Uamuzi huo wa Serikali umekuja baada ya Jukwaa la Wakristo kutoa tamko la kuwataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupigia kura ya hapana.
Serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, imetoa tamko kali la kutishia kuanza kutekeleza sheria inayodhibiti asasi za kijamii na kidini, ikizitaka taasisi hizo kuacha mara moja kutoa matamko yanayolenga kuwashawishi waumini wao waikatae Katiba Inayopendekezwa na pia kuwapangia nini cha kufanya katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua kali.
Uamuzi huo wa Serikali umekuja baada ya Jukwaa la Wakristo kutoa tamko la kuwataka waumini wake kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupigia kura ya hapana.
Kwa mujibu wa tamko hilo kutowasilisha hesabu za mwaka na kujihusisha na siasa ni ukiukaji wa sheria na adhabu yake ni kufutiwa usajili. Hatutetei uvunjaji wa sheria, lakini uamuzi wa Serikali unazua maswali mengi kuliko majibu.
Mfano kwanini uamuzi huu umekuja wakati kuna tamko la Jukwaa la Wakristo au sintofahamu kati ya Polisi na Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima.
Inawezekana uamuzi huu ni kukasirishwa na mtazamo wa taasisi za dini unaopinga na kuhamasisha waumini wake (si Watanzania wote) kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa. Kama huo ndiyo ukweli ni ipi nafasi ya viongozi wa Serikali, makada na taasisi zingine ambao wanahamasisha kura ya ndiyo kwa Katiba Inayopendekezwa.
Tunavyofahamu kura ya maoni inatumika katika demokrasia ili kuchagua viongozi wa nchi au kuamua kama sheria fulani itumike. Kawaida kura ya maoni hupigwa na wale wote wenye umri halali wa kupiga kura ili kukubali au kukataa pendekezo, sera, sheria, mabadiliko ya katiba, katiba mpya, kukataa au kumuunga mkono kiongozi fulani. Kura ya maoni huchukuliwa kuwa ni aina mojawapo ya demokrasia ya moja kwa moja.
Kwa hoja hiyo, viongozi wa dini walikuwa wanatumia haki yao ya kidemokrasia kutoa mawazo yao, kama wanavyofanya wengine wanaohamasisha kura ya ndiyo kwa Katiba Inayopendekezwa.
Lakini sote ni mashahidi kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83. Sheria hii inatamka aina tatu za Wajumbe wa Bunge la Katiba, Wabunge, Wawakilishi na Wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali 10 wanaotajwa na Kifungu na. 22(1c) cha sheria hiyo. Ndani yake kuna kundi la Taasisi za Kidini lenye wajumbe 20.
Tunaamini na ndivyo ilivyo wajumbe 20 kutoka taasisi za kidini, waliteuliwa kwenda kujadili na kulinda maslahi yao ndani ya Bunge la Katiba, na ndiyo maana masuala ya mivutano ya kidini, mfano Mahakama ya Kadhi, yalijadiliwa kwa upana wake kuanzia kwenye kamati hadi ndani ya Bunge zima.
Baada ya Bunge kumalizika wajumbe wote zikiwemo taasisi za kidini walirudi kwenye maeneo yao kupeleka mrejesho, kuna makundi hayakuridhika kwa sababu mambo yao mengi yalitupwa na kuna makundi yaliridhika na walichopata. Ubaya uko wapi kwa wanaoipinga Katiba Inayopendekezwa. Ndiyo maana kwenye Kura ya Maoni kuna ‘ndiyo’ na ‘hapana’. Kama Serikali inataka watu wote wapige kura ya ndiyo hakuna maana ya kutumia fedha nyingi kuitisha Kura ya Maoni.
Tunaiomba Serikali iache demokrasia ishamiri, Wajumbe wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba wana haki ya kusema hapana au ndiyo kwa makundi yao. Makundi hayo ndiyo yaliyowatuma bungeni.
No comments :
Post a Comment