipopeana naye mkono, sikujua kuwa hiyo ndiyo ilikuwa siku yangu ya mwisho ya kuagana naye.
Nilimpenda kutokana na mengi. Alikuwa mkweli, anayechukia waziwazi matendo ya dhuluma, uonevu na ukandamizaji wa namna yoyote ile. Mwalimu alikuwa na upendo wa kweli na mzalendo kwelikweli.
Kama mtu niliyepata bahati ya kuhudumia watu katika mambo ya kiroho, namhesabu Mwalimu Nyerere kama “mtumishi” wa watu wote bila kubagua dini, rangi, kabila au tabaka la maskini na tajiri. Kibiblia, namwona kama ni Musa aliyetumwa na Mungu kuwakomboa Watanzania.
Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa Taifa alionya, kukemea na hata kuadhibu mambo yote yaliyokwenda kinyume na jamii.
Mwalimu Nyerere aligusa mioyo ya wote wacha Mungu na wasiomcha Mungu, wasomi na wasiosoma wote walikuwa walengwa wake. Pia watenda maovu walikuwa wanaishi kwa hofu wakikosa amani siku hata siku.
Mmoja wa mapadri nchini Uingereza aliyemhudumia kiroho wakati amelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, London Uingereza, mwaka 2004 alinisimulia mjini London jinsi alivyojisikia furaha na heshima ya pekee kumhudumia mmoja wa watu mashuhuri duniani. Ndiyo kwa maana nathubutu kuandika kwa uwazi kwamba “Hajatokea kama Mwalimu Kambarage Julius Nyerere.”
Marehemu Kapteni John Komba, mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za kisiasa aliyeaga duniani mwishoni mwa wiki aliimba katika mazishi ya Mwalimu Nyerere kwamba: “Kama siyo juhudi zake Nyerere Tanzania leo hii ingekuwa wapi?”
Mchango wa Mwalimu
Maisha ya Watanzania yasingefika hapa bila juhudi za Mwalimu Nyerere. Aliwapa misingi imara ya Taifa hili kama vile umoja, uzalendo, amani, utu, elimu, usawa, uongozi wa kutumikiana kwa upendo na kuheshimiana.
Mwalimu alipenda maendeleo ya watu na siyo ya vitu na zaidi aliwapenda maskini. Aliongoza kwa kutumia misingi ya imani yake bila kulazimisha wengine kuiga bali aliwavutia kwa mifano na matendo yake. Mimi nasema “bado hajatokea kama Nyerere".
Kila tunapokaribia Uchaguzi Mkuu tunajiuliza je, hali ya viongozi wetu wa Serikali au chama ni ile inayofuata misingi ya kujali masilahi ya Taifa na kuzingatia miiko ya uongozi kama alivyofanya Nyerere?
Watanzania leo wanalalamikia viongozi mafisadi, uporaji wa rasilimali, udini, mauaji ya walemavu wa ngozi, mauaji yanayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama, ubabe na mengineyo.
Utiaji sahihi wa mikataba ya mibovu kama gesi asilia ni alama wazi ya kukosekana kwa roho ya uzalendo kwa viongozi wetu. Mashirika mengi yameuzwa katika hali inayotia simanzi.
Watanzania wanaona kwamba nchi hii inawanufaisha wageni kuliko wazawa. Kibaya zaidi waliokuwa wafanyakazi wa mashirika na kampuni hizi, wengi wao hawajalipwa hadi leo, hata wengine wamekufa bila kulipwa!
Miiko ya uongozi iko wapi?
Tumesikia viongozi wengi wakituhumiwa kwa rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, ukandamizaji, wizi wa fedha za umma kama escrow, na hapa unajiuliza je, miiko ya uongozi iko wapi?
Leo hii viongozi wanafanya wanavyotaka na hakuna wa kuwakemea wala kuwawajibisha kama alivyofanya Mwalimu Nyerere, ambaye hakuwa na huruma na kiongozi mzembe na aliyekosa nidhamu. Je, tutakuja kumpata tena Nyerere mwingine?
Serikali ya awamu ya tatu ndiyo ilyokomaza rushwa na ufisadi Serikalini na mashirika ya umma. Rushwa na ufisadi vimeendelea kuwa kero na sumu mbaya chini Tanzania. Pia sasa kansa hii imekuwa mbaya katika Serikali ya sasa.
Suala la demokrasia na utawala bora linazidi kupoteza matumaini katika awamu hii sababu ya matumizi mabaya ya vyombo vya ulinzi na usalama.
Ubinafsi, umimi na “u-mungu” mtu kwa viongozi unaongezeka, viongozi wengi wakiambiwa ukweli wanasema “umewadharau au umewatukana.” Kwa mantiki hii, wananchi wametawaliwa na hofu na unafiki.
Sheria nyingi zinatungwa, lakini hakuna anayezisimamia, wananchi wengi bado hawaelewi haki zao hata zile za msingi. Uandikaji wa Katiba Mpya umetupilia mbali maoni ya wananchi yakapachikwa ya CCM. Je, hii ni sahihi?
Kwa upande wa amani ya nchi yetu, tumeendelea kuona maovu mengi kama mauaji kati ya wafugaji na wakulima. Migogoro ya wafanyakazi na waajiri wao, mathalan walimu na wauguzi. Tumeshuhudia mauaji katika mikutano ya kisiasa yakiendeshwa na Jeshi la Polisi mfano halisi mauaji ya mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Chuki za kisiasa zinaendelea kukua kila kukicha kati ya CCM na wapinzani hasa Ukawa. Vikundi vya kihuni vimeendelea kuibuka kama panya road na mauaji ya walemavu wa ngozi yanapamba moto na kutoa alama kwa jumuiya ya mataifa kwamba “nchi ya Tanzania imetia fora katika suala zima la ushirikina na uchawi,” najiuliza angekuwa Nyerere leo Serikali yake ingefanya nini?
Zaidi ya hayo, tunashuhudia elimu ikivurugwa na wanasiasa uchwara kwa masilahi binafsi, ajira kwa vijana ikikosekana kwa kiwango kikubwa, matibabu yakikosekana hospitalini na huduma nyingine muhimu.
Mwalimu Nyerere alifundisha kwamba; “Ukitaka amani tenda haki.” Ni ukweli usiopingika kwamba “ bado hajatokea kama Nyerere.” Mungu ibariki Tanzania hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015.
Ni kweli Mwalimu alikuwa zawadi pekee kwa nchi yetu na ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania imesimama kwenye msingi imara aliouweka Mwalimu. Mungu amlaze mahali pema. Hata hivyo ningependa kuwaasa watanzania wa sasa tusimtumie Mwalimu vibaya.
Sasa hivi tunaishi dunia tofauti na ya Mwalimu. Mambo yamebadirika, na rais yeyote wa sasa hawezi kutawala nchi kwa style ya Mwalimu. Ni kweli sasa hivi yameibuka mambo yasiyopendeza katika jamii kama alivyoelezea Fr Mapunda, lakini nasikitika kiongozi wa dini kama yeye ameyaelezea kisiasa. Amani ya nchi hii inawategemea sana viongozi wa dini na bora wakajitathmini pale wanapoongea wavue kabisa ushabiki wa kisiasa. Namshauri Fr Mapunda afanye uchaguzi kati ya kuwa kiongozi wa dini au mwanasiasa, kama alivyofany Dr Slaa.
Pamoja na maovu aliyoyaorodhesha Fr Mapunda, yapo mengine mazuri ambayo nayo inabidi yaongelewe ili kuleta mwanga wa matumaini. Watanzania hatuwezi kujenga nchi yenye matumaini kama kila mara tunaangalia maeneo hasi tu. Kuna mahali tunafanya vizuri. Nimekuwa nikimsoma Fr Mapunda yeye kila mara ni kuponda tu kwa kutumia lugha inayoonyesha yeye yupo upande fulani wa mlengo wa kisiasa. Hii si sahihi kwa kiongozi wa dini kama Fr Mapunda. Inabidi ajitambue yeye ni nani katika jamii.
Sina uhakika kama maoni anayoyatoa katika makala mbali mbali kupitia gazeti la Mwananchi ni maoni ya Kanisa Katoliki. Sijasikia kiongozi yeyote wa ngazi ya juu katika kanisa Katoliki akikemea tabia hii ya Fr Mapunda. Kanisa Katoliki limejipambanua kwa msimamo wake wa kutetea ukweli bila kujihusisha na upande wowote wa kisiasa ndiyo maana Kanisa linaheshimika duniani kote na kila mtu. Katika safari yetu ya kujenga taifa lenye heshima na maendeleo tunahitaji kanisa lituongeze wote wenye mawazo tofauti ili tuweze kupita salama katika changamoto zinazotukabili sisi watanzania bila kuharibu amani yetu ambayo wahasisi wetu wametuachia. Watanzania wakianza kuwa na hisia kuwa Kanisa linajiambatanisha na mlengo fulani wa kisiasa hatutakuwa salama katika nchi. Ndiyo, kanisa lina wajibu wa kukemea maovu lakini lifanye hivyo katika lugha ambayo haitoi hisia kuwa linaegemea upande fulani wa mlengo wa kisiasa. Nawaomba viongozi wote wa dini waiombee nchi yetu ili tupite salama katika changamoto zilizoko mbele yetu kama vile mchakato wa katiba mpya na viongozi wapya watakaopeleka nchi yetu mbele. MUNGU IBARIKI TANZANIA.


No comments :

Post a Comment