Wazazi wa wanafunzi hao waliofika kwenye ofisi za The Guardian zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, walieleza mazingira tofauti ya kutoweka kwa watoto wao akiwamo huyo aliyeacha ujumbe kwa baba yake.
Katika tukio la kwanza, mwanafunzi wa kidato cha tatu, Murtaza Petro (16) wa Shule ya Sekondari Mikwambe, ametoweka nyumbani na kumwachia baba yake ujumbe unaosomeka:
“Baba samahani mimi naondoka kwa sababu walimu wamenikasirisha wamenipiga mno bila kithibitisho wakasema nimekaa chimbo wakati sio kweli,’ baada ya maelezo hayo aliikunja na kuandika juu yake kuwa,
“Sio kwamba sipendi shule bali kitendo nilichofanyiwa.” Baba mzazi wa mtoto huyo, Petro Murtaza, alisema mwanae alitoroka nyumbani Mei 16, mwaka huu na kwenda kusikojulikana.
Alisema siku moja nyuma Murtaza aliadhibiwa na walimu wake kwa kosa la kwenda kukata nywele kwenye eneo ambalo shule imezuia.
Petro amemuomba mtoto wake popote alipo arudi nyumbani ili aendelee na masomo yake na kuomba yeyote atakayemuona apige simu namba 0757 877588 au atoe taarifa kituo chochote cha polisi.
Katika tukio la pili, mwanafunzi wa darasa la nne, George Afumba (11) katika shule ya Msingi Atlas, jijini Dar es Salaam, naye ametoroka nyumbani mara baada ya kutumwa na mzazi wake akachukue nyanya gengeni.
Mama mzazi wa mtoto huyo Agnes Afumba alisema kuwa mtoto wake alitoroka wiki iliyopita na kwenda kusikojulikana.
Alisema mtoto huyo amekuwa na tabia za kutoroka nyumbani mara kwa mara na alipokamatwa hudai alikuwa kwenye michezo.
Alisema mara ya mwisho kutoroka ilikuwa ni mwezi wa Aprili ambaye alikaa mtaani kwa muda wa siku tatu na kukutwa kwenye baa ya Mango Garden akiangalia televisheni.
Mama huyo ametoa mawasiliano yake kwa yeyote atakayemuona ambayo ni 0684 693754 au 0688 200218.
Katika tukio la tatu, mwanafunzi wa kidato cha pili, Boniface Bilimu (15) katika Shule ya Sekondari Kibwegere, ametoweka nyumbani Ijumaa iliyopita akidai kuwa anaelekea shuleni kwenye masomo ya ziada.
Mama mzazi Rehema Bilimu aliliambia gazeti hili kuwa, siku ya tukio mtoto wake aliondoka akiwa hajavaa sare za shule huku akiaga kwenda shule.
Ameomba yeyote atakayemuona wapige simu namba 0756 037762.
Wakati huo huo, Mwanafunzi wa Shule ya Awali, Qusay Nyambi (5) katika shule ya Jeshi la Wokovu huko Tabora, ametoweka nyumbani muda mfupi wakati akicheza.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, Gaudensia Ngongi, mkazi wa Makongo Juu, mtoto huyo ambaye alikuwa akiishi na baba yake mzazi huko Tabora, siku ya tukio alionekana akichezea tairi na alipolirejesha ndani alitoka na kwenda kusikojulikana.
Ameomba kwa yeyote atakayemuona apige simu namba 0752 565656.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment