Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, September 4, 2015

Hatujachelewa kuepushia nchi mitafaruku, ilivyo lolote laweza kutokea!


KAMA kuna neno wakilishi linaloweza kuelezea hali ya mambo tulimo hapa nchini leo, neno hilo ni “Mtafaruku”.
Mtafaruku ni hali ya mkanganyiko, isiyotoa jibu kwa yanayotokea, yasiyotia matumaini na kuzaa hofu kwa yajayo. 

Kiuchumi, pato la mwananchi linazidi kupungua na umasikini kukithiri kutokana na kukumbatia sera za ubinafsishaji, uwekezaji usiojali na uporaji wa rasilimali za taifa usiodhibitiwa kufanya Mtanzania wa leo kuwa masikini kuliko alivyokuwa enzi za uhuru. Ni kazi ngumu sana kutawala watu wenye njaa na wenye manung’uniko.

Kisiasa hali si shwari pia. Mfumo wa vyama vingi ulioshinikizwa kwetu na “wafadhili”, umeligawa taifa kwa misingi ya vyama vya siasa ambapo Chama dola kinawaona wapinzani kama watu wasio wazalendo “wapumbafu” na “malofa” Hata uwakilishi bungeni umegawanyika kwa misingi hiyo, ambapo sasa kuna “hoja za wapinzani” na “hoja za Chama tawala”. Hali inakuwa mbaya zaidi Bunge linapokuwa Spika “Mchama” na mwenye kuongozwa kwa rimoti na wenye uwezo wa kifedha na nia mbaya kwa nchi.

Kero za Muungano nazo zinazidi kuyumbisha Taifa kwa hoja zenye kutaka majibu sahihi badala ya kuzinyamazia. Mapendekezo shirikishi ya Muundo wa Muungano ya Tume ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba, yaliyotokana na maoni na utashi wa wananchi, yametupiliwa mbali na Bunge la Katiba mwaka huu kwa ushabiki wa kivyama na kuzua sintofahamu miongoni mwa wananchi juu ya hatima ya Muungano.
Ukisikiliza kampeni za wagombea urais wetu leo, ndipo utafahamu kiwango cha mtafaruku tulimo: kila mmoja anaahidi kupiga vita rushwa na ufisadi na kumtuhumu mwenzake au awamu ya serikali kwa kulea au kushiriki rushwa na ufisadi kana kwamba wagombea wakuu wawili, Edward Lowassa na John Magufuli, hawakuwa sehemu ya mfumo wa rushwa na ufisadi unaotesa nchi.

Wakati Magufuli ameshindwa kuukana mfumo uliopo na badala yake anaendelea kuusifia akipewa nguvu na marais waliokomaza rushwa hii, Lowassa naye ameingia Chadema na kokoro la viranja wa kale wa rushwa na ufisadi kumpigia kampeni, huku nyangumi wa ufisadi mkubwa nchini akiwasifia kama “role model” – mfano wa kuigwa kwa maendeleo.

Malumbano haya tuyaone kama “vita vya panzi furaha kwa kunguru”, kwamba kadri wanavyozidi kuumbuana ndivyo tutakavyofahamu jinsi walivyofilisi nchi yetu. Ukweli, huu ni mnyukano wa majambazi unaopashwa kumwamsha mwenye nyumba.

Mwandishi Keneth Martin, anaielezea ifuatavyo hali tete tulimo sasa, katika kitabu chake: “French Liberal Thought” ifuatavyo: “Ni jamii iliyochoka na kuchakaa; ni jamii iliyooza na kuchoma pua kwa harufu ya uvundo wa rushwa, ufisadi na ukandamizaji; ni jamii isiyojua mbele wala nyuma, ni jamii iliyokosa dira”.

Anasema, Bunge lilikuwepo kwa jina tu kwa sababu liliwekwa kwapani na watawala; Madaraka ya Mfalme (kama yalivyo madaraka ya Rais hapa kwetu) yalikuwa makubwa kiwango cha kupora demokrasia: “L’ Etat C’es moi”, ulikuwa msemo wa Mfalme kumaanisha “ukiwa Mtawala kamwe usikubali kuwajibika kwa watawaliwa; uwe na kauli isiyohojika”.

Utajiri wa nchi ulikuwa mikononi mwa kikundi kidogo cha “wateule” na watawala kilichowageuza wananchi wadunda kazi wasiofaidi jasho lao. Na pale maandamano ya wanawake wenye njaa yalipopita karibu na Ikulu, Mfalme Louis wa XVI, alisimama ghorofani, akawatazama na kuuliza, “kulikoni?”. Na alipoambiwa kwamba yalikuwa ya “malofa” wenye njaa waliokosa mkate wa kila siku, yeye alijibu: “Kama ni hivyo, kwa nini wasile keki?”.

Ndiyo lugha ya watawala wetu hivi leo; ya kuyaita mabilioni ya fedha wanayomiliki “vijisenti”, au fedha ya mboga, wakati kipato cha Watanzania walio wengi ni chini ya shilingi mia nane kwa siku.

Kama ilivyokuwa kwa Mfalme Louis wa XVI alipoingia madarakani mwaka 1774, ndivyo vivyo hivyo Rais Kikwete alivyokuta hali mwaka 2005 ikiwa tete, yenye miguno tele kwa uongozi kushindwa kutatua matatizo ya wananchi tuliyoyaelezea mwanzo. Nchini Ufaransa ya kale, hali hii ilichochea mapinduzi; na pale saa ilipowadia, watawala wa Ufaransa hawakuweza kuyazuia.

Kama ilivyo hivi leo, jamii ya Kifaransa iligawanyika katika matabaka matatu au “Estates”. Tabaka la kwanza lilikuwa la Viongozi wa Kanisa [the Clergy], likijumuisha maaskofu, mapadri na makasisi. Lilimiliki ardhi na mali nyingi na lisiloguswa. Lilihubiri umasikini kama tiketi ya mtu kufika mbinguni. “….. Heri masikini (wa roho), kwa maana Ufalme wa mbingu ni wao, heri ukiwa mpole, kwa maana utaitwa mwana wa Mungu..….. Jikane kila siku, uchukue vema Msalaba wako; ……. huo ndio mwanzo wa Ufalme wa Mungu……”, lilikariri msahafu.

Tabaka hili liliundwa na watu 100,000 kati ya Wafaransa milioni 25. Hapa kwetu tabaka hili linawakilishwa na wanasiasa, wafanyabiashara na mawakala wa ubepari wa Kimataifa wanaoshinikiza nini kifanyike, sera na aina ya demokrasia kama injili mpya ya ukombozi. Hawahojiki; wana kauli turufu juu ya maisha yetu.

Tabaka la pili lilikuwa la watu wenye vyeo na madaraka (the Nobility), wasiozidi 500,000. Hawa walikuwa matajiri wakubwa, wakitumia nafasi zao kujitajirisha: lilikuwa la watu wenye nasaba bora, waliohodhi nafasi kubwa za kazi na uamuzi serikalini na jeshini, isipokuwa vikosi vya mizinga; walirithisha watoto wao vyeo, kama ambavyo tu tabaka la “wateule” linavyorithisha hapa kwetu leo.

Hapa kwetu, tabaka hili linawakilishwa na watawala mafisadi, wenye kuweka maslahi yao mbele badala ya maslahi ya taifa na umma. Hawa ndio wamiliki wa kampuni hewa mumiani, na yaliyosajiliwa kitapeli kuangamiza uchumi wa nchi; ndio walioiingiza nchi katika mikataba ya kifisadi kama ile ya IPTL, Richmond/Dowans, TRL, Meremeta na mingine. Ndio hao hao ambao kwa ukwasi wao mkubwa, wanaweza kununua Bunge linatunga sheria kwa matakwa na kwa manufaa yao, kama lilivyonunua Bunge Maalumu la Katiba hivi karibuni.

Tabaka la tatu na la mwisho liliundwa na makabwela, walalahoi na wadundakazi kwa msemo wa siku hizi; wakiwamo wachuuzi, wafanyabiashara, wasomi na wakulima wadogo wadogo wapatao milioni 23. 

Hawakuwa na nafasi wala kuota siku moja wataingia tabaka la pili au la kwanza. Asilimia 75 ya wanyonge hao waliishi katika vijishamba vidogo vidogo, ama kama wapangaji (serfs), vibarua au wamiliki kwa adha kubwa ya mfumo wa kidikteta. Waliandamwa kwa kodi lukuki kama anavyoandamwa msaka tonge wa Kitanzania.

Baadhi ya kodi hizo, zilikuwa ni kodi ya Mapato (the tithe), ambayo ni asilimia 10 ya mapato; kodi ya ardhi (the taille), kodi ya kichwa (capitation), na kodi ya kumiliki mali (vingitience) ambayo ilikuwa moja ya sita ya thamani ya mali. Zingine ni kodi ya chumvi (the gabelle), kwa kila mtu mwenye umri kuanzia miaka minane kutakiwa kununua kwa nguvu, angalau ratili nane za chumvi kwa mwaka na kulipia kodi kwa chumvi hiyo. Adhabu ya kutonunua chumvi ilikuwa faini au kifungo gerezani.

Wakulima walitozwa pia kodi ya kusagisha nafaka kwenye vinu vya matajiri, mbali na bei ya kusagisha nafaka zao. Walitakiwa pia kufanya kazi kwenye barabara kuu za mfalme mara tatu kwa wiki (corvee); walitozwa kodi kwa kutumia barabara kuu za wenye ardhi, kama ambavyo nasi tungetozwa, kama mpango wa serikali wa kubinafsisha barabara nchini, uliokusudiwa kutungiwa sheria miaka minne iliyopita, ungepita.

Si hivyo tu, mikate (chakula kikuu) na mvinyo vilitozwa kodi kubwa na kusababisha maisha kuwa magumu kwa walala hoi. Kwa jumla, kodi zilichukua asilimia 65 ya pato la wadundakazi na kuwaacha wakiwa masikini zaidi kuliko mwanzo. Hali hii inamkabili Mtanzania wa leo, wakati “wakubwa” wamesamehewa au kuruhusiwa kukwepa kodi.

Kama ilivyo hapa kwetu, pamoja na kodi hizo, uchumi haukupanda. Sababu ilikuwa ni matumizi mabaya, makubwa na ya anasa ya serikali na Ikulu, wakati jeshi lilitumia zaidi ya asilimia 25 ya bajeti kila mwaka, huku deni la nje likiongezeka na riba ya mikopo ikitafuna zaidi ya asilimia 50% ya Bajeti ya Serikali kufanya Ufaransa nchi isiyokopesheka.

Wakati huo huo, waandishi na wanafalsafa waliandika kushambulia utawala kwa kutojali kilio cha wananchi, kama ambavyo waandishi wa habari hapa nchini wanavyoendelea kuandika, na wasomi makini kujitoa mhanga kuikosoa jamii na serikali inaposinzia ili kuuamsha na kuuelimisha umma. 

Ndivyo yalivyofanya pia makundi haya huko Ufaransa, ambapo watu kama Baron Montesquieu (1689 – 1755) aliandika kushambulia ukubwa wa madaraka na mamlaka ya watawala, na kwa kuendesha maisha kwa jasho la wanyonge. Katika kitabu chake, “The Spirit of the Law”, Montesquieu alitetea mfumo wa mgawanyo wa madaraka kupunguza nguvu turufu za watawala dhidi ya watawaliwa.

Naye Fracois – Marie Arouet, maarufu kwa jina la uandishi, “Voltaire” [1694 – 1788], yeye aliandika kushambulia ukiritimba wa Kanisa, utawala msonge na kwa kanisa hilo kuhodhi ardhi, wakati Jean Jacques Rousseau [1712 – 1788], katika kitabu chake, “The Social Contract”, alibainisha kuwa, watawala hupata mamlaka ya kutawala kwa ridhaa [mkataba] ya wananchi; na utawala unapokiuka au kutotelekeza wajibu wake, unapaswa kuondolewa madarakani sawia.

Uchumi ulipozidi kuporomoka, Louis alimteua Robert Turgot kuwa Waziri wa Fedha ili kuokoa hali. Turgot alianzisha Mpango maalumu wa kurekebisha uchumi (SAP); akapendekeza kuondolewa ubaguzi katika ulipaji kodi, kwa maana ya kodi kwa wote ili kutunisha mfuko wa taifa.

Hapo akawachokoza wakubwa, hakudumu; kwani likaja shinikizo kutoka kwa mke wa Mfalme [first lady], Marie Antoinette, aliyemiliki miradi lukuki pale Ikulu [linganisha na Mifuko ya Ma-First ladies hapa kwetu: Fursa Sawa kwa Wote, WAMA au ANBEM?] kwamba afukuzwe kazi na ikawa hivyo.

Akaingia Jacques Necker; naye akapendekeza kama alivyopendekeza Turgot, yaani kodi kwa wote. Kwa sababu ya kutishia usalama wa “vijisenti” vya mafisadi, Necker naye akapigwa buti.

Akateuliwa Mwanauchumi, Colonne; yeye akapendekeza serikali ikope kwa wingi kutoka nje. Wazo lake likakubaliwa; deni la nje likaongezeka na riba kuitafuna vibaya nchi. Lakini alipopendekeza kuwa wenye kumiliki ardhi nao walipe kodi pia, akafukuzwa kazi hima.

Nafasi ya Colonne ikachukuliwa na Askofu Mkuu wa Jimbo la Toulouse, Lomerie De Briene. Ili kurudisha hadhi ya Serikali iweze kukopesheka, alipendekeza kodi mpya na kulipwa kwa madeni yote ya nyuma. 

Mfalme alikubali pendekezo, lakini Bunge la Paris likakataa kupitisha muswada huo kwamba halikuwa na uwezo huo ila Bunge kuu pekee la tabaka zote tatu [the Estates General]. Hiyo ilikuwa mwaka 1788, na Bunge hilo halikupata kuitishwa tangu 1614.

Bunge hilo liliitishwa Mei 1789, mjini Versailles na kuhudhuriwa na wawakilishi 308 kutoka tabaka la kwanza, 285 kutoka tabaka la pili, na 621 kutoka tabaka la Makabwela. Tabaka la kwanza na la pili walitaka muswada huo upite; makabwela wakakataa katakata; kikao kikavunjika kwa kutoelewana.

Kwa hasira, makabwela hao 621 walicharuka na kukusanyika kwenye uwanja wa Tenesi [Tennis court], wakajitangaza wao kuwa ndio Bunge la Ufaransa. Wala majeshi ya mfalme yalipotumwa kuwatawanya hayakufaa kitu, badala yake baadhi ya askari walitupa silaha na kujiunga na “wanamapinduzi” hao. Serikali ikasalimu amri kwa nguvu ya umma.

Ni katika uwanja huo wanamapinduzi hao wakala kiapo na kutangaza “Azimio la kwanza duniani juu ya Haki za Binadamu”, kwamba: “Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa; wanayo haki ya kumiliki mali, haki ya kulindwa na serikali yao, wao pamoja na mali zao na kutonyanyaswa”.

Pia kwamba: “Sheria ni jambo la utashi wa wengi; kila mmoja anayo haki ya kushiriki moja kwa moja, au kupitia wawakilishi wake [Bunge] kutunga Sheria”.

Vile vile kwamba “Ni marufuku mtu kukamatwa ovyo, kushitakiwa na kufungwa, isipokuwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa”. Bunge hilo lilitambua pia kuwa, uhuru wa kuabudu, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujiendeleza ni mihimili mikuu katika uhusiano kati ya mwananchi na Serikali yake.

Leo, Maazimio haya yanatambuliwa na Katiba yetu [angalia sehemu ya tatu ya Katiba] ingawa utekelezaji wake ni wa mizengwe. Huo ndio ulikuwa mwanzo wa Mapinduzi maarufu ya Ufaransa, 1789, ambayo kisababishi chake kinaelekea kushabihiana na yanayojili nchini mwetu.

Septemba, 1791, Katiba ya Ufaransa iliyokuwa ikingojewa kwa hamu na wanyonge, yenye kubainisha haki za msingi za raia na mgawanyo wa madaraka kati ya utawala, Bunge na Mahakama, ikazaliwa. Utawala wa Kidikteta ukawa umebanwa mbavu; na Oktoba, 1791 pale joto la kimapinduzi lilipozidi kuchoma, Mfalme Louis wa XVI alijaribu kutoroka nchi, lakini akakamatwa mpakani na kurejeshwa Paris, akanyongwa kwa kosa la uhaini.

Watanzania tunajifunza nini kwa historia hii? Ni kwamba, ubaguzi wa kitabaka (kiuchumi, kisiasa na kijamii) unaoanza kushamiri nchini mwetu ni tishio kubwa kwa amani na utulivu. Ufisadi unaolikumba taifa ni tishio kwa usitawi wa nchi, haki na demokrasia kama hatutachukua hatua za haraka na za makusudi kutokomeza jeuri ya pesa na kutowajibika kwa Viongozi [“L’Etat C’es moi”]. 

Ni mbegu haramu inayochipua haraka, inayoligawa taifa kati ya “wateule” na “watwana wadunda kazi”, wasio na uhakika na mlo wa siku, na ambao kwa umasikini wao, jasho la mwili ndiyo maji ya kuoga.
Tunaweza kujidanganya kwa kufikiri kwamba, kwa sababu tabaka hili la chini ni nyonge, “malofa” na halina elimu, kwamba linaweza kufinyangwa finyangwa tutakavyo bila kucharuka siku moja. Huko ni kupotoka kwani kina Montesquieu, Voltaire na Rousseu wa enzi zetu wanafanya kazi kubwa kuamsha watu waliolala, wakati watawala hawataki hilo kwa hofu kwamba “ukimwamsha aliyelala utalala wewe”.

Kuna kila dalili kwamba historia ya Ufaransa inaweza ikajirudia katika mazingira yetu, kwani Kero zinapokithiri bila kushughulikiwa, umma haujui nguvu ya Jeshi ambalo hata hivyo ni la watoto wa wasaka tonge hao hao wanaolalamika.

Kuna sauti nyuma, inayosikika daima bila kukoma, kama asemavyo mshairi, Profesa Kulikoyela Kahigi [MB] ikisema: “Imbeni juu ya haya na mengineyo/Lakini msisahau kuimba Juu ya hofu na mkanganyiko/Iwatatao watu mioyoni. Juu ya domo la wanasiasa,/Na uhalali wa hali halisi Imbeni, imbeni waimbaji/Macho ya watu yazidi kufunuka wajitome uwanjani watende.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/hatujachelewa-kuepushia-nchi-mitafaruku-ilivyo-lolote-laweza-kutokea#sthash.INFP97xZ.dpuf

No comments :

Post a Comment