Dar es Salaam. Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema wanaodhani wanatumika CCM wamekosa mwelekeo kwani alikuwa kinara wa kuitaka itoke madarakani.
Profesa Lipumba aliyekuwa mwenyekiti mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alijiengua kwenye wadhifa huo kwa kile alichodai nafsi yake itamhukumu kwa kumkaribisha kundini, Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
Lowassa aliyejiunga na Ukawa Julai 28, amepitishwa na vyama vya Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi kuwania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Akizungumza juzi usiku kwenye mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha Azam, Profesa Lipumba alisema wanaosema wanatumika hawana hoja kwa kuwa walipambana kuitoa CCM madarakani.
“Hivi inaingia akilini kweli? Unapambana kuitoa CCM madarakani halafu hao hao uliokuwa unawapiga, wakutumie kuitetea?,” alihoji Profesa Lipumba.
Akizungumzia msimamo wake, Profesa Lipumba alisema dhamira yake inamsuta kuendelea kubaki ndani ya umoja huo kwa kuwa bado anakumbuka mapambano waliyokuwa wakiyafanya dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma na uadilifu huku akidai kwa sasa ajenda hiyo haipo tena kwenye upinzani.
“Hivi wapinzani watazungumzia kuhusu ufisadi? wanasimamia wapi kwenye uadilifu?,” alihoji Profesa Lipumba wakati akihojiwa kwenye televisheni hiyo.
/Mwananchi.
No comments :
Post a Comment