Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, August 18, 2015

MAFURIKO YA UKAWA YAIKUMBA ZANZIBAR!

  Maelfu wamlaki, madereva wa bodaboda wakwepa polisi na kumsindikiza, Mwenyewe aduwazwa asema hajawahi kuona umati kama huo, aibua shangwe baada ya kuzungumzia hatima ya masheikh wanaoshikiliwa Bara.

Maefu ya wakazi wa Zanzibar, wakimsikiliza mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (hayupo pichani), wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Demokrasia Kibanda Maiti visiwani humo jana.PICHA: OTHMAN MICHUZI
Umati mkubwa jana ulijitokeza kumlaki mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, baada ya kuwasili visiwani hapa kusaka wadhamini.
Tangu Lowassa aanze msafara wake wa kusaka wadhamini katika mikoa kadhaa nchini, amekuwa akipata mapokezi makubwa kutoka kwa wananchi.
Alipata mapokezi makubwa katika mikoa ya Mbeya, Arusha na juzi alikuwa mkoani Mwanza.
ULINZI WAIMARISHWA
Wakati Lowassa akiwasili visiwani Zanzibar kwenye Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume kisha viwanja wa Kibandamaiti, ulinzi wa Jeshi la Polisi na vikosi vya ulinzi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ulikuwa umeimarishwa .
Aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume saa 5:30 asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake, mgombea wa urais wa Zanzibar wa Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad.
NIPASHE likiwa katika uwanja huo, lilishuhudia polisi wenye silaha za moto waliokuwa kwenye magari aina ya Defender wakiimaimarisha ulinzi kila kona.
Baada ya kupokelewa, msafara wa magari uliondoka uwanjani hapo na kuungana na msafara mwingine wa pikipiki maarufu kama bodaboda uliokuwa ukimsubiri Lowassa nje ya uwanja huo na kuelekea uwanja wa Kibandamaiti.
Licha ya ulinzi mkali wa polisi, waendesha bodaboda hao walifanikiwa kuwapiga chenga polisi na kuungana na msafara wa Lowassa uliokuwa ukiongozwa na gari maalum la polisi kwa ajili ya msafara wa viongozi wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif.
Akihutubia mkutano huo, Lowassa aliwaambia Wazanzibar kuwa atahakikisha anazingatia taratibu za kisheria ili Masheikh wa Jumuiya ya Mihadhara ya Kiislamu (Uamsho) wanaoshikiliwa katika mahabusu jijini Dar es Salaam, wanapata haki zao.
Ahadi hiyo ya Lowassa ilisababisha umati huo kulipuka kwa furaha na vifijo huku ukimuita `Rais, Rais, Rais. 
Alisema kwa mara zote alizokwenda Zanzibar, hajawahi kushuhudia umati mkubwa kama aliouona jana. 
Lowassa alisema amekwenda Zanzibar kuomba dhamana ya wananchi na kurudia kauli yake kwamba anawania urais kwa kuwa anauchukia umaskini.
“Nataka kuwahakikishia Watanzania popote kwamba mabadiliko yataletwa na vyama vya upinzani. Nimetembea sehemu mbalimbali nimeona wananchi wanataka mabadadiliko ya uongozi,” alisema.
Kuhusu Katiba, alisema yeye ni muumini wa Serikali Tatu zitakazosaidia kuimarisha Muungano na kwamba msimamo wake huo aliouonyesha tangu miaka ya 90 wakati wa harakati za kundi la G55.
Alisema suala hilo litafafanuliwa vizuri wakati wa uzinduzi wa ilani ya uchaguzi Jumamosi wiki hii na wakati wa kampeni.
Hata hivyo, Lowassa alisema njia ya kuiondoa CCM madarakani, ni kwa kupiga kura na wananchi wajiandae pia kulinda kura.
MASHEIKH WALIOFUNGWA
Alisema Masheikh mkoani Mwanza walimwomba azungumzie jambo hilo na kwamba atakachofanya atakapoingia madarakani, atazingatia taratibu za kisheria kufuatilia stahili zao.
KUFUKUZWA KINGUNGE
Kuhusu kufukuzwa kwa Mzee Kingunge Ngombare-Mwiru, alisema ni jambo la kusikitisha kuwa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kumfukuza mtu ambaye alikuwa ni kielelezo cha nchi kwani alikuwa msemaji mkubwa wa masuala ya uchumi wakati wa mabadiliko mbalimbali na bila yeye, CCM isingevuka na kufikia hapo kilipo.
UVCCM mwishoni mwa wiki iliyopita ilitangaza kumvua Ukamanda wa Umoja wa Vijana, Ngombale-Mwiru ikidai ameonyesha wazi kumuunga mkono Lowassa katika mbio zake za kuusaka urais.
Uamuzi huo unatokana na kinachoonyesha ni kauli zake dhidi ya CCM kabla na baada ya Lowassa kukatwa jina lake na kuhamia Chadema.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda, alikaririwa juzi akisema kwa jinsi walivyompima Ngombale- Mwiru, wameona hafai tena kuwa Kamanda wa UVCCM kutokana na kauli zake na wanaiomba CCM kumfuatilia kwa karibu.  
JAMES MBATIA
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa); unaoundwa na vyama vinne vya upinzani vya Chadema, Cuf, NCCR-Mageuzi na NLD, umewaagiza wanasheria nguli nchini kufuatilia mwenendo wa uchaguzi hasa vitendo vya ukandamizaji wa raia wasio na hatia unaofanywa na vyombo vya dola na kuandaa waraka utakaopelekwa Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC), iliyopo The Hague, Uholanzi baadaye mwaka huu.
Aidha, waraka huo utawasilishwa kwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC na kwenye balozi zote za nchi za Ulaya nchini.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, wakati akimtambulisha Lowassa kuwa mgombea urais wa umoja huo na Mgombea Mwenza wake, Juma Haji Duni na Maalim Seif Hamad Sharif, anayegombea urais wa Zanzibar.
 Mbatia alisema waraka huo utaandikwa kueleza uhalifu unaofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia na kwamba mwaka huu vyama vinavyounda umoja huo havitakubali kupokonywa ushindi.
 Alisema Ukawa inataka uchaguzi huru na haki usio na ukandamizaji wowote wa haki za binadamu.
Mbatia alisema Maalim Seif amekuwa akipambana kutetea maslahi ya Wazanzibar kwa miaka mingi hadi akafungwa gerezani mwaka 1989, lakini akiwa kizuizini, hakukata tamaa kwani aliandika waraka maalum ulioelezea azma ya maridhiano.
Alisema ni kwa kupambana huko kulikosababisha maridhiano ya Zanzibar kati ya Maalim Seif (Cuf) na Rais mstaafu Amani Abeid Karume (CCM); yaliyozaa serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani hapa hata baada ya uhasama na mauaji ya wananchi wa Zanzibar.
MAALIM SEIF
Akihutubia maelfu ya wananchi viwanjani hapo, Maalim Seif alisema Wazanzibar wamefurahi kwa ujio wa Lowassa kwani ni ishara ya kuwathamini.
“Kwa Zanzibar, usiwe na wasiwasi, wanakuamini na watakupeleka Ikulu ya Magogoni,” alisema.
Hata hivyo, alisema wamepata taarifa za kusikitisha kutoka CCM zikieleza mikakati ya uvunjifu wa amani na kwamba mgombea ubunge wa Jimbo la Shaurimoyo ametekwa na `janja widi' akanyang’anywa fomu zake wakati akisaka wadhamini.
“CCM nawaambia la kuvunda halina ubani, mnaondoka,” alisema.
Alisema siku zote wafuasi wa Ukawa wamekuwa ni watulivu, lakini mara zote wanaovuruga amani ni polisi ambao huwashambulia wananchi kwa mabomu.
Alisema Rais Jakaya Kikwete, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, anapaswa kuhakikisha amani kwani bila kufanya hivyo  ikivurugika atakayepekwa The Hague ni yeye.
“Ulichukua nchi ikiwa salama salimini, ondoka uiache salama; haya matendo hayataiokoa CCM,” alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema atachukua fomu Jumapili wiki hii na baada ya kufanya hivyo atazungumza na wananchi.
MBOWE
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kwa nyakati tofauti vyombo vya dola vimetumika kupora ushindi wa wananchi na kwamba mwaka huu hawatakubali.
Alisema vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kufanya kazi bila kupendelea chama chochote kwa kuwa Ukawa itakapoingia madarakani, vyombo hivyo ndivyo vitakavyoendelea kulinda ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
“Tunaomba hao wenye madaraka, wayatunze majeshi yetu siyo kuyatumia kujenga chama kimoja. Ndiyo majeshi tunayoyataka,” alisema.
JUMA HAJI DUNI
Mgombea Mwenza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Chadema, Juma Haji Duni, alisema mwaka huu ni fursa ya pekee kwa wananchi kuiondoa CCM madarakani na kuwa kinachotakiwa kufanywa ni kutanguliza maslahi ya Taifa mbele vyama baadaye.
“Ni tabia ya watawala kudhania kwamba bunduki itawasaidia; mabavu yatawasaidia na kwa bahati mbaya sana hata hawajifunzi. Hakuna taifa lililokuwa linajidai kwa nguvu kubwa, lakini wananchi waliliangusha; Ujerumani Mashariki ilianguka hivyo hivyo,” alisema.
Alisema tawala za Tunisia na nchi nyingine za Afrika, zilianguka kutokana na wananchi kuchoka, hivyo Tanzania inapaswa kujifunza.
Alisema jukumu la kwanza la serikali ya Ukawa ni kufufua mchakato wa Katiba ya Wananchi na kumaliza tofauti zote zilizopo ili kujenga nchi na maendeleo.
HAMISI MGEJA
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja, aliipongeza Ukawa akisema ni meli salama ambayo inaweza kuwavusha Watanzania na kuwafikisha kwenye malengo makubwa.
Mgeja alisema aliamua kujiengua CCM kwa sababu Watanzania wanataka mabadiliko, hivyo kujiunga kwake Chadema ni kushiriki kikamilifu kuleta mabadiliko hayo.
Alisema CCM ni chama kinachowaumiza Watanzania kutokana na mfumo dume ndani yake.
“Na ikifika mahali unauguza mgonjwa bila kupona, ujue kwamba kuna tatizo zaidi...tatizo la CCM ni kutopenda kuambiana ukweli,” alisema.
Alisema ndani ya CCM, watu wanaosema ukweli wanakutwa na matatizo makubwa kama yaliyomkuta mzee Ngombale-Mwilu aliyevuliwa Ukamanda wa UVCCM na aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Himid Mansoor.
KATIBA
Kuhusu Katiba, alisema ni roho na mustakabali wa raia na kwamba hata halikuwa ajenda ya CCM kwani lilikuwa la Chadema na Cuf ambao wamelipigia kelele kwa muda mrefu.
Alisema hakuna kikao chochote cha CCM kilichowahi kujadili suala la kuanza mchakato wa kuandika Katiba, bali madai ya Katiba yalipozidi, Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, walikaa kwa dharura na kukubaliana waanzishe mchakato huo ambao hata hivyo, haujafanikiwa.
Alisema mchakato huo umeligharimu taifa mabilioni ya fedha, lakini katika hali ya kushangaza, CCM ilichakachua maoni ya wananchi kwa makusudi, jambo lililowalazimu viongozi wa Ukawa kususia vikao vya Bunge Maalum la Katiba.
Alisema hata Mgombea Mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, amepewa zawadi ya kuwania nafasi hiyo baada ya kusimamia mchakato kandamizi wa Bunge hilo ambao umechakachua mawazo ya wananchi.
Alisema viongozi pekee wanaoweza kufufua mchakato wa Katiba ya wananchi ni Ukawa kwa kuwa CCM imeyazamisha maoni ya wananchi.
TASLIMA
Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Cuf, Twaha Taslima, alisema hata baada ya kuondoka kwa Prof. Ibrahim Lipumba, Cuf imebakia ngangari na kamwe haitatetereka.
Alisema katika nchi maskini, umoja ni jambo la msingi kufikia maendeleo makubwa akieleza kuwa nchi tajiri duniani zilizoendelea kiviwanda na kiuchumi, zimeungana, lakini inasikitisha kuwa nchi maskini zinashindwa kufanya hivyo pamoja na kwamba zinakabiliwa na umaskini mkubwa.
Alisema CCM au kiongozi yeyote ndani ya chama hicho, hawapendi kuona Ukawa baada ya mabavu ya CCM ndani ya Bunge la Katiba; kufanikisha kuzaliwa kwa umoja huo.
Alisema: “Wakati Ukawa inaanzishwa, CCM walijua watatusambaratisha kama ambavyo wangeweza kuona paka wakiwa sehemu fulani na kuwatupia nyama ili waparuane, ndivyo wanavyotaka na sisi itokee; lakini nataka kuwahakikishia Ukawa hatutasambaratika.”
Alisema Ukawa uliundwa kutokana na mabavu ya CCM ndani ya Bunge ambayo pia yalitumika kwenye mchakato wa chama hicho wa kumpata mgombea urais ambao ulizaa majeruhi wengine walioamua kujiunga na harakati za mabadiliko, akiwamo Lowassa.
MAKAIDI
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk. Emmanuel Makaidi, alisema kila zama ina kitabu chake na kwamba zama ya CCM imekwisha na sasa ni zama ya Ukawa.
SALUM MWALIMU
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu, alisema umati mkubwa kukusanyika siku ya kazi na kuacha shughuli zao, umeonyesha imani kubwa kwamba wana ujumbe ambao wanaamini kuwa ni Lowassa atatekeleza.
“Umevunja rekodi kwa watu kuitikia mkutano siku ya Jumatatu kujaa kwa wingi kukusikiliza...hii inaonyesha watu hawa wana jambo lao moyoni wanataka kukueleza na wanaamini wewe ndiye utakatimiza,” alisema.
BURUDANI
Mbali ya umati mkubwa wa watu waliofurika kwenye viwanja vya Kibandamaiti, mkutano wa jana ulipambwa na burudani ikiwamo ya morani wa Kimasai waliotoa burudani ya kimila.
Aidha, msanii Kassim Issa, aliimba wimbo maalum wa Ukawa ambao ulisisimua watu uwanjani hapo kiasi cha kumnyanyua mke wa Lowassa, Mama Regina.
Mkutano wa jana ulikuwa na ulinzi mkubwa wa Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na wa KMKM ambao walitanda njia nzima kuanzia Uwanja wa Ndege wa Sheikh Amani Abeid Karume.

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment