Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, August 17, 2015

Ni funga kazi jijini Mwanza.

Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akihutubia umati uliofurika katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza jana. PICHA: MPIGAPICHA WETU
Haijawahi kutokea. Siyo mabomu ya machozi wala polisi wenye silaha walioweza kuzuia halaiki ya wananchi kufika kwenye viwanja vya Furahisha kuhudhuria mkutano wa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.
Hii ni kwa sababu umati uliojitokeza kuanzia Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambako polisi walilazimika kupiga mabomu yasiyohesabika kuwatawanya wananchi ambao walifunga barabara inayoingia uwanjani hapo, kutozaa matunda.
Msafara wa Lowassa anayeungwa na mkono na vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na Cuf, ulilisimamisha Jiji la Mwanza kwa takriban saa tatu kutokana na msafara kutembea kilomita sifuri kwa saa.
Pamoja na polisi kupiga mabomu mita chache kutoka uwanjani hapo, Lowassa alipotoka tu uwanjani, umati mkubwa wa wafuasi wake na wa Ukawa, waliokuwa wamejificha waliibuka wakiwa na chupa za maji; mbele ya askari waliokuwa kwenye magari wakiwa na silaha za moto na mabomu ya machozi.
Kilichochangia msafara kutembea mwendo mdogo ni baadhi yao kumwaga maji barabarani kama ishara ya kupiga deki ili Lowassa apite huku wengine waliokuwa na fagio za chelewa, wakifagia.
Wananchi wengine walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ikiwamo ‘Richmond ilikuwa ni maagizo ya juu’; ‘pombe mwisho kaunta, Ikulu ni Lowassa’; ‘kufuli mwisho mlangoni’; na ‘Tanzania bila Lowassa haiwezekani.’
 KAULI YA POLISI
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, akizungumza na waandishi wa habari uwanjani hapo, alisema polisi hawajawazuia wananchi kushiriki mkutano bali wamepiga mabomu kuzuia wale ambao wamekwenda uwanja wa ndege ambako siyo eneo la mkutano.
“Hatuna nia ya kuzuia mkutano, wananchi tumewaambia kwamba waende Furahisha kwa sababu wakija huku watasababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa uwanja,” alisema.
Alisema pamoja na agizo hilo, wananchi waling’ang’ania kwenda uwanjani na hata polisi walipowaelimisha ilishindikana, ndipo walipoamua kutumia mabomu ili wafungue njia.
Alisema: “Hapa wamekuja zaidi ya wananchi 500, tumeona hali ya usalama itakuwa ni ngumu na ndiyo maana tuliwazuia na jitihada zetu zilitulazimu kupiga mabomu kadhaa ili kuwatawanya.”
Ikiwa uwanjani hapo, Nipashe ilisikia milipuko ya mabomu zaidi ya 30 yaliyopigwa kwa takriban saa moja kabla msafara wa Lowassa haujaondoka kuelekea Furahisha.
Tofauti na mikoa mingine, maandamano ya Mwanza hayakuwa na pikipiki, bajaj wala magari zaidi ya yale ya viongozi wa Ukawa taifa na wabunge wa Chadema kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, bali ni wananchi wasiohesabika ambao walilazimisha mkutano kutembea kilomita sifuri kwa saa.
Idadi ya watu waliojitokeza kwenye uwanja wa Furahisha, nusura usababishe mkutano kuahirishwa baada ya watu kuanza kuzimia na kupoteza fahamu, jambo ambalo lilisababisha kikosi cha Msalaba Mwekundu uwanjani kuzidiwa nguvu.
Kutokana na hali hiyo,  Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliwaambia wananchi warudi nyuma na wengine wakae chini ili kutoa nafasi kwa viongozi, waandishi na wapigapicha wafanya kazi yao.
Hata hivyo, tangazo hilo halikufua dafu kwani baadhi ya wananchi waliokuwa mbele, walikaa chini lakini halaiki hiyo iliendelea kusababisha usumbufu mkubwa kutokana na idadi ya watu walioendelea kupoteza fahamu.
Taarifa nyingine zilieleza kuwa baadhi ya wafuasi wa Ukawa walilala katika viwanja vya Furahisha ili kuwahi nafasi za kumshuhudia Lowassa.
Baada ya kuanza kusukumana, wananchi wengine walianza kulia na kusema kuwa walilala uwanjani kumsubiri Lowassa na viongozi wa Ukawa, lakini wanasikitika kusukumwa na kukanyagwa.
LOWASSA
 Akiwahutubia wananchi alisema alichokiona Mwanza siyo mapenzi bali ni mahaba.
Alisema wananchi wanataka mabadiliko makubwa ambayo hayawezi kuletwa na CCM bali vyama vya upinzani.
Alieleza kusikitishwa na taarifa za wananchi kupigwa mabomu na kukumbusha kuwa askari wanaoendelea kunyanyasa raia hasa wakati wa uchaguzi, watawapeleka ICC kupambana na sheria za kimataifa.
Alisema yeye ni mtu wa maamuzi magumu kwa manufaa ya Watanzania na mtu yeyote atakayejaribu kukwamisha mchakamchaka wa maendeleo ya serikali yake, atamwondoa.
“Nayajua mambo ya Mwanza, matatizo ya wamachinga, meli ya MV Bukoba, kiwanda cha ng’ombe, treni ya abiria na mizigo, nayajua nitayaeleza zaidi wakati wa kampeni,” alisema.
“Najua tatizo kubwa la umeme, tatizo kubwa kabisa la pamba na ahadi ya uwanja mkubwa wa ndege, nitakuja kueleza baadaye,” alisema.
Alipotaja tatizo la umeme, wananchi walipiga kelele kuonyesha kukerwa na mgawo usio rasmi, hali iliyomlazimu Lowassa kumwagiza Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje, aende kwa Meneja wa Tanesco akaulize sababu za tatizo hilo na kwamba akishindwa ampigie simu ili alishughulikie mwenyewe.
MBOWE
 Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe, alisema nchi nzima kuna msiba wa umaskini kuanzia kwa watumishi wa umma, sekta binafsi, wakulima, wafugaji, wamachinga na mama lishe.
Hata hivyo, alisema msiba huo umesababishwa na kikundi kidogo cha viongozi wachache wanaotumia woga na umaskini huo kuendelea kuwakandamiza wananchi.
Alisema wananchi mkoani Mwanza waliojitokeza kumdhamini Lowassa na mgombea mwenza wake, Juma Haji Duni, ni zaidi ya 100,000, lakini waliojazwa kwenye fomu ni 200 kama kanuni na taratibu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), zinavyotaka.
“Namwambia Mkuu wa Majeshi, asiliingize Jeshi la Wananchi wa Tanzania kusaidia ushindi wa CCM...vijana watatu wataalam wa kompyuta aliowachukua katika Jeshi la Wananchi na kuwapeleka Nec kwa majukumu maalum ambayo yataisha Novemba 15, amewapeleka kufanya nini?” alihoji.
Aliongeza kuwa: “Namuuliza Jaji Lubuva, hao vijana wa kijeshi uliowapokea ofisini kwako umewapokea kwa kazi gani?...nipo tayari kutoa ushahidi wa taarifa hizi.” 
Alisema ana ushahidi wa namba, majina na vikosi wanavyotoka askari hao pamoja na tarehe waliyoanza kazi Nec.
Hata hivyo, juhudi za Nipashe kumpata Msemaji wa JWTZ, kujibu madai hayo ya Mbowe jana zilishindikana baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana kama ilivyokuwa kwa Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima. 
WENJE
 Akiwahutubia wananchi uwanjani hapo, Wenje alisema Tanzania hivi sasa inamhitaji kiongozi jasiri anayeweza kufanya maamuzi kama Lowassa.
“Tunataka rais anayeweza kufanya maamuzi magumu ya kufufua viwanda vilivyouawa na CCM ili vijana wapate ajira. Tunahitaji maamuzi magumu ya kuwalipa polisi posho ya Sh. 300,000 badala ya Sh. 150,000 wanayopigwa chenga na tunahitaji rais atakayeboresha huduma za elimu na afya siyo kugawa laptop kwa walimu,” alisema.
TWAHA TASLIMA
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Cuf, Twaha Taslima, alisema kwa mujibu wa sheria, polisi wanapaswa kulinda amani iliyopo na siyo kusababisha fujo kwa kuwapiga mabomu wananchi wanapokusanyika kwa amani.
MBATIA
 Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema polisi wakiendelea kutumia nguvu dhidi ya raia wasio na silaha, wataishia The Hague kwenye Mahakama ya Uhalifu wa Kivita (ICC), Novemba.
Alisema ilani ya Chadema chini ya mwavuli wa Ukawa itakayozungumzia malengo ya serikali ya awamu ya tano, itazinduliwa Jumamosi wiki hii sambamba na uzinduzi rasmi wa kampeni.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment