Haiba ya Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Kijiji cha Umbuji ulipo Jimbo la Uzinin ndani ya Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja unavyoonekana kwenye picha baada ya kukamilika ujenzi wake na kuzinduliwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr Ali Mohammed Shein.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Kijiji cha Umbuji mara baada ya kuuzindua Msikiti wa Ijuma wa Kijiji hicho.
Naibu Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Thabit Nauman Jongo akitoa mawaidha katika hafla ya uzinduzi wa Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji cha Umbuji Jimbo la Uzini ,Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wakisikiliza Hotuba ya Balozi Seif mara baada ya uzinduzi wa Msiku wa Ijumaa wa Kijiji hicho.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al – Hajj Dr. Ali Mohammed Shein amesema ni jambo la faraja kuona kwamba waumini wa Dini ya Kiislamu waliojalaliwa uwezo wanaendelea kujitokeza katika ujenzi wa majengo ya Misikiti na madrasa za Kisasa katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Alisema mwamko huo umesaidia kupata majengo mazuri na ya kisasa kwa mujibu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia kiasi kwamba mazingira ya kufanyia Ibada yanaridhisha katika kuwafundisha vijana Quran n a mafundisho mengine ya Dini ya Kiislamu.
Al-Hajj Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo wakati akizungumza na Waislamu wa mbali mbali mara baada ya kuuzindua rasmi Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji cha Umbuji { Masjid Shuraa } ndani ya Jimbo la Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Al-Hajj Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo wakati akizungumza na Waislamu wa mbali mbali mara baada ya kuuzindua rasmi Msikiti wa Ijumaa wa Kijiji cha Umbuji { Masjid Shuraa } ndani ya Jimbo la Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Alisema Waislamu na Jamii ni mashahidi katika miaka iliyopita Waislamu wa Zanzibar na maeneo mengine Duniani hawakuwa na sehemu muwafaka wakati walipokuwa wakitaka kutekeleza ibada zao.
Alisema mazingira ya sasa yamekuwa bora zaidi kwa kuwapa utulivu waumini wa Dini ya Kiislamu ambapo hufanya ibada zao katika maeneo mazuri yanayotoa fursa kuendelea na ibada hizo hata wakati wa usiku.
“ Leo Mashaallah misikiti yetu na madrasa zetu zina umeme, mifereji, mafeni na vipaza sauti kwa ajili ya kusaidia mawasiliano wakati wa adhana au kupeana mawaidha “. Alisema Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar alisema ujenzi wa msikiti huo ni neema kubwa ambayo waumini wa Kijiji hicho wana wajibu wa kushukuru na kuhakikisha wanautumia vyema katika kutekeleza ibada za sala, kuendesha madrasa, kukuza imani, kuuendeleza Uislamu na kufanya matukio ya Kijamii ambayo yana mnasaba wa kutumia msikiti.
Al-Hajj Dr. Ali Mohammed Shein alieleza kwamba kutokana na kuzidi kutanuka kwa Kijiji cha Umbuji na hatua tofauti za Maendeleo wanazoziendeleza, ni vyema waumini hao wakafikiria kutumia sehemu ya kiwanja kilichobakia katika sehemu hiyo kujenga madrasa kwa ajili ya Vijana wao ambao watapenda kuongeza maarifa katika masuala mbali mbali ya Dini.
Alisema ipo haja ya kuhakikisha eneo lote la ardhi walilopewa kwa ajili ya ujenzi huo linapimwa vyema na kupatiwa hatimiliki pamoja na kusajiliwa katika taasisi zinazohusika.
Aliwanasihi waumini hao kuitunza nyumba hiyo ya mwenyezi Muungu kwa kuwaunganisha wakikumbuka kwamba uwepo wa jengo hilo tukufu ujenzi wake umetokana na Umoja na moyo wao wa kujitolea ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya ujenzi.
Dr. Shein aliwatanabahisha waumini na Wananchi wa Kijiji cha Umbuji kujiepusha na cheche zote zinazoweza kusababisha migogoro kama waumini wanavyoshuhudia katika baadhi ya Misikiti hapa Nchini.
Akizungumzia suala la malezi Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wazazi na Walezi kuendelea kusimamia watoto wao katika misingi ya maadili mema kama yalivyokuwa yakitolewa na jamii zilizopita.
Alisema vijana lazima waaswe kuachana na matumizi ya Dawa za kulevya, wizi na vitendo vyote ambavyo vinaweza kuvunja amani na kuathiri maisha yao ya baadaye.
Katika kuunga mkono juhudi za Waumini hao wa masjid Shuraa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif yeye binafsi aliahidi kusaidia mashine ya kusukumia maji pamoja na ile ya kusafishia mchanga kwenye mazulia kwa ajili ya Msikiti huo.
Akitoa mawaidha katika hafla hiyo Naibu Katibu wa Maufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Thabit Nauman Jongo alitahadharisha kwamba Msikiti lazima upewe heshima yake kwa Waumini kuendelea kukumbushana ili kuutumia katika kufanya Ibada.
Sheikh Jongo alisema Msikiti ni wakfu kwa ajili ya Mwenyezi Muungu . Hivyo Muumini ye yote aliyeamua kujitolea hata kwa shilingi moja katika kuchangia ujenzi wa nyumba hiyo tukufu hakutupa bali ameweka wakfu kwa ajili ya Allah.
Aliwakumbusha na kuwaasa akina Baba kuelewa kwamba wao ndio watakaobeba dhima siku ya hukumu endapo wake na watoto wao watashindwa kuwakumbusha katika kutekeleza Ibada.
Alisisitiza kwamba kwa kuwa wajibu wa kuulinda msikiti uko ndani ya himaya ya waumini wenyewe ni vyema mambo yote ya kidunia ikiwemo ugomvi wakahakikisha kwamba yanaishia nje ya msikiti vyenginevyo watakuwa wamefuata nji ya washirikina wasio na uwezo wa kuimarisha nyumba hiyo tukufu.
Akisoma Risala ya Waumini na Wananchi wa Kijiji cha Umbuji Ustadhi Haji Shauri Issa alisema ujenzi wa Msikiti huo wa Ijumaa wa Kijiji hicho ulioanza Miaka Mitatu iliyopita umekuja kutokana na changamoto ya ongezeko kubwa la Waumini waliokuwa wakifanya ibada katika msikiti wa asili.
Ustadhi Shauri alisema waumini wa Kijiji hicho wamepata faraja baada ya kukamilika kwa msikiti huo uliojengwa kwa nguvu za waumini wenyewe na na kuwashukur washirika mbali mbali wa Dini waliojitolea kuchangia ujenzi huo.
Msjid Shuraa ambao una uwezo wa kusaliwa na waumini zaidi ya 600 kwa wakati Mmoja umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 200,000,000/- za Kitanzania licha ya kuendelea kuwepo baadhi ya changamoto katika kukamilisha msikit .
No comments :
Post a Comment