Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, August 30, 2015

Sumaye ajibu mapigo ya CCM

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye akihutubia wananchi katika viwanja vya Jangwani kwenye uzinduzi wa kampeni za Ukawa. Picha na Edwini Mjwahuzi
By Goodluck Eliona, Mwananchi
Dar es Salaam. Wakati Waziri Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye akitangaza kuihama CCM, alidokeza kuwa siku moja chama hicho kitaona umuhimu wake, na jana alianza kuonyesha hilo alipopangua hoja dhidi ya mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa huku akianika uozo wa Serikali.
Sumaye, ambaye hadi sasa hajatangaza anajiunga na chama gani, jana alikuwa kivutio kwenye uzinduzi wa kampeni za urais za Ukawa, ambayo inaundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, kiasi cha maelfu ya watu waliofurika kutaka aendelee kuzungumza licha ya muda kuwa finyu.
Akizungumza mbele ya umati huo mkubwa kwenye viwanja vya Jangwani, Sumaye alirejea tena sababu zilizomfanya aingie Ukawa kuwa ni haja ya kufanya mabadiliko wanayotaka Watanzania ambayo alinyimwa nafasi na CCM.
“CCM wanawajaza Watanzania kitu kinaitwa woga wa usilolifahamu au woga wa usilolijua kwa hiyo kila siku wanawaambia Watanzania mkiwapa wapinzani nchi itaingia kwenye vita,” alisema Sumaye.
“Baada ya Lowassa kuliona hilo, na kujiridhisha kuwa Watanzania wanamfahamu akienda kuwasaidia, woga huo hautakuwepo tena.
“Hata mimi nimeingia upinzani kwa ajili ya kushirikiana na Lowassa kuleta mabadiliko nchini ili wananchi waanze kufurahia maisha bora.”
Lakini kelele za shangwe ziliongezeka wakati alipoanza kujibu hoja mbalimbali zinazotolewa na makada wa CCM dhidi ya viongozi wa vyama vya upinzani.
Sumaye, ambaye alishika nafasi ya uwaziri mkuu kwa kipindi chote cha miaka 10 ya Serikali ya awamu ya Tatu, alisema Rais Jakaya Kikwete alimteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu katika Serikali yake, akisema ni jambo la kushangaza kuona leo mkuu huyo wa anamwona hafai.
“Kuna mtu anamuweka Waziri Mkuu asiyefaa? Lakini ni Lowassa huyu huyu aliyemwingiza Kikwete Ikulu,” alisema na kusababisha mlipuko wa kelele za shangwe.
“Kwamba Lowassa ni mchapakazi halina mjadala.”
Kuhusu kumhusisha Lowassa na ufisadi na kula rushwa, Sumaye alisema kama mbunge huyo wa Monduli ni fisadi na mla rushwa, mbona hakukimbia nchi tangu alipotoka madarakani mwaka 2008.
“Angekuwa fisadi si wangeshamweka mahali? Lowassa amechukua ustaarabu wa kujiwajibisha baada ya tatizo kuingia katika Serikali. Hivi nani mkubwa wa Serikali? Tangu lini waziri mkuu akawa mkubwa wa serikali?” alihoji.
“Waziri Mkuu anabebeshwa mzigo ili kumwokoa Rais na serikali yake.”
Sumaye alieleza kuwa baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati fulani alitoa machozi kwenye kikao cha Halmashauri Kuu kuwa hajaona mtu mvumilivu kama Rashid Kawawa kwa sababu alikuwa akibeba mizigo ambayo ilipaswa kubebwa na Nyerere.
“Hiyo ndio kazi aliyofanya Lowassa,” alisema Sumaye huku akishangiliwa na wananchi waliofurika uwanjani.
“Hivi angekuwa mtu mchafu kiasi hicho, hawa watu wote wangekuja kufanya nini?”
Lowassa alijiuzulu wadhifa huo mwaka 2008 baada ya Bunge kuunda kamati kuchunguza sakata la Serikali kuingia mkataba wa ufuaji umeme wa dharura na kampuni ya Richmond Development ya Marekani iliyobainika baadaye kuwa haikuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo.
/Mwananchi.


No comments :

Post a Comment