Kwamba wapo maelfu ya wananchi wanaosimama kudai mabadiliko si jambo geni; kwamba wapo wanasiasa ambao wanavutia watu na kuwapa hamasa ya kudai mabadiliko hayo hili nalo si geni. Vyovyote vile ile ilivyo lazima mahali fulani lifikie kikomo ama kwa kuleta mabadiliko ya kweli au mabadiliko ya kiini macho.
Jambo la msingi na kubwa zaidi ni lazima tujue tunachotaka kubadilisha ni nini hasa? Wapo ambao wanazungumza ambao ukiwasikiliza sana utafikiri wanasema tunataka kubadilisha "sura". Kwamba ukiwaondoa watu wenye sura hii, na mavazi ya rangi ile, na ukiwaondoa watu wenye kuimba hivi au kuimba vile basi tutakuwa tumepata mabadiliko. Unaweza ukadhani tatizo letu ni sura za watawala na siyo sera za watawala.
Ni muhimu sana kudai na kulazimisha kujua wanachotaka kukibadilisha ni nini hasa; ni kitu gani kwa mfano tunataka kibadilishwe sasa hivi; ni kitu gani tunataka wakishika madaraka tu basi kiwe cha kwanza kubadilishwa na tuone kimebadilishwa. Vinginevyo, tutafanya kilichofanywa Zambia; walitaka mabadiliko wakapewa, na baadaye wakataka mabadiliko ya mabadiliko na mwisho wakajikuta wanataka mabadiliko ya mabadiliko ya yale mabadiliko ya kwanza waliyoyataka!
Kumbe muda wote hakukuwa na kilichobadilishwa isipokuwa sura za watawala! Tusije kukuta tunabadilisha sura za watawala wa sasa ili baadaye watoto wetu nao waje kubadilisha sura za watawala wajao waliobadilisha sura za watawala wa sasa! Tutake mabadiliko, tuyadai mabadiliko na tuone mabadiliko ambayo yatatufanya tukubadiliane kuwa "duh nchi imebadilika bwana" na hapo tuwe tunazungumzia kwa uzuri.
MMM
http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/910128-wazo-la-leo-haya-ndiyo-mabadiliko-tunayoyataka-tuyataje-tuyatambue-na-tuyakubali-9.html
No comments :
Post a Comment