CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeteua vigogo 32 kuunda kamati ya kampeni za mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli katika kuhakikisha kinashinda Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Hatua ya kuteuliwa kwa kamati hiyo ambayo itakuwa chini ya uenyekiti wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, inaelezwa kuwa ni njia ya kukabiliana na nguvu za mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Kamati hiyo inadaiwa kuwa itakoleza mnyukano wa hoja kati ya CCM na upande wa timu ya Ukawa, ambayo juzi imehitimisha kazi ya kusaka wadhamini mikoani kwa mgombea wao.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kuundwa kwa kamati hiyo ya kampeni kitaifa kutafuatiwa na uundwaji wa kamati za ushindi katika ngazi za mikoa na wilaya kwa nchi nzima.
Alisema kutokana na kuimarika na kujiamini kwa CCM, kikao cha Kamati Kuu (CC), kilichoketi juzi Dar es Salaam kimefanya uteuzi wa wajumbe wa kamati hiyo huku kundi la waliokuwa wagombea urais katika mchakato wa chama hicho nao wakiteuliwa.
Walioteuliwa kuingia katika kamati hiyo ambao pia walikuwa wagombea urais ni pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, pamoja na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Wengine ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rajab Luhwavi ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti Bara, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai atakayekuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Sophia Simba, Muhamed Seif Khatib, Issa Haji Ussi, Nape, Amina Makillagi na Christopher Ole Sendeka.
Mbali na hao, pia wapo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazizi wa CCM, Abdallah Bulembo, Hadija Aboud, Mohamed Aboud, Waride Bakari Jabu, Mahmoud Thabit Kombo, Shamsi Vuai Nahodha, Maua Daftari, Stephen Masele, Dk. Pindi Chana, Shaka Hamdu Shaka, Sadifa Juma Khamis, Antony Diallo, Livingston Lusinde pamoja na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Ummy Mwalimu.
Nape alisema uamuzi huo ulifanywa na kikao cha CC chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.
“Kamati Kuu imewateua wagombea hao kushiriki katika kamati hiyo itakayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana,” alisema.
MBINU ZA KAMPENI
Nape alisema baada ya kuundwa kwa kamati hiyo, CCM imejipanga kushinda Uchaguzi Mkuu katika ngazi zote, huku akitamba wao watatumia mbinu tofauti na wapinzani wao Ukawa.
“Tangu lini jeshi la angani huwa linashinda, CCM kwa kupitia mtaalamu wa jeshi (Abdulrahman Kinana), ataweka utaratibu wa kutumia kuipatia ushindi CCM kwa jeshi la ardhini, na kazi ya kamati hiyo ya ushindi itaanza kuonekana Agosti 23, mwaka huu,” alisema Nape huku akitamba.
WAGOMBEA VIPORO
Nape alisema Kamati Kuu ya CCM pia imekamilisha kazi ya uteuzi wa wagombea ubunge katika majimbo mawili ya Singida Mashariki na Kiteto.
“Wagombea ubunge walioteuliwa kupeperusha bendera ya CCM katika majimbo hayo ni Jonathan Njau (Singida Mashariki) na Emmanuel Papian (Kiteto),” alisema.
KINANA NI NANI?
Abdulrahman Kinana ni Katibu Mkuu wa CCM kwa sasa, ambaye alipata kuwa mbunge wa Arusha mwaka 1985-1995 wakati huo Mkoa wa Arusha ukiwa kitovu cha harakati zake za kisiasa katika kipindi chote cha miaka 25 alichotumikia nafasi mbalimbali ndani ya chama na Serikali.
Amekuwa mjumbe wa NEC kwa miaka 25, huku ikielezwa kuwa kukaa kwake katika nafasi hiyo kumempa heshima kubwa ndani na nje ya CCM, ikiwamo kuwa mwanasiasa wa kupigiwa mfano.
Ni mmoja kati ya viongozi wanaoamini falsafa ya uongozi wa kupokezana vijiti.
Pia Kinana atakumbukwa kama meneja mahiri wa kampeni za wagombea urais wa CCM tangu mwaka 1995 hadi 2000 wakati wa ugombea wa Benjamin Mkapa na kati ya mwaka 2005 na 2010 katika kipindi cha Jakaya Kikwete, vipindi ambavyo vimeipa CCM ushindi mkubwa ukiacha ule wa mwaka 2010 ambao chama hicho kilipata kutikiswa na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa.
/Mtanzania
No comments :
Post a Comment