Akizungumza kwenye hafla fupi ya kufunga mafunzo ya wataalamu katika masuala ya ukame, kilimo, mafuriko na moto wa misituni iliyohusisha sekta mbalimbali nchini, Mkurugenzi wa TMA, Agnes Kijazi, alisema kuwa tangu walipotoa utabiri wa hali ya hewa kwa kipindi cha mvua za vuli (Oktoba mpaka Desemba), wameendelea kufuatilia mabadiliko ya joto katika Bahari ya Pacifiki na kugundua joto linazidi kuongezeka na kwa sasa limefikia nyuzi joto 2.5 juu ya wastani.
Alisema kuwa kuongezeka kwa joto magharibi mwa Bahari ya Hindi mpaka kufikia nyuzi joto 2.0 na kupungua kwa joto mashariki mwa Bahari ya Hindi ni wazi maeneo mengi ya nchi yatakumbwa na mvua kubwa huku ukanda wa bahari ya Pacifiki kukitarajiwa kuwa na mvua za El- nino.“Tunaendelea kusistiza juu ya mvua hizi kubwa ambazo zitaanza kunyesha nchini kuanzia Oktoba, ni vizuri mamlaka husika kuanza kuchukua hatua za kujihadhari sasa hivi tunavyoelekea kwenye msimu wa mvua,” alisema.
Alisema kuwa TMA inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wakiwamo wakulima, wafugaji na mamlaka za wanyamapori, sekta za maji na afya watafute na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika juu ya kukabiliana na hali hiyo ya mvua kubwa inayotarajiwa nchini.
Akizungumza na washiriki 27 kutoka sekta mbalimbali waliodhurua mafunzo hayo, Kijazi, alisema kuwa malengo ya mafunzo hayo yamefikiwa na wahusika wayatumie katika kuboresha utendaji wao wa kazi katika taasisi zao.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment