Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku akizungumza wakati wa Mdahalo kuhusu umuhimu wa maadili katika kuimarisha amani, umoja na haki uliofanyika, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeulea mtandao wa watu wasiopungua 10 ambao unaendelea kukitesa ndani na nje.
Butiku alisema hayo jana kwenye mdahalo wa maadili katika kuimarisha amani, umoja na haki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 ulioandaliwa na MNF na kubainisha kuwa mtandao huo usio na imani na CCM upo tangu kabla ya mwaka 1990.
“Wanasema ndani ya chama kuna mizengwe, hawataki utaratibu, hawataki waulizwe maswali, wanataka mambo yaendeshwe kiholela… wanasema tunachelewa kutajirika, sasa kama walikuwa wanajua hilo kwa nini hawakutoka tangu mwaka 1992,” alihoji Butiku na kushangiliwa.
Alisema Mwalimu Julius Nyerere aliwaruhusu mapema kuondoka CCM lakini walitega na wameendelea kukaa ndani ya chama huku wakivuruga kwa kutumia agenda ya vijana tangu miaka ya 1990.
“Hata Rais alipochaguliwa (Jakaya Kikwete) alisimamishwa na vijana Morogoro wakamwambia tumechoka. Sasa ndiyo maisha bora, sasa kuna maisha bora?” alisema Butiku na kuwataka wananchi watazame masilahi yao.
Alisema kwa sasa CCM ni kama kimejengwa katika mazingira ya kuyumba na kosa walilofanya waliotoka sasa na wanaoendelea kutoka ni kubaki ndani ya chama kwa miaka yote hiyo wakati hawakubaliani nacho.
Butiku alimwambia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula aliyehudhuria mdahalo huo chama hicho kilifanya makosa kutoudhibiti mtandao huo tangu awali na kwamba kimeuvumilia na sasa unakisumbua.
Awali, Butiku alisema mdahalo huo wa tisa ni wa mwisho kwa mwaka huu kabla ya Uchaguzi Mkuu kwa kuwa kuendelea kufanya mijadala kutavuruga mwenendo wa kampeni zitakazoanza Jumamosi.
Alisema: “Wananchi wasikubali mtu awazuie kwa namna yoyote ile, ya chini au ya juu, wazungumze mambo yao.”
Kwa upande wake, Mangula alisema CCM siku zote inasimama kwenye misingi ya kanuni na taratibu na yeyote anayekiuka anashughulikiwa, akitolea mfano chama kilivyowafungia makada wake sita kwa miezi 12 baada kuanza kampeni za urais mapema.
Akitoa mada juu ya maadili katika taasisi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alisema uchaguzi wa mwaka huu una mwamko mkubwa miongoni mwa Watanzania, hivyo yanahitajika maadili ya kiwango kikubwa ndani ya taasisi zinazohusika.
Profesa Baregu alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inatakiwa kufanya kazi kwa weledi kwa kuweka bayana yanayoendelea katika uandikishaji kwa kuwa hadi sasa kuna hofu ya kuchakachua idadi ya wapiga kura.
“Ninavyozungumza sasa hivi sijui NEC imefika wapi katika uandikishaji na tayari kuna watu wengine wanasema zile takwimu za waliojiandikisha zimeongezwa, siyo halali,” alisema Profesa Baregu.
Alieleza kuwa hivi karibuni alipokwenda kuhakiki jina katika kituo alichojiandikishia alikuta fomu za waliojiandikisha zikiwa zimezagaa bila uangalizi maalumu, jambo linalotishia usalama wa taarifa za mpiga kura.
Baada ya baadhi ya wachangiaji kuzungumzia kwa kiasi kikubwa ujio wa Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ndani ya Chadema na kuhusisha na suala la maadili, Profesa Baregu alifafanua namna walivyopishana kumpokea kiongozi huyo na kwamba haikuwa rahisi kujiridhisha juu ya maadili yake.
Jaji Mstaafu, Amir Manento alisema suala la maadili linategemea mtu binafsi na taasisi kwani mtu anaweza akawa msafi na akafanya kazi katika ofisi isiyo na uadilifu, akaambukizwa.
Kuhusu Uchaguzi, Jaji Manento alisema NEC ikiamua kuvuruga amani kwa kuacha kufuata maadili inaweza kwa kuwa hadi sasa kuna taarifa za watu 125 wenye vitambulisho lakini majina yao hayaonekani kwenye uhakiki.
“Kwa bahati mbaya tume ipo juu sana, inapelekewa tu matokeo kutoka kwa wakurugenzi wa wilaya ambao ni watumishi wa Serikali na ni rahisi kwao kufanya matokeo yachakachuliwe. Hivyo, kuzuia hayo, vyama vya siasa viruhusiwe kupeleka wawakilishi wao ili taarifa zinazokwenda makao makuu ziwe sahihi,” alishauri.
NEC yafafanua
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Kombwey alisema amesikitishwa na kauli iliyotolewa na Profesa Baregu katika mdahalo huo na kusema taarifa hizo siyo sahihi na kusisitiza kuwa yeyote mwenye pingamizi dhidi ya maadili ya mgombea apeleke ushahidi wa maandishi Agosti 21.
“Taarifa alizozitoa siyo sahihi na za upotoshaji. Ni kauli hatari kuelekea Uchaguzi Mkuu, niwaombe wanasiasa na wanazuoni kujiepusha na kauli za hatari zisizokuwa na usahihi wowote,” alisema Kombwey na kusisitiza kuwa hakuna fomu zinazozagaa kwa kuwa huwa ‘zina-scaniwa’ (kunakili na kusafirisha maandishi kielektroni) wakati wa uandikishaji.
Aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole alisema kamwe hataacha kuongea ukweli juu ya viongozi wasio na maadili na yupo tayari kuonekana anaegemea upande fulani.
“Sipendi siasa za kihuni. Sioni hasara kuwa kutokuwa sehemu ya siasa hizo… tajiri akiwa rais wetu hatakuja kutumia utajiri wake kwa ajili yenu maskini. Tajiri ni tajiri tu awe CCM au Ukawa,” alisema Polepole.
Mmoja wa watoa mada katika mdahalo huo, Mohammed Mshamba alisema kauli za viongozi za “tutashinda hata kwa bao la mkono” na “hatuwezi kukubali kuachia nchi kwa karatasi” ni za hatari zinazotakiwa kukemewa kabla ya kuleta maafa.
No comments :
Post a Comment