MGOMBEA urais wa Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema anahitaji kura milioni 10.2 aweze kushinda uchaguzi mkuu.
Kutokana na hali hiyo amewataka Watanzania wajitokeze kwa wingi kupiga kura Oktoba 25 mwaka huu na watakapomaliza kumpiga kura, wawe tayari kuzilinda zisiibwe na Chama Cha Mapinduzi.
Lowassa aliyasema hayo mjini hapa jana alipohutubia maelfu ya wakazi wa Mji wa Iringa katika Uwanja wa Gangilonga.
“Mwaka huu ni lazima CCM waondoke madarakani kwa sababu vyama vikongwe vyote vyenye umri kama wa kwake vimeshaondoka.
“Angalieni Frelimo cha Msumbiji kimeshaondoka, kule Zambia nao chama chao kimeshaondoka, kile chama cha Obote (Milton Obote Rais wa zamani wa Uganda), kimeshaondoka, KANU cha Kenya nacho hakiko tena madarakani ila kimebaki ZANU P F cha Zimbabwe.
“Lakini kumbeni kwamba ili nishinde nahitaji kura milioni 10.2 na hizi zitapatikana tu kama mtajitokeza kupiga na kulinda kura zenu.
“Najua Iringa ni waaminifu kwa CCM kwani mmekuwa mkiwapa kura nyingi. Kwa hiyo, naomba uaminifu huo muuhamishie kwangu nipate kura za kishindo na hatimaye tuunde Serikali imara kwa ajili ya kuleta maendeleo.
“Naomba mumpe pia kura Msigwa (Mchungaji Peter Msigwa, mgombea ubunge Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chadema) kwa sababu huyu ni mchapa kazi na amediriki hata kuwaambia viongozi wa CCM kwamba wanauza pembe za ndovu.
“Mwakalebela anayegombea ubunge kwa tiketi ya CCM hapa Iringa mjini namfahamu, lakini amepanda gari bovu msimpe kura kwa sababu hata kwa utendaji hamfikii Mchungaji Msigwa.
“Wapeni kura pia madiwani wote wa Ukawa kwa sababu huko kwenye halmashauri kuna ulaji mwingi wa fedha na kama mkiwachagua Ukawa watasaidia kudhibiti wizi huo,” alisema Lowassa.
ILANI YA UCHAGUZI
Akizungumzia kwa kifupi ilani hiyo, Lowassa alisema wakati anazindua kampeni Dar es Salaam juzi alishindwa kuisoma kutokana na ufinyu wa muda.
Hata hivyo, alisema kutokana na umuhimu wa ilani hiyo aliisoma juzi hiyo hiyo na kuonyeshwa katika televisheni usiku ingawa awali aliitaja tovuti inakopatikana ilani hiyo.
Kwa mujibu wa Lowassa, ilani hiyo inaeleza jinsi Serikali yake itakavyofuta kodi za vifaa vya michezo nchini ili vijana wa Tanzania waweze kunufaika na michezo na ushuru wa mazao yote nao utafutwa kuinua sekta hiyo.
Alisema Serikali yake itatoa kipaumebele zaidi katika elimu na kipaumbele hicho kitasaidia kukabiliana na tabia ya mabinti wa Mkoa wa Iringa wanaopenda kufanya kazi za ndani.
Pia alisema suala la pensheni kwa wazee, masuala ya kilimo na viwanda na ajira yatapewa kipaumbele kuwakomboa Watanzania na maisha magumu yanayowakabili kwa kuwa yamefafanuliwa vizuri kwenye ilani hiyo ya uchaguzi.
SUMAYE
Wakati Lowassa akiyasema hayo, Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, aliwatoa hofu Watanzania kwa kuwaeleza kuwa hawana haja ya kuhofia usalama wao Ukawa watakapochukua nchi.
“Kuna watu walikuwa wanasema wapinzani wakipewa nchi wataweza kuleta vita nchini eti kwa sababu ni wachanga.
“Sasa mimi nawaambia nilikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10na sasa niko upinzani. Je, mna haja tena ya kuwa na wasiwasi?
“Lowassa naye alikuwa Waziri Mkuu na sasa yuko upinzani, je bado mna haja ya kuwa na wasiwasi wakati tuko upinzani?
“Nawaambia CCM hawawezi kuleta tena maendeleo, msiwape kura kwa sababu tangu nilipomaliza muda wangu bidhaa zote zimepanda bei wakati waliwaahidi mtapata maisha bora.
“Nawaambia mwaka huu CCM watakiona cha moto. Hata wakiiba kura zitabaki nyingine za kutupatia ushindi lakini hatutawaruhusu watuibie,” alisema Sumaye.
Kama alivyosema juzi wakati wa ufunguzi wa kampeni za Chadema na Ukawa Dar es Salaam, alisema Lowassa ana akili nyingi za kuweza kuoiongoza Tanzania tofauti na baadhi ya watu wanavyofikiri.
Alisema wanaosema anaumwa hawana hoja za msingi kwa sababu kila binadamu anapofikisha umri wa kuanzia miaka 50, mwili wake unaanza kudhoofika kutokana na maradhi mbalimbali.
MUNGAI
Naye Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni, Joseph Mungai, alipanda jukwaani na kumnadi mtoto wake, William Mungai ambaye pia ni mgombea ubunge wa Mafinga Mjini kwa tiketi ya Chadema.
Mungai ambaye pia ni mmoja wa wana CCM wanaoheshimika nchini, alisema baada ya kustaafu ubunge aliyerithi nafasi yake alishindwa kutimiza wajibu wake jambo ambalo linaifanya CCM iwe na wakati mgumu.
Kutokana na hali hiyo alimtaka mtoto wake huyo afanye kazi kwa kushirikiana na wananchi kwa kuwa bila hivyo hataweza kuliongoza jimbo hilo kwa mafanikio.
MASHA
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani wa zamani, Lawrance Masha, alisema wananchi wa Iringa hawana haja ya kuogopa kushiriki kufanya mabadiliko kwa kuwa hata yeye baada ya kuamua kuhamia Chadema akitokea CCM, ameanza kupata misukosuko ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kesi mahakamani.
MGEJA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, aliwataka wananchi wa Iringa wamchague Lowassa kwa kuwa ana historia ya kuleta maendeleo nchini.
“Kwanza kabisa najisikia vibaya kusema nilikuwa CCM kwani hata nilipotangaza kuhama watu wengi walinipigia simu za kunipongeza kutokana na uamuzi nilioufanya.
“Kwa hiyo naomba mumchague Lowassa kwa sababu huyu ni jembe na sisi kule Shinyanga alitusaidia kuleta maji kutoka Ziwa Viktoria na hadi sasa maji yale tunayaita Malowasa,” alisema Mgeja.
Mgeja pia alimshangaa Mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli kwa kauli zake ambazo amekuwa akizitoa majukwaani akionyesha kushangaa ni kwa nini hospitali za Serikali zinakosa dawa wakati maduka binafsi yanazipata.
/Mtanzania.
No comments :
Post a Comment