Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe (Kushoto), mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Anna Mghwira na mgombea mwenza, Hamadi Mussa Yusuph wakionyesha ilani ya chama hicho baada ya kuizindua katika Uwanja wa Zakhem, Dar es Salaam jana. Picha na Omar Fungo
Kiongozi huyo ambaye alitumia dakika 20 katika hotuba yake, alisema CCM na Ukawa wanazungumzia kuleta mabadiliko kwa kutumia mchango wa mawaziri wakuu waliosababishia Taifa hasara kubwa.
Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ATC - Wazalendo, Zitto Kabwe amesema mabadiliko wanayotaka Watanzania hayawezi kuletwa na watu walewale waliosababisha hasara Taifa.
Zitto alisema hayo jana wakati wa ufunguzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu za chama hicho zilizofanyika kwenye uwanja wa Zakhem Mbagala, jijini hapa.
“Hatuwezi kuwarejesha watu walewale waliyotusababishia kadhia tuliyonayo sasa… sisi tunataka kuleta mabadiliko ya kimaudhui kupitia ACT – Wazalendo,” alisema Zitto.
Kiongozi huyo ambaye alitumia dakika 20 katika hotuba yake, alisema CCM na Ukawa wanazungumzia kuleta mabadiliko kwa kutumia mchango wa mawaziri wakuu waliosababishia Taifa hasara kubwa.
Alisema tangu kuanzishwa kwa Taifa, kumekuwa na mawaziri 10, ambao hivi sasa wawili wako Ukawa na wanne wanamuunga mkono mgombea urais wa CCM.
“Watatu walishapumzika mbele ya haki na mmoja hajasema yupo upande gani, sasa hawa waliopo Ukawa na CCM watawezaje kuleta mabadiliko wakati wameleta hasara kwa Taifa?” alihoji Zitto.
Alisema kwa sasa, mgombea wa CCM, Dk John Magufuli amekuwa akiahidi kuunda mahakama maalumu ya kushughulikia rushwa wakati alikuwa miongoni mwa wajumbe waliokataa rasimu ya Katiba Iliyopendekezwa ambayo ilikuwa na kipengele cha kuipa meno Takukuru kushughulikia watuhumiwa wa rushwa.
“Sasa leo hii Magufuli amepatwa na nini, wakati alikuwa miongoni mwa wajumbe wa kamati ya sheria,” alihoji Zitto na kuongeza: “Mama ni mwema, tumchague Mama Mghwira ili tubadilishe gia ardhini na siyo angani.”
Ushauri wa Profesa Kitila
Mshauri mkuu wa chama hicho, Profesa Kitila Mkumbo aliwataka Watanzania kuwa makini katika uchaguzi huu ambao umetawaliwa na mambo matatu aliyoyataja kuwa ni mbwembwe, ulaghai na misingi na sera.
“Ukitaka misingi na sera chagua ACT – Wazalendo lakini ukitaka mbwembwe na ulaghai nenda vyama vingine,” alisema Profesa Mkumbo ambaye awali, alipendekezwa na chama hicho kuwania nafasi ya urais lakini hakuwa tayari.
Wakati akitoa ushauri huo, Profesa Mkumbo alitumia nafasi hiyo kufafanua ‘nini maana ya uchaguzi mwaka huu’ kupitia aina ya wagombea na kampeni zinazoendelea nchini, huku akitaja sifa za mgombea urais anayefaa.
Alitaja sifa hizo akisema lazima awe na fikra pana kwa ajili ya kutoa dira na mwelekeo wa taifa.
“Lazima tuwapime wagombea hao kwa uwezo wa fikra zao, kama kuna mgombea anatoa ahadi ya maji au anategemea ilani ya chama chake basi huyo hatufai, huyo anafaa kuwa waziri mkuu tu,” alisema na kuongeza:
“Jambo la pili, tunataka mgombea urais awe na uwezo wa kulinda tunu za taifa, kama kuna wagombea wana tabia za ujanjaujanja, ulaghai au chama kinafikiria ukabila, ukanda basi huyo mgombea wake hatufai, lazima kuangalia kama anawajali wanyonge je, atalinda tunu za taifa au atakuwa mateka wa matajiri.”
Kuhusu jambo la tatu, Profesa Mkumbo alisema rais lazima awe mlinzi wa Muungano wa Taifa, uadilifu na ulinzi wa demokrasia na awe kiongozi atakayekuwa na utambulisho wa Taifa.
Kuhusu demokrasia, Profesa Mkumbo alisema, lazima Watanzania wampime mgombea urais atakayelinda uhuru wa demokrasia, kwa kuwa wapo wagombea waliopatikana katika mazingira yasiyokuwa kidemokrasia.
“Je, alipatikana vipi katika uteuzi wake, alipatikana kwa udikteta? Kama mgombea anaonekana kuwa na jeshi kabla hajapewa jeshi itakuwaje, hiyo ni hatari sana,” alihoji.
Profesa Mkumbo ambaye alitumia lugha ya mafumbo bila kutaja majina ya vyama na wagombea hao, alisema ACT-Wazalendo pekee ndicho chama chenye misingi na sera zinazotekelezeka.
Madongo ya Mchange
Meneja wa Kampeni wa chama hicho, Habibu Mchange alitumia muda mrefu kuwashambulia Ukawa, hasa mgombea urais, Edward Lowassa na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Alikumbushia orodha ya watuhumiwa 11 wa ufisadi waliotajwa na viongozi wa Chadema katika Viwanja vya Mwembeyanga, Temeke mwaka 2007, akieleza kushangazwa kuona Lowassa ambaye pia alitajwa kwenye orodha hiyo kusimamishwa na chama hicho kuwania urais.
“Kwa sasa kuna sumu mbili ziko kwenye chupa, moja ni CCM na nyingine ni Ukawa ambayo ina maji ya sumu kwa hivyo tunaomba Watanzania watuamini tunapita katikati ya chupa hizo za sumu.”
Alisema ufisadi kwa sasa umeota mizizi na hata kuhamia Ukawa; “Naomba kwa sasa wanivumilie viongozi hao (CCM na Ukawa) kwa sababu ninayo mengi ya kusema.
“Jana, Sumaye naye ametulaghai kwamba, anashangaa CCM inaendelea kuaminiwa na wananchi wakati yeye alikuwa kiongozi wakati mambo hayo yakitokea.
“Mwaka 1995 wanasiasa walikuwa na mjadala wa kununua ndege, Waziri wa Fedha kipindi hicho (Basil Mramba) alisema Watanzania watakula hata nyasi lakini ndege itanunuliwa, Sakata la EPA, Waziri Mkuu alikuwa nani?” alihoji na kujibiwa na umati wa watu, “Sumayeee”.
Aliendelea: “Na wakati wa sakata la Richmond, waziri mkuu alikuwa nani? alihoji na kujibiwa na wafuasi wa chama hicho, “Lowassaaa”.
Hali ilivyokuwa uwanjani
Mkutano huo ulianza saa nane mchana kwa wasanii mbalimbali kutumia jukwaa hilo kwa ajili ya burudani. Wasanii wakongwe waliopotea kwa muda mrefu akiwamo Luteni Kalama aliyekuwa kundi moja na Juma Nature, Bwana Misosi, D Nob walikuwapo, huku ngoma za uswazi zikiteka hisia za wakazi hao kwa burudani waliyoitoa.
Wengine waliokuwapo ni Kimbunga mchawi, Baba Levo huku Zitto Kabwe na Afande Sele wakishangiliwa baada ya kupanda jukwaani kucheza na Bwana Misosi.
Msanii Kala Pina ambaye ni mgombea ubunge wa Kinondoni, alionyesha mbwembwe zake kwa lugha za kisanaa huku akishangiliwa na maelfu ya wafuasi hao.
No comments :
Post a Comment