Taarifa zilizoifikia Nipashe jana zilieleza kuwa Dk. Slaa atajitoa hadharani leo saa 8:00 mchana wakati atakapozungumza na waandishi wa habari katika hoteli moja maarufu iliyopo maeneo ya katikati ya jiji la Dar es Salaam.
Afisa mmoja wa serikali ambaye ni mmoja wa waandaaji wa mkutano huo wa Slaa aliithibitishia Nipashe jana jioni kuwa mkutano huo upo na waandishi wanakaribishwa kuhudhuria.
Hatua hiyo ya Dk. Slaa kuzungumza hadharani inatarajiwa pia kutoa picha halisi kuhusiana na mustakabali wa mwanasiasa huyo machachari aliyeshiriki kwa kiasi kikubwa kuimarisha upinzani tangu alipopewa madaraka ya kuwa katibu mkuu wa Chadema na kugombea urais mwaka 2010.Dk. Slaa alijiweka kando na kutoonekana hadharani tangu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa alipokaribishwa Chadema akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kisha kupitishwa kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ukawa; nafasi ambayo awali ilikuwa ikitarajiwa kuwaniwa na Dk. Slaa.
Mbali na Chadema, vyama vingine vinavyounda Ukawa ni NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF).
Jitihada za kumpata Dk. Slaa ili kuzungumzia taarifa za mkutano wake na waandishi wa habari leo ziligonga mwamba kwani alipopigiwa kupitia simu yake ya mkononi hakupatikana na hata alipoulizwa kupitia ujumbe mfupi wa simu yake hiyo, bado hakukuwa na majibu.
KUHAMA CHADEMA
Katika hatua nyingine, chanzo kimoja kiliiambia Nipashe jana kuwa kwenye mkutano wake huo wa leo, Slaa ataweka wazi yale yote yaliyo uvunguni mwa moyo wake kuhusiana na kile kilichomlazimu kujiweka mbali na shughuli za chama chake na pia kueleza hatma yake kisiasa.
Aidha, chanzo hicho kimeongeza kuwa upo uwezekano mkubwa kwa Slaa kutangaza kuwa anarudisha kadi ya Chadema.
"Kuna kila dalili kuwa atatangaza kujiondoa uanachama wa Chadema... hiyo kesho ndiyo itajulikana," kilidai chanzo hicho.
Hivi karibuni, mengi yamekuwa yakiripotiwa kuhusiana na Slaa. Kamati Kuu ya Chadema kuridhia uamuzi kuwa apumzike na kuungana nao baadaye pindi wakati muafaka wa kufanya hivyo ukifika.
Nipashe iliwahi kuripoti kuwa Slaa amejiweka pembeni kwa sababu ya kutoridhishwa na mchakato wa kumsaka mgombea urais ndani ya Chadema na Ukawa na kwamba, licha ya jitihada kadhaa za kuzungumza naye, bado alishikilia msimamo wake wa kutounga mkono uamuzi wa kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wa nafasi hiyo.
Ilidaiwa kuwa miongoni mwa wale walisohiriki mazungumzo yaliyogonga mwamba ya kumshawishi Slaa ili akubaliane na uamuzi wa wengi ndani ya Ukawa kuhusiana na uteuzi wa Lowassa kugombea urais ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment