Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, August 17, 2015

JK ajitetea uteuzi urais CCM.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amesema hakuna aliyeonewa katika uteuzi wa jina la mgombea urais ndani ya chama hicho kwani taratibu zote zilifuatwa.
 
Akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Rais Kikwete alisemaanayehama CCM hivi sasa anafanya hivyo kwa hiari na mapenzi yake mwenyewe kwani uamuzi wa nani agombee urais kupitia chama hicho ulifanyika kwa pamoja.
 
Aidha, alisema uamuzi huo ulifanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM na kuwa ilipigwa kura ndani ya Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya mjadala mrefu na mwishowe maamuzi yalichukuliwa kwa pamoja.
 
Vile vile, Rais Kikwete alisema hakuna haki iliyovunjwa katika mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM kwa sababu taratibu zote zinajulikana wazi.  Kadhalika, alisema ukweli ni kwamba baadhi ya watu walikwishaamua kutoka CCM hata kabla ya vikao vya Dodoma vilivyopitisha jina la mgombea urais kuanza. “Aliyetoka, katoka mwenyewe kwa uamuzi wake mwenyewe, lakini pale tuliamua wote. Maana pale tulipokubaliana kupiga kura, tulikubaliana kupiga kura kwa majina yale matano. Siyo uamuzi wangu peke yangu bali ulikuwa uamuzi wa sote. 
 
Maana tulijadiliana na kukubaliana kwamba kwa mujibu wa katiba yetu, majina ni haya haya. Tukapiga na kura, yakaisha,” alisema Rais Kikwete.  “Hivyo, anayetoka, anatoka kwa hiari yake mwenyewe kwa sababu pale Dodoma sote tulikubaliana, tuliamua wote kwa mujibu wa katiba yetu na kwakweli, wote wanaotaka kutoka ndani ya CCM wanatoka kwa hiari yao wenyewe na wala siyo kwa sababu ya kunyimwa haki.”
 
Aliongeza: “Sasa mchakato umekwisha. Aliyepata kapata. Aliyekosa kakosa. Mchakato huo haurudiwi tena...   hatuwezi kuitisha tena mkutano mkuu. Lililobakia sasa tunasubiri ndugu Magufuli arudishe fomu na baada ya hapo ni Iyena Iyena... na mambo yanakwenda. Haya ndiyo mapenzi ya Mungu.”
 
Katika mchakato huo wa Dodoma, CCM ilimteua Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, kuwa mgombea urais wa chama hicho.  Awali, walijitokeza makada 42 kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo na 38 kati yao ndiyo waliorudisha.
 
Baada ya Dk. Magufuli kupitishwa, baadhi ya wagombea walilalamikia mchakato ulivyoendeshwa, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyeamua kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Lowassa amepitishwa kuwa mgombea wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unaoundwa na Chadema, Chama cha Wananchi (Cuf), NCCR-Mageuzi na NLD. 
 
Atachuana na Magufuli katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment