Mwenyekiti wa ACT, Anna Mghwira
Mshauri wa chama hicho, Profesa Mkumbo alisema wameamua kumpitisha Mghwira kwa kuwa anazo sifa za kuwania urais.
Dar es Salaam. Hatimaye Chama cha ACT – Wazalendo kimempitisha mwenyekiti wake, Anna Mghwira (56) kuwania urais baada ya mshauri wake, Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa amechukuliwa fomu kukataa kubeba jukumu hilo.
Sambamba na Mghwira, mkutano mkuu wa chama hicho uliokutana jana ulimpitisha Hamad Mussa Yusuf kuwa mgombea mwenza.
Chama hicho kimefikia hatua hiyo baada ya kusota kwa siku kadhaa kutafuta mgombea na pigo kubwa lilikuwa juzi baada ya Profesa Mkumbo kukataa.
Akisoma maazimio ya Halmashauri Kuu katika mkutano mkuu jana usiku, mshauri wa chama hicho, Profesa Mkumbo alisema wameamua kumpitisha Mghwira kwa kuwa anazo sifa za kuwania urais.
Alisema mwenyekiti huyo anao uwezo na sifa za kuwa rais, kwa kuwa kazi za rais ambazo ni kufikiri, kuwa mlinzi mkuu wa umoja, tunu za Taifa na kuwa mfano bora wa ubinadamu anazimudu.Alisema Mghwira anaweza kufikiri na amekuwa akiandika makala mbalimbali, jambo ambalo baadhi ya wagombea hawaliwezi kwa kuwa hata hotuba wanaandikiwa.
Baada ya kumtangaza, wajumbe wa mkutano huo walishangilia kwa mbwembwe kumpata mgombea huyo.
Kwa uteuzi huo, Mghwira atalazimika kuachia ule wa awali wa kuwania ubunge katika Jimbo la Singida Mjini na atakuwa na kibarua ya kutafuta wadhamini nchi nzima na kukamilisha kazi hiyo kabla ya kurejesha fomu kwa muda aliopangiwa wa saa 7.30 mchana leo.
Akiwashukuru wajumbe wa mkutano huo, Mghwira alisema Taifa linahitaji kiongozi mwenye moyo wa nyama, mwenye upendo, uadilifu na mwenye uwezo wa kuwaunganisha watu wote bila upendeleo.
Alisema wamechelewa kumtangaza mgombea kwa kuwa walikuwa wanatafakari kauli ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya “Ikulu ni mahali patakatifu”, hivyo wamempata rais mtakatifu.
Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe alisema ilani ya uchaguzi ya chama hicho imejikita katika mambo matano ambayo ni hifadhi ya jamii, elimu, afya, ajira na utalii.
No comments :
Post a Comment