a
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya za Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga viwanja vya Shycom, Sitta alidai kuwa ana ushahidi wa kutosha kumhusisha Lowassa na masuala ya ufisadi, hivyo kutaka wawe na mdahalo utakaowezesha kila kitu kuwekwa hadharani.
Sitta, mmoja wa wajumbe 32 wa kamati ya kampeni za CCM, alitaka mdahalo huo kati yake na Lowassa ufanyike wiki ijayo.
“Ninaomba mdahalo na Lowassa wiki ijayo katika televisheni ili Watanzania wabaini ukweli,” alisema Sitta.
Hata hivyo, Sitta aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond ikinguruma bungeni, hakueleza ni kwa nini ushahidi anaodai kuwa nao hajaufikisha kwenye vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe.Hivi karibuni, Lowassa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu kabla ya kujiuzulu kutokana na kashfa hiyo ya Richmond mwaka 2008, amekuwa akisisitiza kuwa hahusiki na ufisadi wowote bali anachafuliwa na wapinzani wake; huku akiweka msimamo kuwa yeyote mwenye ushahidi auweke hadharani au aende mahakamani.
Lowassa alikuwa miongoni mwa watia nia 38 waliotaka kugombea urais kupitia CCM kabla hajakihama chama hicho na kutua Chadema kutokana kile alichoeleza kuwa ni kutoridhishwa na mwenendo wa sasa wa chama hicho tawala.
Mara kwa mara Lowassa amekuwa akisema CCM kimepoteza misingi ya kuundwa kwake. Vilevile, alisema hakufurahishwa zaidi na kile alichodai kuwa ni kuondolewa kimizengwe katika mchakato wa uliomteua John Magufuli kuwa mgombea urais wa CCM Julai 12, mwaka huu.
Akizungumzia mchakato wa kumpata rais wa awamu ya tano, Sitta alisema wanamshangaa Lowassa kwani hakuondolewa peke yake kwenye kinyang'anyiro cha urais ndani ya CCM.
“CCM ilitupima, ikatuona hatutoshi... mbona Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wameachwa... na hata mimi mzee wa viwango nimeachwa na hatujalalamika?” alihoji Sitta ambaye pia alikuwa miongoni mwa wasaka urais 38 wa CCM.
Aidha, Lowassa amekuwa akivutia maelfu ya watu katika mikutano yake, hivyo kuonekana kuwa tishio kwa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Baada ya kutua Ukawa unaoundwa na Chadema, CUF, NLD na NCCR-Mageuzi, makada kadhaa wa CCM wakamfuata wakiwamo waliokuwa wenyekiti wa chama hicho mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja; aliyekuwa wa mkoa wa Singida, Mgana Msindai na aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga.
TIMU YA LOWASSA
Akizungumza na Nipashe jana kuelezea kauli ya Sitta kuhusiana na mdahalo, Msemaji wa Lowassa, Aboubakar Liongo, alisema hawajasikia jambo hilo na kwamba midahalo hiyo ikitokea kwenye majukwaa wao wako tayari.
Aliongeza kuwa hoja yoyote itakayoibuliwa itafafanuliwa vizuri kwenye mikutano ya kampeni.
SILINDE: LOWASSA HAHUSIKI RICHMOND
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, David Silinde, amesema Lowassa hahusiki hata kidogo na kashfa ya Richmond.
Akizungumza katika kuzindua kampeni za uchaguzi katika Jimbo Momba, katika mji wa Tunduma, mkoani Songwe jana, Silinde alisema kabla ya kumpokea Lowassa na kumpatia nafasi ya kugombea urais kupitia Ukawa, walijiridhisha kuwa hakuhusika na kashfa ya Richmond.
“Mimi ni mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema. Alipokuja Lowassa ndani ya chama chetu, tulimhoji kwa wiki mbili mfululizo tukitaka kujiridhisha. Kwa sababu tuko watu makini mle ndani, alituletea vielelezo vyote vikiwamo vya sauti na baada ya kujiridhisha kuwa hakuhusika moja kwa moja na suala la Richmond, ndipo tukampa nafasi agombee urais,” alisema Silinde.
Alisema kuwa kutokana na ushahidi walionao, ndiyo maana wakamtaka mtu yeyote mwenye ushahidi kwa tuhuma dhidi ya Lowassa aende mahakamani.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment