Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, August 31, 2015

Siri ya Lowassa Ikulu yaanikwa.

  Sumaye afichua na kuonya hakuna bao la mkono Ukawa kufuta JKT, Joseph Mungai aibuka

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Hatimaye Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amesema kwamba mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, lazima atashinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.
 
Sumaye alitoa kauli hiyo jana asubuhi wakati wa kumnadi Lowassa kwa wananchi wa Mufindi, mkoani Iringa.
 
Sumaye, ambaye alishika nafasi ya uwaziri mkuu kwa miaka kumi katika awamu ya tatu iliyoongozwa na Benjamin Mkapa tangu mwaka 1995 hadi 2005,  alisema wananchi wanaojitokeza kwa wingi katika mikutano ya Lowassa ni kwa sababu wanataka mabadiliko, kwani hawataka maisha yao yaendelee kuwa kama ya kisiki ambacho huwa hakibadiliki.
 
“Watanzania wanataka mabadiliko na mheshimiwa Lowassa lazima atakuwa rais, sisi hatusemi atakuwa rais kwa kura za bao la mkono bali kwa kura za wananchi ndani ya boksi la kura,” alisema Sumaye ambaye alijiunga na Ukawa Agosti 21, mwaka huu.
 
Sumaye alisema Ukawa hawana mpango wa kufanya njama za ovyo za kuiba kura na kuwaomba  wananchi wampe kura nyingi mgombea wa Ukawa kwa sababu wanahitaji mabadiliko.

Sumaye alisema kwa kuwa Bunge lina wabunge zaidi ya 360, hivyo ili Lowassa aweze kuunda Baraza lake la Mawaziri, anatakiwa kupata wabunge zaidi ya 300 na 60 wakitoka vyama vingine na pamoja na idadi kubwa ya madiwani.
 
LOWASSA AANIKA VIPAUMBELE
Kwa upande wake, Lowassa alianisha vipaumbele vyake ikiwa wananchi watampa ridhaa ya kuingia Ikulu.
 
Lowasa aliwaambia wakazi wa  Mufindi kama wananchi wa Mufindi kuwa ikiwa watamchagua kuwa rais, atazigeuza kambi zote za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwa Vyuo vya Ufindi Stadi (Veta).“Nauliza kwa nini vituo vyote vya JKT visigeuzwe kuwa vyuo vya Veta na kusoma hapo hapo mambo ya uzalendo kuna ubaya gani?”alihoji Lowassa huku akishangiliwa na wananchi.
 
Alisisitiza kuwa kipaumbele cha kwanza hadi cha tatu ni elimu na kubeza wanaotaka kilimo kuwa kipaumbele cha kwanza.
 
Lowassa alisema ukombozi  wa kweli wa Mtanzania ni elimu na zawadi nzuri ya mzazi ya kumpa mtoto wake ni elimu kwani hata katika nchi zilizoendelea kama Singapore, Indonesia na Malaysia zimesonga mbele kwa sababu ya elimu.
 
“Watu wajinga hupenda kuona wenzao wajinga, wanasema kipaumbele ni kilimo kwanza, sasa utampaje mtu kipaumbele ch kilimo wakati hana elimu?” aliendelea kuhoji.
 
 Alisema serikali yake itagharimia elimu ya msingi hadi chuo kikuu na mtu asiulize fedha zitatoka wapi kwani yapo mabilioni ya fedha yanatumika kwa mambo yasiyofaa.
 
Aliongeza kuwa iwapo watu watakuwa na elimu ya kutosha itakuwa rahisi kupata ajira.
 
KUFUTA USHURU WA MAZAO
Kuhusu mazao, alisema akichaguliwa atafuta ushuru wa mazao na kwamba ni jambo la kushangaza mkulima analima mazao yake halafu serikali inamkopa.
 
Akizungumzia kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka huu, alisema wapo watu wanaosema CCM ni hodari wa kuiba kura na kuwaondoa hofu hiyo kwa kuwahimiza wananchi watakaokwenda kupiga kura wahakikishe wanazilinda zisiibwe.
 
“Wapo watu wanasema CCM ni hodari wa kuiba kura na kwamba wataiba hizo kura halafu nitaanguka, nataka kila mtu ahifadhi kichinjio chake na siku ya kwenda kupiga kura kila mtu afanye hivyo, watu wabakie kwenye vituo hadi kura zihesabiwe, tumewasha moto wanatetemeka,” alisema Lowassa.
 
Alisema nchi ikikiachia chama kimoja kikatawale kwa muda mrefu kinawanyanyasa wananchi wake, hivyo wananchi hawanabudi kufanya mabadiliko kama walivyofanywa raia wa Malawi, Zambia na Kenya waliovipumzisha vyama tawala vilivyodumu madarakani kwa miaka mingi na kuhoji kwa nini Watanzania wasiweze.
 
“Vyama vikongwe vikikaa kwa muda mrefu, wananchi wanateseka, angalia wenzetu wa Malawi, Zambia na Kenya wamevitoa madarakani vyama tawala, tukikosea tutajutia,” alisema Lowassa.
 
MUNGAI AIBUKIA UKAWA, AMPIGIA DEBE LOWASSA
Wakati huo huo;  Mwanasiasa mkongwe nchini na waziri wa zamani, Joseph Mungai, jana aliibukia katika mkutano wa kampeni wa Lowassa na kumnadi.
 
Mungai ambaye alitumikia serikali ya awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu, aliibukia katika mkutano huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Wambi na kuanza kumnadi Lowassa.
 
Mbali na kumnadi Lowassa, Mungai ambaye amekuwa mbunge wa jimbo la Mufindi kwa miaka mingi, pia alitumia mkutano huo kumnadi mtoto wake, Willy Mungai, ambaye anagombea ubunge kupitia Chadema katika Jimbo la Mafinga Mjini.
 
Willy Mungai anapambana na mgombea wa CCM, Cosato Chumi, katika jimbo hilo. 
 
Mungai alisema Lowassa na Sumaye ni viongozi ambao wanapenda sana kusonga mbele kimaendeleo na hawapendi kubakia hapo walipo na ndiyo maana wameamua kuhamia upinzani.
 
“Hawa mawaziri wakuu mimi nikiwa waziri wao waliniongoza vizuri, ndiyo maana kuna mambo mengi ya msingi yaliyofanyika katika jimbo hili ikiwa ni pamoja na miradi ya elimu,” alisema.
 
Akimnadi mtoto wake, alimtaka kuhakikisha anavaa viatu vyake ili kuhakikisha wakazi wa jimbo hilo wanakuwa na maendeleo.
 
“Nawaombeni wananchi mumpe mwanangu kura kwa sababu yeye ndiye mwenye uwezo wa kuvaa viatu nilivyoviacha mimi na siyo mtu mwingine,” alisema.
 
Mungai alisema ikiwa Willy atashinda, ahakikishe anajenga uwanja wa mpira wa kisasa ili wananchi wawe wanapata fursa ya kuburudika baada ya saa za kazi.
 
Hata hivyo, Nipashe lilipomuuliza Mungai kama amehamia rasmi Chadema, alisema: 
 
“Mimi ni mwanasiasa mstaafu, si CCM wala chama chochote cha upinzani.”
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment