Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, August 29, 2015

Rais Kikwete alivyoitabiria kifo CCM

Viongozi wa chama ndio mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu. Nawaombeni tubadilike, kama tutaendelea hivi, hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali, nawaambieni. Kikwete
By Joster Mwangulumbi, Mwananchi
Kwenye mikutano ya hadhara, Rais Jakaya Kikwete huonyesha ujasiri, mbwembwe na kuwapa imani wanachama wa CCM kwamba watashinda Uchaguzi Mkuu ujao, lakini hayo si maneno anayozungumza kwenye vikao na mikutano ya ndani ambako anatakiwa kueleza hali halisi.
Na ndivyo inavyotokea kwenye vikao vingi ambavyo mwenyekiti huyo wa CCM hushiriki, na pia kwenye mikutano na mahojiano na vyombo vya habari vya nje.
Novemba 2007, Rais Kikwete alifanya ziara ya kiserikali nchini Uingereza, ambako kwa mara ya kwanza alitoa dokezo juu ya uwezekano wa CCM kushindwa katika Uchaguzi Mkuu na kisha ikalazimika kukabidhi madaraka kwa upinzani.
Dokezo hilo alilitoa katika mahojiano na gazeti la Financial Times (FT). Alikiri kuwa ipo siku chama chake kitakabidhi madaraka kwa upinzani japokuwa siku hiyo bado iko mbali.
FT: Je, unaona uwezekano kwamba iko siku chama tawala kitakabidhi mamlaka kwa chama cha upinzani kitakachokuwa kimeibuka mshindi?
JK: Ndiyo, siku hiyo inakuja. Lakini sioni uwezekano huo siku za hivi karibuni. Bado tuko imara; tunapendwa; nafikiri tunatekeleza mambo yetu vizuri.
FT: Lakini pia kuna matatizo mengi ndani ya chama chenu (tawala) CCM, siyo kweli kwamba yapo? Kwa mfano, Bwana (mkurugenzi wa Takukuru), Edward Hoseah amekuwa akitoa malalamiko dhidi ya wabunge wa CCM kwamba wananunua kura. Je, si kweli kwamba kuna matatizo makubwa ya ufisadi ndani ya chama hicho kongwe?
JK: Ni kweli kuna matatizo. Suala muhimu ni kwamba, je, tunayafahamu matatizo hayo? Je, tuko tayari kukabiliana nayo? Hili ni moja ya mambo ya msingi katika chama chetu. Ni chama kinachobadilika kulingana na wakati; hakijasimama. Ikitokea umefanya jambo ovu, hatua zinachukuliwa dhidi ya mhusika…Ikiwa watu wanataka uongozi kwa mbinu chafu, za rushwa, nafikiri haipendezi; tunachukua hatua.
Majibu ya Rais Kikwete, kwa wakati ule, yalitokana na ukweli kwamba katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 alishinda kwa asilimia 80.28. Hakuona uwezekano wa CCM kuangushwa haraka, lakini mtazamo huo ulibadilika kuanzia mwaka 2010 ushindi uliposhuka hadi asilimia 62.83.
Novemba 18, 2010 alipozindua Bunge la 10 mjini Dodoma aliwaambia wabunge: “Kwa upande wa mapambano dhidi ya rushwa katika miaka mitano iliyopita tumechukua hatua mwafaka za kujenga uwezo wa kisheria, kimfumo na kitaasisi kupambana na rushwa nchini. Tumetunga sheria mpya kali zaidi na yenye upeo mpana zaidi wa kukabili tatizo hili. Pia, tumetunga Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya kuzuia na kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi. Tumeunda chombo kipya cha kuzuia na kupambana na rushwa, Takukuru, chenye mamlaka zaidi kisheria na chenye uwezo mkubwa zaidi wa rasilimali watu na vifaa wa kutekelezea majukumu yake.
“…Katika kipindi hiki tuhuma nyingi zimeibuliwa, kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani. Watuhumiwa wengi zaidi wamepatikana na hatia na kuhukumiwa. Rushwa kubwa zimeshughulikiwa na vigogo wamewajibishwa bila kuonewa muhali. Pamoja na hayo, bado ipo haja ya kufanya kazi zaidi kwani tatizo la rushwa bado ni kubwa.”
Hayo yalikuwa mafanikio ya Serikali siyo chama, kwani kuanzia wakati huo, wananchi wameshuhudia kansa ya rushwa inavyokitafuna chama hicho na ndipo alianza kuonya mfululizo kwenye vikao vya ndani kwamba CCM isipobadilika haraka na kuondokana na makundi, chuki, visasi na fitina itaanguka kama si mwaka 2015 basi mwaka 2020.
Oktoba 2012, katika mikutano ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Umoja wa Wanawake (UWT) na mkutano mkuu, Rais Kikwete alionya kwamba vitendo vya rushwa vinavyojitokeza katika chaguzi za ndani ya CCM visipodhibitiwa, vitakitumbukiza chama hicho kwenye shimo.
“Kuna mambo mengi, mengine yanasikitisha, hata kuyasema ni aibu; na wakati wote naendelea kukumbusha: Ndugu zangu haya tukiendelea nayo sura tunayoijenga kwa wananchi na chama chetu… tunaona sisi tunapata, lakini athari yake kwa wananchi na ndani ya chama ni mbaya sana, tena sana. Sina namna ya kutafuta maneno mazuri ya kulieleza hilo la kununua na kuuza kura,” alisema Rais Kikwete.
Kuonyesha kwamba matatizo ndani ya chama ni mazito, akifunga mkutano mkuu wa CCM, Kikwete alifichua mikakati michafu kwamba kuna wanachama waliokuwa na ndoto za kuona Mkutano Mkuu wao ukimalizika kwa mpasuko. Alisema anawashangaa baadhi ya wanachama ambao wanaifahamu vizuri CCM, lakini walikuwa wakiombea mabaya ili mkutano umalizike vibaya waweze kujivunia kile walichokikusudia.
“Namshukuru sana Mungu tumemaliza salama; kuna watu walikuwa wakitambika usiku na mchana CCM imalize vibaya mkutano wake na walitamani itoke na vipande, lakini wameshindwa na sijui watamdai nani gharama zao?” alihoji.
Oktoba 2013 alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu wa mikoa, makatibu na wenyeviti wa wilaya wa chama hicho nchini, alionya kuwa ikiwa rushwa haitakomeshwa ndani ya chama hicho, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015 kitaanguka vibaya na iwapo kitanusurika, hakitapita kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kuonyesha uzito wa jambo hilo, Kikwete alisema amempa makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula jukumu la kushughulikia viongozi wa CCM wanaokula rushwa. Kikwete aliendelea kusema kuwa tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku, hali ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
 “Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea shilingi laki mbili za airtime (muda wa mawasiliano), ndugu zangu hatutafika ama wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema Kikwete.
“Viongozi wa chama ndio mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu. Nawaombeni tubadilike, kama tutaendelea hivi, hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali, nawaambieni.”
Kikwete alisema hayo wakati alipohutubia kwa saa mbili kufunga mafunzo hayo. Na hakuishia hapo aliweka mkazo akisema: “Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa.”
Februari 2014 Kikwete alitoa utabiri mwingine mbaya dhidi ya CCM wakati wa maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa CCM mkoani Mbeya. Alisema chama kimekithiri kwa ufisadi, dhuluma, rushwa, hongo, umangimeza na vitendo vingi vichafu, mambo ambayo yanapunguza imani ya wananchi kwa chama na Serikali.
Alisema endapo chama hakitachukua hatua za makusudi kujisafisha, hakitavuka 2015 na kuwataka wanachama wake kujiandaa kisaikolojia kuchukua nafasi ya chama kikuu cha upinzani baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 kwa kuwa haoni dalili za chama kujirekebisha na kurejesha mvuto kwa Watanzania kabla ya uchaguzi ujao.
Mtifuano mkali
Uchaguzi wa viongozi ndani ya CCM na jumuiya zake, mbali ya kutawaliwa na rushwa pia hukumbwa na vurugu. Mwaka 2012 walichapana makonde katika chaguzi za UVCCM na UWT walikashifiana sana.
Mwaka huu yamejitokeza matukio kadhaa. Kwanza ni tukio la kupigwa mgombea urais Dk Muzammil Kalokola; pili ni baadhi ya makada kupigana wakati wa kampeni za kura za maoni hadi mmoja kulazwa; na tatu kuibuka kwa maandamano maeneo kadhaa wakati wanachama wakipinga wagombea wao kuibiwa kura.
Matukio haya yameudhi makada wengi na makumi kwa mamia wanahama na kujiunga na chama kikuu cha upinzani, Chadema. Kichocheo kikubwa cha kuhama kwao inadaiwa ni njama zilizofanywa na vikao vya CCM kumkata jina mgombea urais, Edward Lowassa bila sababu za msingi.
Miongoni mwa waliohama CCM na kujiunga Chadema ni wabunge, wenyeviti wa mikoa na wilaya, madiwani na wenyeviti wa mitaa. Viongozi hao wamekuwa wakihama pamoja na mamia ya wanachama.
Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru aliwataka CCM kumpigia magoti Lowassa, kama wanataka chama hicho kushinda Uchaguzi Mkuu, mwaka huu. Alisema: “Lowassa anashikilia mtaji mkubwa wa mamilioni ya wapigakura, hivyo kama CCM haitampigia magoti na kumwomba ushiriki wake katika kampeni za chama hicho, hakitashinda uchaguzi huo.”
Je unaona dalili?

No comments :

Post a Comment