Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, April 15, 2015

Lini watawala watakuwa wasikivu kwa wananchi?


Usitishwaji huo wa Kura ya Maoni unatokana na kutokukamilika kwa zoezi la uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).
Msimamo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wa kusitisha kwa muda usiojulikana kufanyika kwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyokuwa imepangwa kufanyika tarehe 30 Aprili mwaka huu, umepokelewa kwa hisia tofauti miongoni mwa Watanzania.
Usitishwaji huo wa Kura ya Maoni unatokana na kutokukamilika kwa zoezi la uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).
Dalili za kutokufanyika kwa kura ya maoni zilianza kuonekana mapema baada ya idadi ya mashine 250 za BVR zilizokuwapo nchini kutowiana na idadi ya watu milioni 24 wanaokusudiwa kuandikishwa nchini kote.
Kwa muda mrefu makundi mbalimbali yenye ushawishi katika jamii kama vile wananchi wa kawaida; wasomi; wanasheria; taasisi za kidini; asasi za kiraia; wachambuzi wa siasa; wanaharakati; wafuasi wa vyama vya siasa na makundi mengine ya aina hiyo wamekuwa wakiishauri Serikali kuahirisha Kura ya Maoni.
Ni dhahiri kwamba mchakato wa kuandika Katiba Mpya umegharimu fedha nyingi.
Kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba na ukusanyaji wa maoni ya wananchi kwa nchi nzima kuliligharimu Taifa fedha nyingi ambazo hulipwa na walipakodi.
Uundwaji wa mabaraza ya kata na yale ya kitaasisi nako kuligharimu fedha nyingi. Fedha nyingi zilitumika wakati wa uendeshaji wa Bunge Maalumu la Katiba sambamba na uteuzi wa wajumbe wa Bunge hilo.
Sote tunakumbuka jinsi wananchi wengi walivyopinga ukubwa wa posho ya siku iliyolipwa kwa kila mbunge wakati wa vikao vya Bunge hilo Maalumu la Katiba.
Kadhalika iendelee kufahamika kwamba hadi sasa fedha nyingi sana zimetumika katika uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia mfumo wa BVR huko Njombe.
Zaidi ya hayo fedha nyingi zaidi zimetumika katika uchapaji na usambazaji wa nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa nchi nzima.
Wakati mabilioni hayo ya fedha yakiteketea kuna idadi kubwa ya Watanzania wasio na uhakika hata wa mlo mmoja kwa siku.
Vilevile kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaopoteza jamaa zao kwa kukosa fedha ya matibabu.
Ifahamike pia kwamba watumishi wengi wa umma na wale wa sekta binafsi wanaishi na kufanya kazi katika mazingira magumu sambamba na uduni wa mishahara yao.
Kwa nini fedha hizo zisingetumika kulipia ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wasio na uwezo wa kifedha? Je, lisingekuwa jambo la busara fedha hizo kuboresha huduma ya maji; elimu; afya; umeme na miundombinu.
Juhudi za wakulima
Sote tunafahamu juhudi kubwa inayofanywa na wakulima wetu na vilevile tunatambua ukosefu wa uhakika wa masoko ya mazao yao.
Je, isingependeza fedha hizo zikatumika kununua mazao ya wakulima wetu tena kwa bei nzuri.
Bado naendelea kuamini kwamba fedha hizo zingenunua: dawa nyingi za wagonjwa; pembejeo za kilimo; vifaa vya akina mama kwa ajili ya kujifungua; vitanda na mashuka ya wagonjwa; pamoja na vitabu vya wanafunzi.
Kadhalika fedha hizo zingetumika kufadhili waandishi wa vitabu na kugharimia tafiti mbalimbali pamoja na ujenzi wa maabara za sayansi.
Kwa ujumla fedha nyingi zinahitajika kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ni ukweli usiopingika kwamba miradi mingi ya maendeleo hushindwa kukamilika kwa wakati kwa sababu ya ukosefu wa fedha.
Nani anayebisha kwamba Watanzania wengi wanaishi kwenye nyumba za kupanga na hushindwa kujenga nyumba zao wenyewe kwa sababu ya uduni wa vipato vyao?
Lingekuwa jambo la kutia faraja endapo fedha hizo zingejenga nyumba za bei nafuu na kuwauzia wananchi hao.
Mtazamo wangu ni kwamba elimu yenyewe kuhusu maudhui ya Katiba Inayopendezwa bado haijatolewa katika kiwango cha kutosha.
Kadhalika licha ya zoezi la kugawa nakala za Katiba Inayopendekezwa kuna idadi kubwa ya Watanzania walioshindwa kupata nakala hizo.
Kwa upande mwingine iwapo Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa ingefanyika, Aprili 30 mwaka huu kulikuwa na kila uwezekano kwamba wananchi wengi wangepigia kura jambo wasilolifahamu sawasawa.
Kuna usemi mmoja wa kiungwana usemao “Kupanga ni kuchagua”. Bila shaka falisafa ya usemi huu inasisitiza umuhimu wa kutokukumbatia mambo mengi kwa wakati mmoja.
Vilevile naendelea kuamini kwamba falsafa ya usemi huu inaifundisha jamii kuhusu umuhimu wa kutokulazimisha mambo.
Unyumbulifu na usikivu ni jambo jema na la kiungwana. Mfano hai unaotetea hoja hii ni kwamba Serikali iliamua kufanya mambo mengi na mazito kwa wakati mmoja.
Baadhi ya mambo hayo ni: Suala la Vitambulisho vya Taifa ambalo bado linasuasua; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu; mchakato wa Katiba Mpya likiwemo zoezi la uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa BVR; usambazaji wa nakala za Katiba Inayopendekezwa; ufanyikaji wa kampeni na hatimaye kpigaji wa Kura ya Maoni ambao hata hivyo tayari umeahirishwa.
Machoni mwake, Serikali iliamini kwamba mambo hayo yote yangewezekana kwa wakati mmoja. Hiyo ilikuwa ni nadharia tu.
Badala yake uhalisia umethibitisha kwamba Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa haiwezi kufanyia April 30 mwaka huu! Yapo mambo mengi ya kujifunza kutokana na tukio hilo la kuahirishwa kwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa: Jambo la kwanza ni kwamba watawala wetu siyo malaika bali wana mazuri na mapungufu yao kama binadamu wengine.
Inapotokea wameonyesha udhaifu tusiwalaumu wala kuwanyoshea vidole bali tuwasaidie na kuwarekebisha. Pili; kukiri upungufu siyo kujidhalilisha bali ni njia ya kujiimarisha zaidi.
Upungufu wa mchakato
Tatu; turekebishe mapungufu yote yaliyojitokeza kwenye mchakato wa Katiba Mpya kwa lengo la kufanya maandalizi mazuri zaidi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Nne; tujifunze kuwa na upendo wa dhati pamoja na moyo wa usikivu.
Hii ni kwa vile baada ya maisha ya hapa duniani tutaulizwa na Mungu kuhusu jinsi tulivyozitumia karama na vipaji vyetu tulivyopewa ukiwamo uongozi!
Watanzania tusipoteze muda wa kulaumiana wala kutafuta mchawi. Kadhalika tusitazame tulipoangukia bali tutazame tulipojikwaa. Jukumu lililoko mbele yetu ni kumsaidia rais wetu amalize salama kipindi chake cha uongozi wa nchi.
Nawashangaa baadhi ya wanasiasa wanaoiponda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Baadhi ya wanasiasa hao wamekwenda mbali zaidi kwa kuitaka tume hiyo ya Taifa ya Uchaguzi iwajibike. Ufahamu wangu mdogo unanieleza kwamba tume hiyo ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hufanya kazi kwa kushauriana na Serikali. Haitoshi kwa mwanasiasa kuwa hodari katika utoaji wa matamko. Kinachotakiwa kwa mwanasiasa makini ni kuielewa kwa ufasaha dhana ya “uwajibikaji wa pamoja” kabla ya kutoa tamko la aina yoyote. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo!

No comments :

Post a Comment