Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, March 3, 2015

RAIS KIKWETE ALIA KWENYE MSIBA!

Wimbo wa Komba wamliza Kikwete


Rais Jakaya Kikwete akiwa katika hali ya majonzi wakati wasanii walipokuwa wakiimba wimbo maalumu wa kumuaga Mbunge wa Mbinga Magharibi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Marehemu John Komba katika Viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Spika wa Bunge, Anne Makinda. Picha ndogo ni jeneza lililobeba mwili wa Komba. Picha na Anthony Siame 
KWA UFUPI
Wimbo huo uliobadilishwa maneno yanayohusu Mwalimu Nyerere na kuingizwa yanayomtaja mbunge huyo wa Mbinga Magharibi, mbali na Rais Kikwete ulimliza pia Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba na waombolezaji wengine.
Dar es Salaam. Wimbo wa John Komba aliouimba katika msiba wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999, jana uliibua majonzi na kusababisha viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Jakaya Kikwete, kutoa machozi ulipoimbwa kumuaga mbunge huyo.
Wimbo huo uliobadilishwa maneno yanayohusu Mwalimu Nyerere na kuingizwa yanayomtaja mbunge huyo wa Mbinga Magharibi, mbali na Rais Kikwete ulimliza pia Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba na waombolezaji wengine.
Sehemu ya mashairi ya wimbo huo uliokwenda kwa jina la “Nani Yule” ulioimbwa na wanamuziki mbalimbali wa bendi nchini, na kuwatoa watu machozi iliimbwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
“Kapteni Komba familia yako umeiacha na nani, chama chako umekiacha na nani, nenda baba msalimie Mwalimu, mweleze hali ya Watanzania ilivyo hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo hivi sasa hasa wakati huu, msalimie Mzee Kawawa Simba wa Vita”
Baadhi ya wanamuziki walioshiriki kuimba wimbo huo ni King Kiki, Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata, Jose Mara ambaye ni mwanamuziki wa bendi ya Mapacha Watatu na Luiza Mbutu wa African Stars.
Wakati wanamuziki hao wakiendelea kuimba wimbo huo, idadi ya watu wanaolia ilizidi kuongezeka, hasa wanafamilia ndugu na jamaa wa marehemu.
Waombolezaji walisikika wakilia huku wakisema, “Jamani alikuwa akitunga nyimbo kuwaimbia wenzake waliofariki dunia, sasa leo anaimbiwa yeye.”
Alipofariki Mwalimu Nyerere Oktoba 14, mwaka 1999, aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi, Komba akiwa na bendi ya TOT alitunga nyimbo za maombolezo ukiwamo wa “Nani Yule’, ‘Kwaheri Mwalimu’, ambazo jana zilitumiwa na wanamuziki kumuimbia yeye, wakibadilisha baadhi ya maneno.
Mwili wa mbunge huyo (61) aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita kwa ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu, uliagwa katika viwanja vya Karimjee ambapo salamu mbalimbali za rambirambi zilitolewa kabla ya mwili huo kusafirishwa kwenda Songea mkoani Ruvuma.
Hata wakati wa kuagwa mwili huo, idadi kubwa ya wabunge wenzake waliohudhuria walishindwa kujizuia kulia huku wakikumbushana ucheshi aliokuwa nao Komba enzi za uhai wake.
Pengine msiba huo utakuwa umewagusa wengi wanaomfahamu kwa mambo mengi, na kwa kuwa kipindi hiki nchi inajiandaa kupata rais mpya, kwa kuwa kazi yake kubwa ilikuwa ni kuipigia debe CCM kupitia uimbaji wake.
Kulingana na maelezo ya waombolezaji, Mwanajeshi huyo aliyestaafu akiwa na cheo cha kapteni alikuwa ni mtu ambaye hakusita kueleza kile alichokiamini, jasiri asiyekubali kushindwa, mcheshi wakati fulani na mtu wa kutoa misaada.
Kijana mmoja ambaye alishindwa hata kutaja jina lake kutokana na kulia kwa uchungu, alilazimika kuondolewa katika viwanja hivyo baada ya kutaka kwenda kuaga tena mwili wa mbunge huyo, huku akisisitiza kuwa ndiyo aliyekuwa akimsomesha.
“Kapteni jamani umeondoka, hivi nani atanisomesha mimi. Niacheni nikamuage kwa mara nyingine huyu ni kama baba yangu mzazi, nitakuwa mgeni wa nani,” alisema kijana huyo na kuzidisha vilio, hasa kwa watoto wa marehemu.
Watu kutoka maeneo mbalimbali walifika katika viwanja vya Karimjee kumuaga mbunge huyo kuanzia saa tatu asubuhi, akiwamo mama mmoja aliyedai kuwa ametoka mkoani Mwanza kuja kuuaga mwili wa mbunge huyo.
Huku akilia mama huyo alisema, “Komba baba nimetoka Mwanza kwa ajili yako jamani, nenda ndugu yangu, nenda tu ipo siku tutaonana.”
Shughuli hiyo ilianza saa 3 asubuhi kwa wanamuziki mbalimbali wa bendi, muziki wa kizazi kipya na waigizaji wa filamu kuimba nyimbo za kumkumbuka mbunge huyo.
Wakazi wa Dar es Salaam walimiminika katika viwanja hivyo na tofauti na shughuli nyingine kama hizo, hakukuwa na ulinzi mkali wala watu kukaguliwa na vifaa maalumu.
Mara baada ya viongozi wa Serikali kumaliza kuaga mwili wa mbunge huyo, wananchi wengine nao walipewa fursa ya kuaga na kusababisha askari wa Bunge kutumia nguvu ya ziada kuwazuia kutokana na kutofuata utaratibu uliowekwa.
Watu hao walionekana kuwa na shauku ya kuaga mwili wa mbunge huyo, baadhi wakilalamikia kitendo cha kuzuiwa na askari hao wakisema kuwa Komba alikuwa mtu wa watu na wao wana haki ya kumuaga.
Hata hivyo, baadaye askari hao waliwahimiza watu hao kufuata utaratibu uliokuwa umepangwa na wote wakapata fursa ya kuaga mwili huo hadi shughuli zilipomalizika saa 7:30 mchana.
Salamu za CCM
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema, “Sauti ya Komba imezimika lakini imefuatiwa na sauti ya vilio vya watu waliompenda wakiomboleza. Alikuwa mwalimu, mwanajeshi, kiongozi, mbunge, mwanasiasa na mwanamuziki mwenye kipaji cha kutunga nyimbo zinazoendana na wakati.”
Kinana alisema nyimbo zilizotungwa na Komba zilitumika kuwapa hamasa wanajeshi wa Tanzania waliopigana vita vya Tanzania na Uganda mwaka 1978 hadi 1979 vilivyouondoa utawala wa Iddi Amin nchini humo.
“Katika msiba wa Mwalimu Nyerere nyimbo alizozitunga ziliwaliza Watanzania, atabaki kuwa mfano wa kuigwa. Kifo chake ni pigo wa CCM, bendi yake, wasanii na wana familia yake,” alisema Kinana na kufafanua kuwa chama hicho kimetoa rambirambi ya Sh5 milioni.
Kambi ya Upinzani
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alisema kifo cha Komba kimewagusa wabunge wote bila kujali itikadi zao za vyama.
“Kifo hiki kinatukumbusha kuwa hapa duniani binadamu tunapita tu. Tunatakiwa kutenda mema kwa ndugu, rafiki na Taifa letu,” alisema.
Kamati ya Bunge
Mbunge wa Mchinga na Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ambayo Komba alikuwa makamu wake, Said Matanda alisema kuwa alizungumza na marehemu saa tano kabla ya kufikwa na mauti.
“Tulikuwa tukizungumzia safari ya kamati yetu kwenda Ethiopia ambayo ilikuwa tuifanye kesho yake (Jumapili iliyopita), lakini saa tano baadaye nikapata ujumbe kuwa amefariki dunia, sikuamini,” alisema.
Alisema marehemu alikuwa zaidi ya kiongozi kwa kutunga nyimbo zenye ujumbe mzuri kwa jamii na alikuwa na uzoefu wa miaka tisa katika kamati hiyo na ndiyo maana wajumbe wa kamati hiyo hawakusita kumchagua kuwa makamu mwenyekiti wao.
Salamu za Serikali
Akitoa salamu za Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu wa Bunge), Jenista Mhagama alimwelezea Komba kama kiongozi aliyejitolea katika kila jambo.
“Juhudi na mipango aliyoifanya Komba katika jimbo lake Serikali kupitia ilani ya CCM itatekeleza. Serikali itatoa rambirambi zake kwa familia ya Komba wakati mwafaka,” alisema.
Ujumbe wa Makinda
Spika Makinda aliwataka Watanzania kuwa na tabia ya kusamehe hata kama wametendewa mambo yanayowakwaza.
“Hapa duniani tunapita tu, hatutakiwi kuwatendea watu mambo ambayo sisi hatupendi kutendewa. Tusidhani kuwa kila tunachokitaka na kukiamini kitadumu, si hivyo. Komba ameondoka kama moto wa kibatali unavyozimika,” alisema.
Makinda alisema kama Komba angepewa dakika 15 za mwisho kabla ya kufariki ili aseme jambo lolote, ni wazi kuwa angesema kama kuna aliowakosea wamsamehe.
Alisema binadamu wote ni ndugu na hata wakifa inaelezwa na viongozi wa dini kuwa wanakwenda kukutana na raha au shida ambazo zinategemea na matendo yao waliyokuwa wakiyafanya duniani.
“Wanachama wa CCM tunamwombea marehemu na tunaamini kuwa Mungu atatupa Komba mwingine,” alisema.
Salamu za familia
Msemaji wa familia ya Komba, Dominick Mwakangale alisema mwili wa mbunge huyo ambao baadaye jana jioni uliagwa na wakazi wa Songea, utazikwa leo kijijini kwake Lituhi wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma.
Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.
Wengine ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) Jaji Damian Lubuva, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Hussein Katanga, Katibu wa Shughuli za Bunge John Joel, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Adam Kimbisa.
.

No comments :

Post a Comment