Waziri huyo ameibuka na baadhi ya hoja hizo akizitumia kama ahadi za Chama Cha mapinduzi (CCM) kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Baadhi ya ahadi hizo zilishatolewa na Chama hicho, lakini hazijaanza kutekelezwa hadi sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sitta alimtetea aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrson Mwakyembe akisema kuwa hakuhusika katika sakata la uingizwaji wa mabehewa feki nchi kutoka India.
Wakati wa uzinduzi wa kampeni za Ukawa Jumamosi iliyopita, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, aliaainisha baadhi ya kashfa zilizotokea wakati wa serikali ya awamu ya nne ni ununuzi wa mabehewa 274 nchini humo, kati ya hayo 150 yaliingizwa nchini na mengine 124 kuzuiwa, baada ya kubainika kuwa feki na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 230.Sitta alisema baada ya bodi kupitia taarifa hiyo, ilibaini mabehewa mengi kati yaliyoagizwa yalikuwa na kasoro, kuwepo kwa uzembe katika uagizaji na ufuatiliaji kuanzia kiwandani na uzembe katika mchakato wa kuyapokea.
Vilevile, alielezea kushangazwa na kauli ya Sumaye ya kumtetea Lowassa dhidi ya tuhuma huku akisema zitaibuka kashfa nyingine dhidi ya Serikali.
Sitta alidai kuwa wanayoyasema dhidi ya Lowassa ni ya ukweli na hakuna matusi waliyotumia.
“Mtu akiamua kugombea urais ni lazima achambuliwe, hakuna matusi na kamati (kamati ya kampeni ya CCM) inasema mambo yalivyo hawajamtusi mtu, ” alisema na kuongeaza kuwa:
“Kuna gazeti moja lilisema kamati yetu ni ya kumtusi fulani, hakuna kumtusi mtu hapa tunasema mambo yalivyo, unataka cheo watu wakikuchambua unasema unatukanwa, acha basi kama hutaki kuchambuliwa bila hivyo utafuatiliwa hadi uwani hiyo ndiyo gharama yake gharama ya uongozi ni kufuatiliwa.”
Alipotakiwa na waandishi wa habari kuelezea sababu za kushindwa kutekeleza maazimio ya Bunge katika sakata la Richmond wakati huo akiwa Spika, Sitta alisema:
“Maazimio yalikuwa 26, Bunge siyo chombo cha utendaji, yalitakiwa kusimamiwa na serikali, mara nyingi watu wanakosea wanadhani Bunge ndiyo chombo kinachokamata mtu na kumpeleka sijui wapi.”
Alisema Bunge lilipofikia maazimio liliyakabidhi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa ajili ya utekelezaji.
Alisema baadhi yametekelezwa na mengine walielezwa kuwa uchunguzi wake ni mgumu mpaka waende nje ya nchi.
“Lowassa alitaka kuvunja mkataba upi wa Richmond halafu ni nani kaunda Dowans, hivi mtu akisema anavunja hili halafu kwa hila anaunda nyingine, hilo ni sawa hivi unaiju vizuri hii hadithi? baada ya Richmond ilikuja nini? Dowans ilipataje mkataba si hao hao wafisadi watupu?” alihoji.
Kwa upande mwingine Sitta alisema hoja za upinzani walizotoa wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo katika viwanja wa Jangwani kuwa watajenga reli na kufufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) hazina msingi wowote kwa sababu ni mipango ya serikali.
Alisema pia sakata la ununuzi wa mabewa feki kutoka nchini India halimhusu aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe kama inavyodaiwa na vyama vya upinzani.
Alisema baada ya kuibuka kwa kashfa hiyo, serikali iliunda tume kwenda nchini India kuchunguza na kubaini kuwapo kwa ubadhirifu katika manunuzi uliofanywa na baadhi ya wahandisi wakiwamo baadhi ya viongozi wa wizara hiyo.
Alisema suala hilo lilikuwa ni la kizabuni na waliotumwa kwenda India walikiuka taratibu na kusababisha kutengenezwa kwa mabehewa hayo.
“Hawakuwa makini wakaharibu, tatizo siyo mamlaka kilichokosekana ni uaminifu kwa vijana wahandisi waliotakiwa kusimamia vigezo vyote vya uhandisi katika mabehewa hayo,” alisema.
Sitta alisema baada ya mabehewa hayo kuingiziwa nchini na kubainika kuwa feki, Waziri alilifuatia na kuchukua hatua za kuunda tume hiyo na kufanya uchunguzi huo.
Kuhusu watuhumiwa wa kashfa hiyo, alisema wanatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni, baada ya uchunguzi dhidi yao kukamilika.
Waliosimamishwa kazi kwa kashfa hiyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TLR), Kipallo Kisamfu; Mhandisi Mkuu wa Mitambo, Ngosomwile Ngosomiles; Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa; Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Fedinarnd Soka.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa reli ya kati, alisema utazinduliwa rasmi Septemba 15, mwaka huu.
Alisema Rais Jakaya Kikwete ataweka jiwe la msingi katika eneo la Soga Mpigi mkoani Pwani, utakapozinduliwa ujenzi wa mradi huo.
Alisema gharama za upanuzi huo wa reli ya kati ni unakadiriwa kugharimu Sh. tirioni 16 ambazo zitajenga kilometa 2561.
Sitta alisema ndani ya miaka 10 wanatarajia kusafirisha tani milioni 25 za mizigo kupitia reli ya kati na reli ya kusini tani milioni 35 na kuinua uchumi wa taifa.
Akizungumzia kuhusu Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), alisema serikali imeamua kulipa madeni yake ili liweze kukopesheka.
Alisema serikali inatarajia kuchukua mkopo Benki la Rasilimali (TIB) na kulikopesha shirika hilo kwa ajili kununua ndege nne.
Alisema ndege hizo zitanunuliwa kwa awali ya kwanza mbili na nyingine miezi michache ijayo ili shirika hilo lianze kufanya safari zake.
Serikali ya awamu ya nne ilishaahidi kulifufua ATCL lakini hadi sasa haijafanya hivyo.
Kadhalika, iliahidi kupitia kwa Sitta kuwa ingeanza ujenzi wa reli ya kati kuanzia Juni mwaka huu, lakini utekelezaji huo haujaanza hadi sasa wakati serikali ya awamu hii ikikaribia kutoka madarakani takribani miezi miwili ijayo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment