Akizungumza juzi baada ya kufungua gesi hiyo, Mkurugenzi wa Shirika hilo, James Mataragio, alisema ni jambo la kihistoria kwasababu kulikuwa na changamoto kadhaa katika kipindi chote cha utafiti wa gesi mpaka kukamilisha ujenzi wa visima.
Aidha, baada ya kuiruhusu kutoka katika kisima ilifikishwa katika mnara maalum uliopo kando na kisima hicho kwa ajili ya kuiunguza kwa lengo la kujiridhisha juu ya uwepo wa gesi na uimara wa mabomba na baadae mnara ulizimwa ili ifikishwe kiwandani. Mataragio alisema, kisima hicho ni kati ya visima vitano na kina vya gesi yenye futi za ujazo milioni 20-30 huku kukitarajiwa kuwa na ongezeko kwasababu utafiti unaendelea.“Kwakweli siku ya leo ninajisikia mwenye furaha sana nafikiri kama alivyosema hapo mtaalam kwamba, kulikuwa na changamoto za hapa na pale...lakini ukizingatia ukubwa wa mradi na muda tulioutumia, huu mradi umetumia muda mfupi sana kwakweli kazi imefanyika vizuri sana, na changamoto zilikuwapo kutokana na baadhi ya Watanzania kutoamini kama tutafikia hapa kwamba gesi kufikishwa kwenye bomba na baada ya muda tutazalisha umeme kwa kutumia gesi..” alisema. Kwa upande wake, Meneja mradi wa kampuni ya Morel and Prom (M & P) inayofanya utafiti na uchimbaji wa visima vya gesi, Christopher Maitre, alisema jambo hilo sio la kawaida na kilichofanyika ni kuwaonesha Watanzania kwamba gesi iko tayari na imeanza kupita katika mitambo.
Alisema hiyo ni hatua kubwa na muhimu zaidi kwasababu kufanikisha kutoa gesi katika kisima ikiwa salama bila kuathiri kitu au mtu yeyote ni jambo la kufurahisha, na hatua itakayofuata baada ya hapo ni kuisafirisha kutoka kiwandani Madimba kwenda Kinyerezi, Dar es Salaam tayari kwa matumizi.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment