NA EDITOR
7th August 2015
Jumanne wiki hii katika safu ya tahariri tulitoa rai yetu kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba kijitenge na uchafu ambao umeshuhudiwa na umma katika mchakato wa kura za maoni.
Tulisema hayo baada ya kupokea taarifa za kutapakaa kwa vitendo vya rushwa kwenye majimbo mbalimbali ya uchaguzi ambako kura za maoni zilipigwa Jumamosi ya Agosti mosi, mwaka huu.
Tulitoa rai hiyo kwa kuwa pamoja na ukweli kwamba kulikuwa na maeneo ambayo kura za maoni zilipigwa kama zilivyopangwa, viashria vya rushwa na ukiukaji wa taratibu za uchaguzi zililalamikiwa kwa kiwango kikubwa na wanachama wa CCM kiasi cha wengine kuamua kufanya vurugu, kama vile kuchoma karatasi za kura na hata kuvunja ofisi za chama.
Tulitafakari maana ya kasoro hizo na tukanona kimsingi ni mikakati iliyokuwa inasukumwa na nguvu ya rushwa ya baadhi ya makada wa chama hicho ya kutaka kupitisha wagombea kwa hila. Tulionya kwamba chama tawala, chama kikongwe kama CCM hakistahili kukumbatia uchafu kama huo.
Tulitoa mfano kwamba ni jambo la fedheha kubwa kwa watendaji wa CCM wenye uzoefu wa miaka na miaka wa kusimamia uchaguzi kuruhusu karatasi za kura ambazo zimekwisha kupigiwa baadhi ya wagombea kuingizwa kwenye masanduku ya kura.
Wakati tukiendelea kushangaa mwenendo huo usiofaa, juzi tulipata mshituko mkubwa baada ya kuelezwa na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (Zaeca), kuwa imewakamata makada kadhaa wa chama hicho, wakituhumiwa kugawa rushwa ya fedha, nguo na wengine kuunganishwa umeme kwenye nyumba zao.
Wakati tukiendelea kushangaa mwenendo huo usiofaa, juzi tulipata mshituko mkubwa baada ya kuelezwa na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (Zaeca), kuwa imewakamata makada kadhaa wa chama hicho, wakituhumiwa kugawa rushwa ya fedha, nguo na wengine kuunganishwa umeme kwenye nyumba zao.
Mkurugenzi wa Zaeca, Mussa Haji Ali, aliiambia Nipashe kuwa makada wengi wakiwamo vigogo wa chama hicho wanatuhumiwa kutoa rushwa katika mchakato huo.
Alisema maofisa wake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waliwakuta wanasiasa hao kwenye maeneo mbalimbali wakitoa rushwa kwa wana-CCM na viongozi wa matawi wa chama hicho.
Uchunguzi wa Zaeca dhidi ya makada hao unaendelea na ukikamilika, watawasilisha majalada ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa ajili ya kufungua mashitaka.
Kwa mujibu wa Zaeca, ushahidi walionayo dhidi ya makada hao ni pamoja na kurekodiwa sauti zao, picha za mnato na picha za video.
Matukio haya kwa ujumla wake yamegeuza uchaguzi kuwa gulio la kuuza kura na mwenye fedha anafika kuzinunua kulingana na bei ya soko. Ndiyo maana wapo watu wamehongwa Sh. 5,000, wengine 10,000, kundi jingine 100,000 na hata milioni moja.
Inaumiza sana akili kuona kwamba mchakato wa kidemokrasia wa kutafuta wagombea uongozi wa kuchaguliwa umegeuzwa kutoka fursa ya wananchi kuwachagua viongozi wao, kuwa gulio la wenye fedha kuwanunua wananchi.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba hali hii imekubalika kama sehemu ya maisha ya wananchi. Hakuna anayeona haya au kinyaa kulipwa Sh, 5,000 ili atoe kura kwa mlipa fedha. Ni aibu kubwa!
Ni jambo la bahati mbaya kama tulivyosema Jumanne wiki hii kwamba madudu haya na uchafu wake wote unafanywa na makada wa CCM. Wanaojua taratibu, sheria na kanuni. Ni makada wanaojua fika kwamba miongoni mwa imani za CCM ni kukataa kutoa na kupekea rushwa kwa kuwa ni adui wa haki.
Kila tunapojitafakarisha na kutazama nyuma tunajiuliza, nchi hii inapelekwa wapi na wanasiasa wanaamini kuwa fedha ni msingi wa kupata uongozi.
Ni kwa nini tumefika hapa tulipo? Ukiwasikiliza wana-CCM wengi walioshindwa kura za maoni, tatizo siyo kwamba kura hazikutosha, ila wengi walibana kutoa fedha. Mwenye dau kubwa ndiye alikuwa na uwezo wa kubadili mwelekeo; siyo uhodari wa kujieleza mbele ya wajumbe; siyo uwezo wake wa kuongozi; siyo historia yake katika uongozi, ila nguvu zake za fedha.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment