Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa ongezeko kubwa la mapato ya wakulima wa karafuu katika kipindi cha miaka minne iliyopita ni uthibitisho wa dhamira ya kweli na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Saba kuimarisha zao hilo.
Alisema katika kipindi hicho, wakulima wa karafuu nchini wamejipatia jumla ya shilingi bilioni 231.2 kutoka Sh. bilioni 42.6 miaka mitano kabla ya hapo ikiwa ni ongezeko la asilimia 359.4.
Akizindua Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu nchini jana katika viwanja vya Kiwanda cha Makonyo Wawi, Chake-Chake, Pemba, Dk. Shein aliwapongeza na kuwashukuru walioshiriki katika kutekeleza programu mbalimbali na mipango ya serikali ya kuimarisha zao hilo hadi kufikia kiwango kilicho sasa.
Alifafanua kuwa serikali iliona haja ya kuwapo ushirikiano uliojengwa katika ukweli na kuaminiana kutoka kila upande serikalini, wakulima na wafanyabiashara ili kujenga mazingira mazuri ya biashara na hilo ndilo lililofanyika na kuleta mafanikio hayo yanayoonekana hivi sasa.
Tulitaka tushirikiane na wafanyabiashara na leo tunao hapa, tulipambana na magendo kwa kutoa bei nzuri na leo mafanikio tumeelezwa hapa; hayo yote ni matokeo ya ushirikiano, alisema.
Wakulima sasa wana matumaini makubwa na mfuko huo kwa kuamini kuwa ni chombo muhimu katika kuendeleza zao hilo hivyo ni lazima kuzingatia masharti ya uendeshaji wa mfuko kwa maslahi ya wote, alisisitiza.
Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Mazrui, alisema kucheleweshwa kwa kupitishwa muundo mpya wa utumishi na mishahara ya watumishi wa ZSTC, Dk. Shein analifahamu na linashughulikiwa na mamlaka zinazohusika.
Mapema akitoa maelezo ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSTC, Mwanahija Almasi Ali alitaja mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika biashara ya zao la karafuu ikiwa ni matokeo ya jitihada za makusudi za uongozi wa serikali ya Awamu ya Saba inayoongozwa na Dk. Shein.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment