Katika Mkoa wa Pwani, Lowassa alipata jumla ya wanachama wa CCM 78,500 waliojitokeza kumdhamini kutoka katika wilaya sita za mkoa huo.
Akimkaribisha Lowassa, kuwashukuru wanachama wa Mkoa wa Pwani waliojitokeza kumdhamini katika harakati zake za kusaka urais, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Maulid Bundala, alisema Halmashauri Kuu ya chama hicho (Nec), Kamati Kuu (CC) na Mkutano Mkuu, umfikirie Lowassa kama anatosha na apitishwe.
Alisema CCM inatakiwa kuangalia maslahi ya chama kwanza na si matakwa ya watu binafsi.
“Mimi tangu tarehe 7 mwezi huu nimefanya ziara katika wilaya zote na kila nilipopita wananchi walisema apelekwe Lowassa kwani anaweza kutatua changamoto zao, wanakujua wewe ni mchapakazi,” alisema Bundala.
Aliongeza: “Wananchi wa Mkoa wa Pwani walisema watakupigia kura Lowassa kutokana na kujenga shule na baadhi ya mambo uliyoyatekeleza kipindi ukiwa Waziri Mkuu."
Kwa upande wake, Lowassa alisema anawashukuru wana-CCM kwa kumdhamini na kusema endapo akipata ridhaa atahakikisha anaboresha Hospitali ya Tumbi pamoja na huduma ya maji.
Alisema katika suala la barabara, atahakikisha analishughulikia katika kipindi cha mwaka mmoja.
Awali, akiwasalimu wanachama wa mkoa huo, Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Dk. Peter Mwamasika, alisema ni lazima atafutwe kiongozi aliyekamilika kiroho, kiafya, kisiasa, kiuchumi na kielimu.
Alisema nchi kama inataka kuondokana na unyonge, umaskini na magonjwa, inahitaji kiongozi kama Lowassa.
CHANZO: NIPASHE

No comments :
Post a Comment