Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, August 21, 2015

Viongozi wetu walipoihepa historia

Image result for Eastern Africa Region Pan-African Congress

BY Ahmed Rajab
LILIKUWA tukio la kihistorialakini viongozi wa Tanzania waliamua kulipiga pande. Kwa kweli lilikuwa jambo la kushangaza kwamba hapa kuwako na kiongozi hata mmoja wa Tanzania, si wa serikali si wa Upinzani, aliyehudhuria Kongamano la Ukanda wa Afrika ya Mashariki la Umajumui wa Kiafrika (Eastern Africa Region Pan-African Congress) lililokutana jijini Nairobi Agosti 10 hadi Agosti 12.

Kuna nchi kama Sudan na Burundi ambazo ziliwapeleka makamu wao wa Rais; nyingine ziliwapeleka mawaziri na mabalozi wao walio Kenya. Tanzania haikuona kwamba Kongamano hilo lilikuwa na umuhimu hata wa kumpeleka Balozi wake.Badala yake Tanzania iliwakilishwa na wanaharakati peke yetu.

Taksiri hiyo inasema mengi kuihusu Tanzania yetuyaleo. Taifa hili silo tena lile lililokuwa mstari wa mbele katika kuongoza mavuguvugu yanayopigania haki, utu wa Mwafrika, maendeleo ya kijamii na yenye kupinga Bara la Afrika lisiwe linanyonywa na kupewa kibepari na ubeberu mamboleo.

Katika kuzikumbatia sera za utandawazi (au “utandawizi”, chambilecho Issa Shivji), serikali ya Tanzania imeghafilika kiasi cha kuifanya isahau wapi inapostahiki iwepo katika medani ya vita baina ya haki na udhalimu, baina ya uhuru wa kweli na utumwa mamboleo.

Ndio maana watawala wetu wanakuwa wepesi kukata maamuzi yanayokwenda kinyume na maslahi ya wananchi, kwajumla, na hawaoni ajizi kuchukua hatua zinazozidi kuwadhalilisha wanyonge.

Kwa kila kipimo, Kongamano la Afrika ya Mashariki la Umajumui wa Kiafrika lilikuwa ni tukio la kihistoria.
Kwa mara ya mwanzo wanaharakati na waumini wa Umajumui wa Kiafrika wa ukanda huu walikutana rasmi wakiinadi kaulimbiu ya “Afrika Moja, Afrika Huru!”.

Katika miaka ya 1950 na 1960, kuliwahi kuwako Vuguvugu la Umajumui wa Kiafrika la Afrika ya Mashariki na ya Kati (Pafmeca) lakini Kongamano la Nairobi lilikuwa la kwanza la aina yake kwa ukanda wa mataifa ya Afrika ya Mashariki.

Kwa mara ya mwanzo wanaharakati wa Umajumui wa Kiafrika kutoka nchi 12 za Afrika ya Mashariki walikutana, walijuwa na walijadiliana.

Hatimaye,walikubaliana kuwa na msimamo mmoja kuhusu masuala kadhaa yanayolikabili bara la Afrika.
Lengo kuu lilikuwa kujiandaa kwa muhula wa pili wa Kongamano la Nane la Umajumui wa Afrika, litalofanywa nchini Botswana Mei mwakani. Mkutano wa Muhula wa kwanza wa Kongamano la Nane ulifanywa Accra, Ghana, Machi mwaka huu.

Waumini wa Umajumui wa Kiafrika waliokutana Nairobi walikubaliana kuhusu mapendekezo watayoyawasilisha kwenye kongamano la nane na kadhalika walikubaliana kuhusu namna ya kuwachagua wajumbe wataohudhuria kongomano hilo.

Kwa kuandaa kongamano la Nairobi, nchi za ukanda wa Afrika ya Mashariki zimekuwa zikiongoza katika maandalizi ya kongamano za kanda.

Ukanda wa Afrika ya Kaskazini unataraji wa kuandaa kongamano lake huko Cairo kuanzia Oktoba 28, na utafuata nyayo za Afrika ya Mashariki.Halikadhalika, matayarisho yanaendelea kufanywa ya kuyafanikisha makongomano ya Afrika ya Magharibi na Kusini mwa Afrika.

Katika miaka ya 1960 na 1970 wengi wangeliitarajia serikali ya Tanzania kuongoza katika kuandaa kongamano kama hilo, hasa kwa kanda ya Afrika ya Mashariki.

Hii leo, ni serikali za Kenya, Uganda na Rwanda zilizo safu ya mbele katika kuunga mkono, kwa hali na mali,harakati za umajumui wa Kiafrika katika huu ukanda wetu wa Afrika ya Mshariki.

Inavyoonyesha ni kwamba serikali ya Tanzania inashughulishwa na mingine. Hatukatai kwamba taifa limo mbioni likijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba, lakini hiyo sio sababu madhubuti ya serikali au chama chochote cha upinzani kuitika wito wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wa kupeleka ujumbe rasmi katika kongomano hilo la kihistoria.

Uhuru atakumbukwa na historia kwa namna alivyojitolea kuhakikisha kwamba kongamano la Afrika ya Mashariki linafanyika, tena kwa mafanikio.
Aliomba binafsi kwamba kongamano hilo lifanywe Nairobi na aliiagiza serikali yake, kupitia kwa mwanasheria mkuu wa serikali, ihakikishe kwamba Kenya inatoa misaada yote inayohitajika kwa ufanisi wa kongamano hilo.

Sina shaka yoyote kwamba Uhuru Kenyatta ni muumini wa dhati wa Umajumui wa Kiafrika. Ni kiongozi aliyeonesha kwamba amepevuka anapozingatia mahusiano ya Afrika na madola yanayojaribu kulidhibiti bara hili, hususani yale ya Magharibi.

Tanguashikehatamuzaserikaliya Kenya, Uhuruamechukuahatuakadhaazenyekuthibitishahayaniyasemayo. Si kwamba amekuwa akipayuka na kupayapaya kwa matamshi ya jazba kuhusu dhana hiyo ya umajumui wa Kiafrika. Amefanya mambo ya maana zaidi kwa kuchukua hatua halisi za kuimarisha mahusiano kati ya nchi yake na jirani zake, kwa mfano, Uganda.

Uhuru pia amekuwa jasiri wa kuchukua hatua za kuzikatalia nchi kama ya Uingereza mikataba yenye kuidhalilisha Kenya na wananchi wake.

Mfano mzuri ni ule mkataba wa kijeshi kati ya Uingereza na Kenya ambao Uhuru ameshikilia urekebishwe ili nchi yake iwe na hadhi sawa na Uingereza.

Labda Uhuru, kwa upande mmoja amejitolea kuitumikia dhana ya umajumui wa Kiafrika akikumbuka mchango adhimu wa baba yake,Jomo Kenyatta,katika Kongamano la Tano la Umajumui wa Kiafrika lililofanywa Manchester, Uingereza, 1945.
Jomo alishiriki kikamilifu katika kongamano hilo la kihistoria, ambamo alitoa hotuba kwa niaba ya nchi za Afrika ya Mashariki.

Baadhi ya vijana wa Kiafrika waliohudhuria kongamano hilo la Manchester, akiwemo Jomo miongoni mwao, baadaye waliziongoza nchi zao katika harakati za kupigania uhuru kutoka kwa wakoloni na hatimaye wakaziongoza nchi hizo zilipopata uhuru.

Wengine walikuwa Kwame Nkrumah wa Ghana na Dk. Hastings Kamuzu Banda wa Malawi. Mkutano huo wa Manchester unakumbukwa kuwa ndio uliowahamaisha Waafrika wadai uhuru wa nchi zao.
Kuna wengi wenye kuibeza dhana ya umajumui wa Kiafrika katika enzi hizi tulizonazo. Wenye kufanya hivyo wanakosea pakubwa.

Bado tunaihitaji dhana hiyo kwa ukombozi wa Afrika na wa Waafrika.

Tunaihitaji awali ili tuweze kujikomboa kimawazo kwa sababu bado akili zetu zimenaswa katika mitandao na mifumo ya kufikiri inayotufanya kifikira tuendelee kuwa watumwa wa fikira za wale wanaoamini kwamba wao ndio wenye kujua kila kitu na kwamba fikira zao tu ndizo zilizo sahihi.

Ukombozi huo ni muhimu na ni wa lazima ili bara letu liweze kujikomboa katika kila Nyanja za kimaisha — za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kimazingira.

Ni ukombozi aina hiyo utaotuwezesha tuwe na umoja tuutakao, umoja wa haki na wa kila taifa na jamii kuheshimiana na kuwa na uhuru.

Ndio maana tulipokuwa Nairobi tukipiga kelele: “Afrika Moja, Afrika Huru” — tuwe na umoja wa kutuunganisha sote na uhuru wa kutufanya tusiwe tunatawaliwa na madola ya kigeni tu lakini na sisi wenyewe Waafrika tusiwe tunawaigiza wakoloni kwa kujaribu kutawalana. Tuwe na umoja wa haki, uhuru na usawa.

Binafsi nilitiwa moyo na kongamano la Nairobi la Ukanda wa Afrika ya Mashariki wa Umajumui wa Kiafrika. Nadhani jambo lililonitia sana moyoni michango ya vijana wa Afrika ya Mashariki na ya wanawake wetu katika mijadala mbalimbali tuliokuwa nayo.

Nilitanabahi kwamba jitihada za kulihuisha vuguvugu la umajumui wa Kiafrika hazikwenda kombo hata kidogo.

Hii ni dhana inayozidi kuwavutia vijana wetu na dada zetu na kinachohitajika ni kuzidi kuieneza katika jamii zetu.

Kwa mintarafu ya hayo, jitihada zinafanywa kulizindua tawi la Umajumui wa Kiafrika la Tanzania katika siku chache zijazo litalokuwa na wanachama kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Tayari jirani zetu wa Ethiopia, Kenya, Rwanda na Uganda wanayo matawi yao na wakati umefika sasa wa Tanzania nayo kuwa na lake.

 - See more at: http://raiamwema.co.tz/viongozi-wetu-walipoihepa-historia#sthash.yIzU6cY7.dpuf

No comments :

Post a Comment