Uamuzi wa wanachama hao umekuja siku chache baada ya CCM kumpitisha Profesa Jumanne Maghembe (pichani), kuibuka mshindi katika kura za maoni ndani ya chama hicho.
Aidha, awali kulikuwa na uvumi mitaani kwamba aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Joseph Thadayo, naye alikuwa akitajwa kutaka kujiunga na Chadema.
Hata hivyo, Thadayo alipotafutwa na Nipashe hakuwa tayari kuzungumzia uvumi huo.
Jana, mgombea ubunge wa Chadema katika jimbo hilo, Hendry Kileo, alimpokea na kumkabidhi kadi ya uanachama mpya, Diwani huyo wa kata ya Jipe, Twalib Kidaya, na hivyo kuunngana na wanachama wenzake waliohama.
Katibu wa CCM Wilaya ya Mwanga, Mwanaidi Mbisha, alipotafutwa na Nipashe kuzungumzia timka timka ya makada hao alisema: ”Huyo Diwani aliyetimka na wenzake hawakubaliki na kimsingi Twalib amekimbia baada ya kuangushwa kwenye mchakato wa kura ya maoni ya udiwani…yeye huwa hakubali kushindwa.”
Makada hao ni miongoni mwa wana-CCM waliokihama chama hicho kwenda Chadema wakidai kufuata mabadiliko wakisema wamechoshwa na mizengwe.
Wakati hayo yakijiri, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Anthony Komu, amedaiwa kumtisha kwa silaha Katibu wa chama hicho Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema.
Tukio hilo lilidaiwa kutokea jana baada ya Chadema makao makuu, kudaiwa kuamuru kurudiwa kwa uchaguzi wa kura ya maoni, ambao awali ulimpa ushindi Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Owenya, baada ya kuwashinda wagombea wengine tisa kwa kura 266, akiwamo Komu aliyepata kura 25.
Akizungumza na Nipashe, Lema alidai kutishwa kwa bastola na Mkurugenzi huyo saa 6:00 mchana eneo la Kibosho baada ya kutaka kujua taratibu zilizotumika kuhamisha mkutano halali wa uchaguzi huo ambao ulielekezwa kufanyika eneo la Garden kata ya Kiboroloni Manispaa ya Moshi.
“Ni kweli amenitishia kwa silaha na hivi sasa nimetoka Kituo Kikuu cha Polisi Moshi Mjini kumshtaki. Wamenipa hati yenye namba MOS/RB/829/2015. Kimsingi mimi nilikwenda kujua kama wajumbe waliopelekwa pale ni halali; kama ambavyo niliagizwa na Kaimu Katibu Mkuu (Salum Mwalimu)…hata hivyo, huo mkutano wake haukufanyika, lakini mkutano halali uliofanyika Garden umempitisha Lucy kuwa mgombea,” alisema Lema.
Hata hivyo, Komu alisema: “Sijawahi kushika silaha na wala similiki silaha.
Nilishika mara ya mwisho nikiwa JKT (Jeshi la Kujenga Taifa). Iweje nimtishe Lema wakati sina ugomvi naye?…yeye kaja kasema amekuja kuvunja mkutano, tukamwambia hapa ni Moshi Vijijini, tunafanya uchaguzi wetu. Hata hivyo, kulitokea rabsha na vijana wake aliokuja nao wa ulinzi wakatofautiana na kupigana.”
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment