- Usingizi asili yake nini? Ni swali alilowahi kuuliza mwanamuziki Dk Remmy Ongala na bendi yake ya Super Matimila katika moja ya nyimbo zake. Lakini katika hali ya kawaida, usingizi unaweza kuelezewa kuwa ni hali inayomtokea binadamu katika kila saa 24, ikisukumwa na ubongo wake ili kukamilisha siku.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linaielezea afya ya binadamu kuwa ni hali ya kustawi kimwili, kiakili na kijamii na siyo kukosa maradhi pekee.
Hata hivyo, wengi hawafahamu ukweli huo ambao unaweza kuwa ndiyo sababu ya kufanya mambo yanayoweza kuhatarisha afya za jamii.
Usingizi ni moja ya mambo yanayoweza kuathiri afya ya mtu. Kulala zaidi au kutolala vya kutosha ni hatari kwa afya.
Hivyo ndivyo ukweli ulivyo kiafya, ingawa tatizo lililopo ni kwamba, wengi hawajui walale muda gani na kwa sababu zipi.
Hili ni tatizo kubwa duniani na linasumbua watu wengi. Kupungua kwa ufanisi katika utendani wa shughuli mbalimbali ni miongoni mwa sababu zinazohusishwa na kutolala. Taasisi ya National Sleep Foundation ya Marekani, mwanzon mwa Februari ilitoa ripoti mpya inayoainisha saa za kulala kulingana na umri wa kila mtu. Ripoti hiyo imetokana na tafiti tofauti.
Kutokana na majibu ya utafiti huo mpya, sasa mtu anaweza kulala kwa muda unaofaa ili kuifanya afya iwe imara bila kujali kazi anayofanya, bali umri.
Ripoti hiyo ya kitaalamu iliyotolewa na jopo la wanasayansi na watafiti 18 kwa kupitia tafiti zaidi ya 300, inaonyesha kuwa watu wanapaswa kulala zaidi tofauti na ripoti za awali zinavyoeleza.
Hata hivyo, wengi hawafahamu ukweli huo ambao unaweza kuwa ndiyo sababu ya kufanya mambo yanayoweza kuhatarisha afya za jamii.
Usingizi ni moja ya mambo yanayoweza kuathiri afya ya mtu. Kulala zaidi au kutolala vya kutosha ni hatari kwa afya.
Hivyo ndivyo ukweli ulivyo kiafya, ingawa tatizo lililopo ni kwamba, wengi hawajui walale muda gani na kwa sababu zipi.
Hili ni tatizo kubwa duniani na linasumbua watu wengi. Kupungua kwa ufanisi katika utendani wa shughuli mbalimbali ni miongoni mwa sababu zinazohusishwa na kutolala. Taasisi ya National Sleep Foundation ya Marekani, mwanzon mwa Februari ilitoa ripoti mpya inayoainisha saa za kulala kulingana na umri wa kila mtu. Ripoti hiyo imetokana na tafiti tofauti.
Kutokana na majibu ya utafiti huo mpya, sasa mtu anaweza kulala kwa muda unaofaa ili kuifanya afya iwe imara bila kujali kazi anayofanya, bali umri.
Ripoti hiyo ya kitaalamu iliyotolewa na jopo la wanasayansi na watafiti 18 kwa kupitia tafiti zaidi ya 300, inaonyesha kuwa watu wanapaswa kulala zaidi tofauti na ripoti za awali zinavyoeleza.
Watoto walale muda gani?
Utafiti huo unaeleza kuwa watoto wachanga, wenye umri wa mwezi mmoja hadi miezi mitatu wanahitaji kulala kwa kati ya saa 14 mpaka 17.
Wenye miezi minne mpaka 11 wanatakiwa kulala kwa saa kati ya 12 mpaka 15, wakati wale wa mwaka mmoja na miwili wanahitaji saa 11 mpaka 14.
Wanafunzi chekechea hadi vyuo vikuu
Wenye umri wa kusoma chekechea, ambao ni miaka mitatu hadi mitano, wanahitaji saa 10 mpaka 13, wakati wale wa shule za msingi, wa umri kati ya miaka sita hadi 13, wanahitaji kati ya saa tisa mpaka 11 za kulala.
Wanafunzi wa sekondari, wenye miaka kati ya 14 na 17, wanashauriwa kutumia muda wa saa nane hadi kumi.
Wanafunzi wa vyuo, walio na umri wa miaka 18 mpaka 25, walale kwa kati ya saa saba hadi tisa. Muda huo pia unashauriwa kwa watu wazima, kuanzia umri wa miaka 26 mpaka 64.
Wazee
Utafiti huo ulitaka vijana walale kwa kati ya saa tisa na 10, wakati watu wazima pamoja na wazee walishauriwa kulala kwa kati ya saa 7 mpaka 8.
“Kulala muda mfupi au mrefu zaidi kuna madhara kwa afya. Magonjwa ya moyo, saratani na wakati mwingine matatizo ya kisaikolojia yanaweza kujitokeza na kuathiri ustawi wa mhusika,” anasema Profesa Lauren Hale kutoka Chuo Kikuu cha Stony Brook, Marekani ambaye ni mmoja kati ya waandaaji wa taarifa iliyotoa ripoti mpya.
Dk Syriacus Buguzi kutoka Hospitali ya Mwananyamala, wilayani Kinondoni, Mkoa wa Dar es Salaam anasema kuwa kutolala kwa muda wa kutosha kama inavyopendekezwa kuna madhara mengi kwa afya mtu, awe mtoto au mtu mzima.
Anasema kuwa matatizo hayo yanaweza kuwa ya muda mrefu au mfupi na kushauri jamii kuwa makini na ratiba za kila siku, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza na kuathiri mipango au shughuli za mhusika.
“Zipo dalili nyingi za mtu ambaye hakupata usingizi wa kutosha. Kukosa umakini kwa akifanyacho, kutomaliza kazi aliyonayo na kutokuwa na ufanisi. Hizo ni miongoni mwa dalili hizo. Hii hutokea kwa watu ambao hawakulala vya kutosha kwa muda mrefu,” anasema Dk Buguzi.
Anaongeza kuwa kwa watu wanaokesha kwa muda mrefu kwa mwaka au miaka kadhaa, wapo katika hatari ya kupata athari kubwa zaidi. Anafafanua kuwa hali hiyo huchangia msongo wa mawazo, ambao huathiri kinga za mwili.
“Baada ya muda mtu huyo huwa anaugua hovyo. Kinga zake zinakuwa dhaifu zisizoweza kushambulia vijidudu vyovyote vya magonjwa,” anaeleza na kufafanua kuwa suala la msingi ni kuchunga majukumu yasiingilie ratiba nyingine, ikiwamo kulala.
Maendeleo ya kiuchumi na kuongezeka kwa mahitaji ya familia kumezifanya familia nyingi kukosa muda maalumu wa kulala. Watu wa vijiji wanakosa muda kutokana na shughuli nyingi za uzalishaji mashambani au kufuata huduma kama maji, matibabu na elimu.
Siyo huko pekee, mijini hali ni mbaya zaidi. Pilikapilika za usafiri huwalazimu baadhi kuamka saa 10 alfajiri, ili kukwepa foleni za magari. Baada ya mchana kutwa kuwapo katika majukumu ya kiofisi, hujikuta wakilala saa nane usiku au zaidi. Muda hauwatoshi huku hiyo ikiwa ni ratiba yao ya mwaka mzima, wakati mwingine mpaka kustaafu kwao.
Wanafunzi wa mijni nao halikadhalika. Ugomvi na makondakta wa daladala huwapotezea muda mwingi na kuwachosha zaidi. Kazi za nyumbani walizonazo na michezo ya kitoto wanayotakiwa kushiriki huchukua muda wao mwingi na kupunguza ule wa kulala.
Wale wa vijijini hali ni hiyohiyo. Umbali mrefu kwenda na kutoka shule. Shughuli za shamba au ufugaji pia. Wakati mwingine utafutaji wa kuni, maji na hata chakula ni miongoni mwa shughuli ambazo huwagharimu.
Muda wa kulala unapunguzwa na shughuli hizo za kutwa nzima. Hawalali vya kutosha. Kazi haziishi kwa wakati, hivyo kulazimika kupunguza muda wa kulala ili kwenda sanjari na ratiba ya siku.
Wazee wenye umri wa miaka 65 na kuendelea wanashauriwa kulala kwa kati ya saa saba mpaka nane.
Muda huo unapendekezwa kwa watu wasio na dharura au wagonjwa. Katika hali kama hizo, muda unaweza kubadilika kulingana na mahitaji. Lakini haishauriwi kuzidisha saa mbili kwa watoto na saa moja kwa watu wazima.
Hata hivyo kumbukumbu zinaonyesha kuwa baadhi ya tafiti za awali ziliwahi kushauri tofauti.
Mfano; ripoti ya Taasisi ya Taifa ya Afya pia ya nchini Marekani, iliwahi kushauri kuwa watoto wachanga walale kwa saa 16 mpaka 18, chekechea walale kwa saa 11 mpaka 12 na wale wa shule za msingi walale walau kwa saa 10.
Ni kawaida kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kutumia muda mwingi zaidi kusoma nyakati za mitihani tofauti na ratiba zao za muhula mzima. Hata hivyo, hakuna ushahidi kuhusu matokeo yao.
Profesa Ernest Kitindi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema kuwa athari za usingizi zinategemea mtu husika.
Wapo wanaopenda kusoma usiku na wengine mchana. Baadhi kwenye kelele na wachache katika mazingira tulivu.
“Wataalamu wanashauri usiku wa siku ya mtihani wanafunzi wasisome, lakini wapo wanaosoma mpaka wakati wanapoingia kwenye chumba cha mtihani,” anasema.
“Hii ni muhimu zaidi kwa watoto kwani yule aliyelala vizuri tabia yake huonekana. Hawezi kufanana na wale wanaozurura mpaka usiku wa manane. Watoto wanaolala muda wa kutosha huwa na akili nzuri.”
Jeniffer Sumi, mkazi wa jijini Dar es Salaam, anasema kwamba kuna changamoto hasa kwa familia maskini kuwa na ratiba ya kulala kama inavyopendekezwa kitaalamu huku akianisha kipato kuwa ni kichocheo kikubwa cha kutofikia malengo hayo.
“Kwa familia bora ni suala linalowezekana. Wana ratiba za kulala, hasa kwa watoto wao. Kwa watu wasio na kipato cha uhakika, hilo ni jambo gumu kulitekeleza. Siyo jambo la kushangaza kukutana na mtoto anafanya biashara saa tatu au nne usiku…watoto kama hawa hawapati muda wa kutosha,” anasema.
Anafafanua kuwa kwa maeneo ya vijijini kuna changamoto nyingi zaidi kwani licha ya kutokuwa na uhakika wa mazingira bora ya kulala, lipo suala la ukubwa wa familia.
Anasema kuwa kwenye familia hizo vijijini unaweza ukakuta watoto watano wanalala kitanda kimoja, jambo ambalo haliwezi kuwapa wasaa wa kutosha.
“Wengi hawatumii neti za kuzuia mbu. Usiku kucha mtu anafukuza mbu, wakati mwingine gizani. Hata kama aliingia chumbani saa tatu usiku, unakuta muda aliolala ni mfupi kuliko ilivyopaswa,” anaeleza.
Jackline Paschal, mwalimu wa shule chekechea iliyopo Ubungo katika Manispaa ya Kinondoni, anasema kuwa kutokana na kutambua umuhimu wa usingizi kwa watoto, wao hutenga muda mwingi wa mapumziko kwao.
“Watoto wengi tunaowapokea wana umri chini ya miaka mitatu, uwezo wao wa kuzingatia masomo ni mdogo. Hivyo, huwa tunawapumzisha kwa saa tatu mpaka nne. Hii huwafanya wawe wachangamfu na kupenda masomo na walimu pia. Kwa namna hiyo, tunawajengea mazingira ya kupenda masomo,” anaeleza mwalimu Jackline.
Zipo athari nyingi zilizoshuhudiwa kama ajali za barabarani zinazopoteza maisha ya mamia na ambazo husababishwa na kusinzia kwa madereva wakati wanaendesha magari, tena umbali mrefu.
Kutokana na utafiti huo mpya ni muhimu kila mtu kutambua na kukumbuka kuwa kuna umuhimu wa kubadili mienendo yao umuhimu kwa kuwa na ratiba nzuri inayozingatia mapumziko ya mtu binafsi.
No comments :
Post a Comment