Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema kuwa wananchi waliopewa nyumba za maendeleo za Serikali na Rais wa kwanza wa Serikali ya Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume wataendelea kuishi bure lakini watakapokufa wazee hao warithi wao watalazimika kulipa kodi kama Serikali ilivyoagiza.
Hayo yamesemwa leo katika ukumbi wa jengo la wasanii liliopo Rahaleo Mjini Zanzibar na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhani Abdalla Shaabani wakati alipokuwa akizungumza na wakaazi wa nyumba hizo.
Amesema kuwa watoto wa wamiliki wa nyumba hizo wataendelea kuishi humo bila ya kubughudhiwa na mtu yoyote na jambo la muhimu ni kufuata agizo la Serikali juu ya kuzitunza na kufuata sheria zilizowekwa ili nyumba hizo ziweze kudumu kwa muda mrefu.
Amesema Serikali ya Mapinduzi tayari imeshapitisha maamuzi baada ya kukutana katika vikao vyake na kuamua kuwa wakazi hao pamoja na wazee wao watakaa ndani ya nyumba hizo bila kulipa kodi lakini kwa upande wa warithi watalazimika kulipa kodi iliopangwa na Serikali ambayo itaaza rasmi ifikapo mwezi wa saba mwaka huu.“Uamuzi wa Serikali kwa watu waliothibitika kupewa nyumba na Mzee Abeid Amani Karume wataendelea kukaa bure, lakini mara tu watakapo kufa wazee hawa warithi wao watalazimika kulipa kodi na huo ndio uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar” aliesma Waziri huyo.
Aidha amewataka wananchi wanaokaa katika nyumba hizo kwenda kuchukua fomu za mikataba kuanzia sasa na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kuenzi juhudi za Mwanapinduzi huyo na kuzilinda, kuzienzi na kuthamini mchangowake kwa Taifa la Zanzibar.
Nae aliyekuwa Mke wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume amesema kuwa Mzee Karume katika uhai wake aliishi miaka saba tu baada ya Mapinduzi ambapo alijenga nyumba za maendeleo na aliwapa watu wasiojiweza kimaisha kukaa nyumba hizo, lakini leo hii kuna watu wanaojaribu kuwapotosha watoto wao kukaa humo bila ya malipo ya kodi ameongeza kwa kusema kuwa kwa hivi sasa karibu ulimwengu mzima wananchi wanakaa katika nyumba za serikali kwa kulipia kiwango kidogo cha kodi.
Nae mmoja wa wakaazi wa nyumba hizo za maendeleo Bi Zamzam amesikitikia kuwepo kwa kodi hiyo hivi sasa na kusema kuwa yeye itamwiya vigumu kulipa kwani hali yake ni mzee, masikini, na hana kazi ya kufanya, hivyo serikali iliangalie na hilo kwa watu wenye hali kama yake kwa kuwasaidia juu sualazima la ulipaji.
Chanzo: ZanziNews
No comments :
Post a Comment