Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama hicho Said Miraaj, alisema baada ya kukabidhiwa kadi na kutangaza nia ataanza ziara yake ya kujitambulisha kwa wananchi.
Alisema mpaka sasa watia nia waliojitokeza kuomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kwa upande wa Zanzibar ni Hamad Rashid pekee.
Miraaj alisema bado milango haijafungwa na kuwaomba watu wengine wanaohitaji kuwania nafasi hiyo kwa upande wa Zanzibar wajitokeze kwa kuwa mwisho wa siku chama ndicho chenye maamuzi ya mwisho ya nani agombee na nani asigombee kulingana na sifa zao.
Kwa upande wa Tanzania Bara, Miraaj alisema tayari wameshajitokeza wagombea watatu wa nafasi ya urais ambao nao wanataraji kutangaza rasmi nia yao hiyo mwezi ujao.Aliwataja watangaza nia hao kuwa ni Abubakari Lakeshi, Emmanuel Faustine na Lutalosa Yemba (maalufu kwa jina la Chifu Yemba) ambao nao baada ya kutangaza wanatarajia kuzunguka mikoa mbalimbali kujitambulisha kwa wananchi mwezi ujao.
Pia alisema pamoja na kujitokeza kwa watia nia hao, lakini bado wanapokea watia nia wengine watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo ndani ya ADC.
Miraaj alisema Chama kimeweka utaratibu wa kuwasaidia watia nia wa nafasi ya urais katika kulipia gharama zote zitakazotumika wakati wanatangaza nia ili kuepusha kuonyeshana ubabe kati ya watia nia hao walio nacho na wasio nacho.
Kwa upande wa nafasi ya Ubunge, Miraaj alisema chama kimepanga kusimamisha wabunge zaidi ya 100 na kwamba mpaka sasa watu waliojitojeza kuwania nafasi hiyo katika majimbo mbalimbali nchini ni zaidi ya 80.
CHANZO: NIPASHE

No comments :
Post a Comment