Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, March 31, 2015

Watengeneza printa ya aina yake Afrika Mashariki

> Meneja wa Maabara ya Buni Hub Jacquline Dismas akieleza namna printa ya 3D inavyofanya kazi hivi karibuni.Picha na Nuzulack Dausen. 
  • Kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki na Kati, Printa inayochapa kitu katika pande tatu maarufu kwa kiingereza kama ‘3D Printer’, imetengenezwa jijini Dar es Salaam katika kituo cha kukuza ubunifu na ujasiriamali cha Buni Hub.
Huenda isiwe inafahamika na Watanzania wengi, lakini mashine ya kwanza ya kuchapa vifaa vya maumbo mbalimbali, imeanza kutengenezwa nchini.
Kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki na Kati, Printa inayochapa kitu katika pande tatu maarufu kwa kiingereza kama ‘3D Printer’, imetengenezwa jijini Dar es Salaam katika kituo cha kukuza ubunifu na ujasiriamali cha Buni Hub.
Printa hiyo, yenye uwezo wa kutengeneza vifaa mbalimbali vya plastiki kutokana na usanifu wake, ilitengenezwa na timu ya wataalamu wa elektroniki na teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) baada ya kupatiwa ujuzi na mtaalamu kutoka Uingereza, Mathew Rogge.
Kwa wengi waliozoea printa za kuchapa karatasi watashangazwa na uwezo mkubwa wa printa hiyo inavyoweza kuuchapa mchoro uliopo kwenye kompyuta hadi kuwa kifaa pasina kukosea.
Baada ya wiki tatu za kuitengeneza, printa hiyo imeshatengeneza vifaa kadhaa vya plastiki vinavyoweza kutumika kama vipuri kutengenezea mashine nyingine ya namna hiyo.
“Mashine hii tulioitengeneza kwa kutumia mabaki ya vifaa vya elektroniki, inaweza kutengeneza vitu unavyoweza kuvishika na kuvitumia katika kazi mbalimbali kama vikombe, midori, sampuli za nyumba, viatu na vinginevyo,” anasema Meneja wa maabara ya Buni Hub, Jacqueline Dismas.
“Tunajaribu kwa hali na mali kuhakikisha mazingira yetu ni safi kwa kupunguza taka ambazo zinaweza ama kutumika tena au kutengenezwa upya.”
Ili kupata vifaa vya kuundia mashine hiyo, anasema iliwahitaji kuzunguka kwenye vituo vya kukusanya taka za kielektroniki kama printa, kompyuta na televisheni vilivyopo jijini hapa.
Matumizi ya taka hizo, zinazosaidia kupatikana kwa mota, chanzo cha nishati ya umeme (power supply) na reli za kujengea printa, yanasaidia kupunguza tatizo la taka ngumu na kujenga tabia ya kutunza mazingira.
Tofauti na printa zinazochapa karatasi ambazo hutumia wino kuchapa, printa za 3D zinatumia malighafi za plastiki, chuma, udongo, na nyinginezo ziitwazo ‘filament’ kuzalisha bidhaa tofauti kutokana na mahitaji.
Kuingia kwa teknolojia ya uundaji printa za 3D hasa kwa kutumia taka za kielektroniki, kutapunguza gharama za ununuzi wa mashine hizo zilizoanza kupata umaarufu ulimwenguni kwa kurahisisha kazi lukuki ambazo awali zilifanyika kiwandani.
Matumizi shuleni.
Kwa mujibu wa Jacqueline, baada ya kupata taaluma ya kuunda mashine hizo wana mipango mbalimbali ya kutengeneza bidhaa muhimu kwa jamii ambazo zimekuwa vigumu kupatikana sokoni.
“Moja ya miradi tunayotarajia kupitia printa za 3D ni kuanza kutengeneza vifaa vya kufundishia katika shule zote Tanzania.
“Hivi sasa shule zote za kata za sekondari zina maabara lakini zinakabiliwa na vifaa vidogo vidogo vya mazoezi kama gia katika somo la Fizikia ambavyo vinaweza kuzalishwa na mashine hizo,” anasema.
Anabainisha kuwa vifaa kama moyo au ubongo wa binadamu unaotumika kufundishia somo la Bailojia pia vinaweza kutengenezwa kirahisi.
Wastani wa bei ya Printa moja ya 3D ya kiwango cha chini ni takriban Sh2.5 milioni iwapo utaiagiza nje ya nchi.
Hata hivyo, kiongozi wa timu iliyotengeneza mashine hiyo Stanley Mwalembe, anasema gharama za jumla ya uundaji mashine waliyointengeneza zinafikia kati ya Sh150, 000 hadi 200,000.
Licha ya kwamba kwa sasa hawajaanza kuzalisha kwa ajili ya biashara, anaeleza kuwa bei ya reja reja inaweza isizidi Sh350, 000.
Mafanikio ya uingizaji wa teknolojia hiyo unafungua ukurasa mpya wa kuimarisha mfumo wa uchumi wa kibunifu na viwanda.
‘’Iwapo printa hizo mpya zikizalishwa kwa wingi zitatoa fursa lukuki kwa wajasiriamali wadogo kutengeneza bidhaa zao majumbani,’’ anabainisha Mwalembe.
Baada ya kupata teknolojia hiyo, Mwalembe ambaye pia ni mhadhiri wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam, (DIT) anasema wataanza kuzalisha printa za 3D kwa ajili ya kuuza reja reja kuwasaidia wajasiriamali.
“Mradi wa kwanza tunaoufikiri ni kuanzisha uzalishaji wa chupa ndogo za plastiki kwa kutumia mashine hizi hali kadhalika kuandaa malighafi (filament) inayotumika katika uzalishaji wa chupa hizo,” anaongeza.
Kwa sasa, anasema wanaweza kutengeneza printa hizo kwa oda maalumu na karakana yao ya nje ya kituo cha Buni ina uwezo wa kuzalisha hadi printa 500 za 3D kwa mwaka.
Kauli ya COSTECH
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), DK Hassan Mshinda anatoa hofu kwamba nia yao ni kuzitengeneza printa hizo na kuzigawa katika vyuo mbalimbali ili wanafunzi nao wajifunze kuzitengeneza.
“Sisi tunatazamia zaidi kuzalisha vitu vingine kama ‘drone’,” Drone ni ndege ndogo zisizo na rubani zinazotumika kufanya kazi tofauti ikiwemo kubeba mizigo, kupiga picha, ulinzi, na kazi nyinginezo,’’ anaeleza.
Kwa sasa, anabainisha kuwa wanataka kusambaza elimu ya teknolojia hiyo kwa wananchi waielewe, ili iwe rahisi kutumia fursa za mashine hizo kufanya ujasiriamali.
“Tunaamini vijana wengi watajifunza na hatuwezi kuepuka teknolojia hii kwa sababu ulimwengu wa viwanda unaelekea katika uzalishaji kwa kutumia printa za 3D,” anabainisha huku akisema zama za viwanda vinavyotoa moshi zimepitwa na wakati.

No comments :

Post a Comment