NA MHARIRI
3rd May 2015
Tunayo kila sababu ya kumpongeza Rais wetu kwa jinsi ambavyo serikali yake ya Awamu ya Nne ilivyojitahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi nchini, hasa katika eneo la maslahi yao.
Katika kipindi cha uongozi wake ambao unakaribia kufikia tamati Oktoba mwaka huu, imekuwapo mivutano mbalimbali kati ya serikali na wafanyakazi ambayo wakati mwingine iliambatana na migomo kudai maslahi yao.
Hata hivyo, ni dhahiri kuwa vitisho vya mwajiri na migomo ya wafanyakazi haiwezi kuwa suluhisho la kuondoa kero za wafanyakazi, hasa kutokana na ukweli kwamba hupunguza ufanisi.
Na kwamba ni lazima tutambue na kukubali kuwa ufanisi sehemu za kazi hutegemea uhusiano uliopo baina ya wafanyakazi na waajiri.
Nyongeza ya mishahara ndilo dai kuu limekuwa mara nyingi linashikiwa mabango hasa pale zinapofanyika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambapo ilizoeleka kuwa serikali ilikuwa na wajibu wa kutekeleza hilo kama motisha katika kuongeza ufanisi katika uzalishaji.
Katika sherehe za Mei Mosi juzi, wafanyakazi nchini walikuwa na shauku kubwa ya kusikia kutoka kwa Rais Kikwete nyongeza mpya ya mishahara, pengine kufikia kile kiwango cha kima cha chini cha sh. 350,000 ambacho kilipendekezwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA). Moja ya bango lilisomeka ’Shemeji unatuachaje?’
Rais Kikwete aliweka bayana kwamba mambo mengi amejitahidi kuyatekeleza chini ya uongozi wake na mengine anaamini yatakamilishwa na Rais ajaye.
Hata hivyo, tunayo kila sababu ya kumpongeza Rais wetu kwa jitihada zake za kuwajali wafanyakazi nchini katika kipindi cha uongozi wake unaomalizika mwishoni mwa mwaka huu.
Kwa mfano, katika sherehe kama hizi mwaka jana, Rais Kikwete aliwaambia wafanyakazi kwamba kama serikali yake ilivyoahidi mwaka juzi, iliweza ilipandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa Umma kwa asilimia 41. Kwa ongezeko hilo, kima cha chini cha watumishi wa umma kiliongezeka kutoka shilingi 170,000 hadi shilingi 240,000.
Nyongeza hii peke yake iliifanya Serikali kutumia asilimia 44.9 ya bajeti ya Serikali kulipa mishahara na asilimia 10 ya pato la taifa (GDP), kiwango ambacho ni kikubwa, lakini kwa kuwa ina dhamira ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake, imekuwa ikilipa fedha hizo. Kwa vigezo vyo vyote vile, kiwango hiki ni kikubwa mno hivyo ni kielelezo thabiti cha dhamira njema ya serikali kujali wafanyakazi nchini.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2005 kima cha chini cha mshahara kilikuwa shilingi 65,000 kwa mwezi, hivyo ndani ya miaka saba kiliongezeka karibu mara nne ya ilivyokuwa na kufikia kima cha chini cha sasa. Hii, hakika ilikuwa dhamira nzuri ya serikali.
Mwaka huu 2015, ingawa serikali ilidhamiria kuongeza, lakini yapo mambo mengi yamejitokeza ikiwa ni pamoja na kuporomoka kwa shilingi yetu, huku dola ya Marekani ikipaa.
Hali ya uchumi wa dunia imechangia kwa kiwango kikubwa kutetereka kwa uchumi wa nchi yetu pia. Shilingi yetu imeonyesha kutokuwa imara na hivyo kulazimisha uchumi kuyumba.
Hata hivyo, kiashiria hicho na vingine ni lazima vitufumbue macho na kujipanga sawasawa katika kuboresha uchumi na nchi yetu kupunguza utegemezi ambao mara nyingi umeambatana na masharti magumu.
Kwa hiyo, lazima sote wafanyakazi kwa ujumla wetu tufanye kila tuwezalo kufanya kazi kwa bidii, kuongeza tija na uzalishaji sehemu za kazi ili kumwongezea mwajiri kipato na uwezo wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Rais JK amejitahidi, mengine tuyafanyie kazi, tuache mazoea na kusubiri kulalamika wakati tunaweza kula matunda ya mikono yetu.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment