Waziri mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa Semina ya Urithi na Utamaduni wa Tanzania. Kushoto ni mkurugenzi wa taasisi hiyo kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM), Profesa Abdallah Bujra.
Dk Salim alisema hayo jana baada ya kufungua semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Utamaduni na Urithi kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM).
Alisema demokrasia katika vyama vya siasa imezidi kukua na kwamba kikubwa kinachotakiwa ni kutumia njia bora na siyo kurushiana maneno ambayo hayana msingi.
“Utakuta viongozi wa vyama wenyewe kwa wenyewe wanarushiana maneno, huyu hafai mara siyo raia wa nchi hii, sasa haya mambo kwenye siasa hayatakiwi.
“Ni lazima kila kiongozi wa chama cha siasa atambue wajibu wake katika jamii,” alisema Dk Salim.
Pia maadili ya viongozi katika Taifa yameporomoka, hivyo aliwaasa wananchi kuchagua viongozi bora kwa masilahi ya Taifa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu.
“Sasa kiongozi anagombea nafasi fulani kwa masilahi yake binafsi, siyo kwa wananchi na anawaomba wampigie kura,” alisema Dk Salim.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu na kuilinda amani katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Katika semina hiyo ya Urithi na Utamaduni wa Tanzania alisema nchi ina urithi lakini haujapewa kipaumbele.
Alisema suala la uchumi na maendeleo ndilo lililopewa kipaumbele.
Hata hivyo, alisema jamii haijachelewa na inaweza kuweka mikakati itakayofanya jambo fulani kutambulika zaidi.
Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Profesa Abdallah Bujra alisema semina hiyo itakuwa ya siku tatu.
Alisema Taifa haliwezi kupiga hatua bila suala hilo kutiliwa mkazo.
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment