Dr kwame Nkurumah
KWAME Nkrumah alikuwa Rais wa kwanza wa Ghana na mwanasiasa ambaye alipigania Uhuru wa nchi hiyo, wakati huo ikiitwa Gold Coast. Katika harakati zake za kupigania uhuru, Nkrumah alikuwa anatumia falsafa ya “utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa na mengine yote yataongezwa kwenu (seek ye first the political kingdom, and all else shall be added unto you).Katika falsafa hii, Nkrumah aliamini kwamba muhimu ilikuwa ni nchi za Afrika kupata uhuru wa kisiasa kwanza na mambo mengine yangefuata.
Falsafa ya Nkrumah ilikuwa ni jibu kwa baadhi ya watu na hasa mataifa ya magharibi yaliyokuwa yakidai kuwa nchi za Afrika zilihitaji maandalizi kabla ya kupewa uhuru wa kujitawala.
Tunatambua kwamba nchi nyingi za Afrika zilizojipatia uhuru miaka ya 1960 hazikuweza kujitawala sawasawa. Hali hii ilisababisha mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara. Hata hivyo uchanga na kushindwa kujitawala sawasawa kusingeweza kuhalalisha kuendelea kwa ukoloni wa kizungu.
Tunaweza kuitumia falsafa ya Nkrumah katika kuelezea mtikisiko wa kisiasa unaoendelea ndani ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi, UKAWA na nchi kwa ujumla. UKAWA walimkaribisha Edward Lowassa kujiunga na umoja huu na kisha kugombea urais ili kuendelea na safari yake ya matumaini.Tayari Lowassa amekubali mwaliko wa UKAWA, ameshajiunga na CHADEMA na ndiye atakuwa mgombea wa urais wa umoja huo kupitia CHADEMA.
Uamuzi wa UKAWA kumkaribisha na hatimaye kumpa nafasi Lowassa kugombea urais kupitia CHADEMA si tu kwamba ni wa kijasiri, bali pia ni tata kwa sababu kadhaa. Mosi, uamuzi wa Lowassa ni wa kijasiri kwa sababu hii ni mara ya kwanza tangu mfumo wa vyama vingi uanze kwa kiongozi wa juu wa CCM mwenye staha ya Lowassa kuhama katika chama hicho.
Binafsi nampongeza Lowassa kwa ujasiri wake huo. Uamuzi aliouchukua ni uamuzi mgumu na ameweza kuishi falsafa yake ya kufanya maamuzi magumu. Kwa vyovyote vile, bila kujali kama atashinda au kushindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, ameandika historia na amejijengea heshima ya kipekee katika kukuza demokrasia pevu hapa nchini kwetu.
Pili, uamuzi wa viongozi wa UKAWA wa kumpokea na hatimaye kumpa nafasi ya kugombea urais sio tu kwamba ni uamuzi wa kihistoria na kijasiri, lakini pia ni uamuzi tata sana na wenye kuonesha roho ngumu sana katika siasa za Tanzania.
Hii ni kwa sababu kubwa mbili. Sababu ya kwanza ni ukweli kwamba Lowassa ndiye mwanasiasa anayehusishwa zaidi na taswira ya ufisadi kuliko mwanasiasa yeyote hapa nchini. Sababu ya pili na ambayo ni kubwa zaidi ni ukweli kwamba taswira hii ilijengwa na viongozi wa CHADEMA ambao ndiyo hao leo wamemkaribisha awe mgombea wa urais kupitia chama chao.
Viongozi hao walizunguka kila pembe ya nchi hii na kumtangaza Lowassa kwamba ndiye kinara wa ufisadi wa Tanzania. Baadhi ya wachambuzi walipojaribu kumtetea Lowassa kwa kutia shaka juu ya tuhuma zake walishambuliwa na wapinzani wake ndani na nje ya chama chake cha zamani kwa kuambiwa kwamba wamenunuliwa naye.
Ni katika mazingira haya naamini ndiyo maana Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk Wilbrod Slaa, amepata kigugumizi kuungana na wenzake katika kumpokea na kumtakasa Lowassa. Hii ni kwa sababu yeye ndiye hasa aliyeongoza jahazi la kumnanga Lowassa.
Ninaogopa kwamba kwa hulka za viongozi wenzake ndani ya CHADEMA hawatamuelewa na sitoshangaa kama wataanza kumpachika majina si muda mrefu ujao kama ataendelea kushikilia msimamo wake wa kutokushirikiana na mgombea huyo mpya wa CHADEMA.
Mazingira ya viongozi wa UKAWA kumpokea Lowassa yanaweza kuelezeka ndani ya falsafa ya Nkrumah ya kutafuta kwanza ufalme wa kisiasa na mengine yataongezewa. Ndiyo kusema viongozi wa UKAWA watakuwa wamezingatia nguvu bayana ya Lowassa katika kuiangusha CCM.
Kwamba muhimu kabisa kwa sasa ni kuiangusha CCM na mambo mengine yatafuata baadaye kama ambavyo ilikuwa ni muhimu kuung’oa utawala wa kikoloni hata kama viongozi wengi wa Afrika walikuwa hawajafanya maandalizi yeyote ya kutawala.
Kwa upande mmoja, falsafa ya viongozi wa UKAWA inaeleweka hasa kwa baadhi ya watu wanaoamini kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kukiondoa chama tawala cha CCM madarakani kama njia ya kuachana na mfumo wa kikomunisti wa kuunganisha dola na chama cha siasa.
Wapo watu pia wanaoamni kwamba kuendelea kwa CCM kutawala ni kikwazo kikubwa katika ujenzi wa demokrasia ya kweli katika nchi yetu. Mfumo wa chama hiki unaunganisha dola na chama cha siasa, na ni kwa sababu hii watumishi wengi wa umma wanajihisi kwamba wanalazimika kuitetea CCM. Ni mfumo unaowafanya viongozi wa chama hicho kuwa wababe na kufikiri kwamba wao pekee ndiyo wenye akili na uzalendo wa kuongoza nchi.
Ni mfumo huu wa chama dola ndiyo uliowapa jeuri wajumbe wa Kamati ya Maadili ya chama hicho kuondoa jina la Lowassa na kupeleka majina matano tu kwenye vikao vya uteuzi kinyume na kanuni na utaratibu wa chama hicho.
Ukiukwaji wa kanuni na taratibu za uteuzi wa CCM na matumizi ya ubabe katika kumpata mgombea wa urais wa chama hicho umethibitishwa na wajumbe wa Kamati Kuu wa Chama hicho na viongozi wengine waandamizi, wakiwemo Kingunge Ngombare Mwiru, Dk. Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa. Wote hawa ni viongozi waandamizi katika CCM na hatuna sababu ya kutilia shaka ushuhuda wao.
Sasa chama ambacho kina uthubutu wa kuvunja hata kanuni zake chenyewe kwa sababu ya chuki miongoni mwa viongozi wake huwezi kudhani kwamba serikali inayotokana nayo itaheshimu utawala wa sheria.
Kwa hiyo, kama tutapata mtu mwenye ubabe wa kisiasa unaolingana au kuwazidi hao waliopo katika chama hicho cha kibabe itakuwa ni silaha muhimu sana kuitumia katika kusambaratisha mfumo wa chama dola ili tuanze upya ujenzi wa mfumo wa kweli wa vyama vingi hapa nchini.
Kwa upande wa pili lazima tukiri kwamba Ndugu Lowassa na CHADEMA ni sawa na mbingu na dunia. Hawafanani kwa lolote na itabidi wafanye kazi kubwa kujaribu kubadilishana kama Lowassa atashinda uchaguzi na kama CHADEMA kitaendelea kubaki kuwa chama cha siasa kama kitashindwa. Kisiasa, Lowassa amekuzwa katika siasa za hoja na kusimamia sera za chama chake cha zamani. Hapo alipo ndiyo kwanza anajifunza kukunja ngumi na kusema people’s power. Lakini inajulikana pia kwamba Lowassa ni moja ya viongozi ambao walikuwa hawaamini sana aina ya upinzani uliokuwa ukifanywa na viongozi wa CHADEMA. Kwa muda mrefu, viongozi wa CHADEMA wamejijengea uhalali na umaarufu wa kisiasa kwa kuibua na kusambaza kashfa za viongozi mbalimbali wa CCM na serikali yake.
Ni kwa sababu hii chama hiki kinajulikana zaidi kwa kuibua kashfa kuliko kujulikana kwa itikadi, misingi na sera zake. Huu ndio utakuwa mtihani wa kwanza mgumu kwa Lowassa wa kujaribu kubadili utamaduni wa kisiasa wa CHADEMA.
Kwa upande mwingine, kwa nguvu aliyonayo Lowassa ya ushawishi na ya kisiasa, ni wazi kwamba ameingia na uCCM wake ndani ya CHADEMA na UKAWA. Hivyo basi, kwa maana ya utamaduni wa kisiasa, kiitikadi na kisera, na kama hatatokea mgombea mwingine mwenye nguvu kutoka chama kingine cha siasa, uchaguzi huu utakuwa ushindani mkali kati ya CCM mbili: CCM ya Magufuli na CCM ya Lowassa ndani ya UKAWA.
Hakuna shaka kwamba falsafa ya utafuteni kwanza ufalme wa kisiasa utaivusha UKAWA na upinzani kwa ujumla kwa kuvunja au kupunguza nguvu za kidola za chama tawala. Hata hivyo, Lowassa na CHADEMA watalazimika kufinyangana sana katika kipindi hiki cha kampeni na hasa baada ya uchaguzi mkuu.
Ama Lowassa atalazimika kuifanyanga CHADEMA ibadili utamaduni wa kisiasa na kuvaa uCCM kwa kiasi fulani, au CHADEMA imfanyange vya kutosha Lowassa ili aachane kabisa na uCCM na kuvaa ukamanda kikamilifu. Wakati ni jibu.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/falsafa-ya-kwame-nkrumah-itaivusha-ukawa#sthash.NYBMdInt.dpuf
No comments :
Post a Comment