dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, September 11, 2015

Uchaguzi:Tutendeane haki, na tuonekane tunatendeana haki!

Na Jenerali Ulimwengu
WATANZANIA, kwa mara nyingine tena, tumeingia katika hamasa ya uchaguzi kwa kishindo, na kila kona ya nchi inarindima kutokana na harakati za kampeni zinazoendeshwa na vyama vya siasa.

Ingawaje tunavyo vyama kadhaa vya siasa, lakini inaelekea ushindani mkubwa, angalau kwa sasa, utakuwa baina ya chama-tawala, CCM na muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi, Ukawa.

CCM ndicho chama kikubwa na kikongwe kuliko vingine vyote, kikiwa ni mrithi wa moja kwa moja wa muungano wa mwaka 1977 kati ya Tanganyika African National Union, TANU ya upande wa Tanganyika Afro-Shirazi Party, ASP, ya upande wa Zanzibar.

Kwa ukongwe wake na kwa uzoefu wake wa kisiasa wa zaidi ya nusu karne, CCM inayo mitaji kadhaa ya kisiasa inayoweza kuitumia kuwashawishi wananchi waichague kwa mara nyingine tena. Vyama vingine, kwa upya wake, havina mitaji kama hiyo kwa sababu umri wake hauzidi miaka ishirini tu, na wala havijawahi kushika madaraka na mitandao yake nchini bado ni dhaifu.

Hata hivyo, ukongwe madarakani unaweza pia kuwa ni aina fulani ya mzigo kwa chama hicho, hususan pale inapoonekana kwamba kimeshindwa kutatua matatizo makubwa ambayo kilikwisha kuahidi mara nyingi kwamba kingeyatatua. Hili ni tatizo ambalo haliwezi kuviathiri vyama vya upinzani kwa sababu ndiyo kwanza vinaomba kupewa majukumu hayo.

Jambo moja linajitokeza kwa nguvu kila kona ya kampeni, nalo ni hoja ya kutaka mabadiliko. Ukawa wamekuwa wakisisitiza kwamba wanataka kufanya mabadiliko, na mabadiliko hayo wanasema yatapatikana tu kupitia kuing’oa CCM madarakani na kuweka utawala utakaotokana na upinzani wa sasa.

Hata mgombea urais kupitia CCM anasisitiza umuhimu wa mabadiliko makubwa katika mambo kadhaa, hususan anapoahidi kupambana na rushwa na uzembe kazini, kiasi kwamba mtu anaweza kushangazwa na waziri wa chama kile kile kilicho madarakani kufanya kampeni kwa maneno yanayotaka kumwonyesha kama tofauti na chama anachokiwakilisha na serikali anayoifanyia kazi hivi sasa.

Hii lugha ya mabadiliko inayosemwa na pande zote bila shaka ina maana yake, na maana yake ni kwamba wote wanaofanya kampeni hizi wanajua, ama wanahisi, kwamba wananchi wanataka sana mabadiliko. Wanataka mabadiliko kwa sababu hali zao za maisha ni mbaya, umasikini umewaelemea na hawana matumaini.

Miaka kumi iliyopita wananchi wetu walipewa matumaini makubwa na wakapiga kura nyingi kumchagua mgombea wa chama-tawala aliyewafanya wafikiri kwamba njozi zao za kuondokana na maisha duni zingetimia. Leo hii njozi hizo zimegeuka kuwa majonzi na kile kilichonadiwa kama “Maisha Bora Kwa Kila Mtanzania” kimegeuka kuwa mzaha mchungu.

Mabadilko yanaweza kuja kwa njia nyingi na kuchukua sura tofauti. Mabadiliko makubwa yatatokea iwapo wapinzani watashinda, ambayo itakuwa na maana kwamba CCM inaondoka madarakani. Hayo yatakuwa ni mabadiliko ya jumla kwa kuwa itakuwa ni mara ya kwanza kwa chama kilichokaa madarakani tangu Uhuru kuangushwa katika Uchaguzi Mkuu.

Mabadiliko yanaweza kutokea iwapo upande mmoja utashinda katika kura za urais lakini upande wa pili ukashinda wingi wa viti bungeni. Lakini pia yanaweza kutokea mabadiliko iwapo upande mmoja utashinda urais na wingi wa viti bungeni, lakini tofauti ya wingi wa viti bungeni kwa vyama ikawa ni ndogo sana kiasi cha kuzipa pande zote nguvu karibu sawa.

Hali kama hiyo inaweza kukilazimisha chama-tawala, kiwe hiki cha sasa ama kingine, kisiweze kutawala kwa imla, na kikalazimika kutafuta mwafaka kila mara kinapotaka kufanya uamuzi mkubwa. Hilo peke yake litapunguza jeuri ya watawala inayotokana na ukiritimba ndani ya Bunge.

Pasi na shaka, iwapo vyama vinavyounda Ukawa ndivyo vitaibuka na ushindi, mabadiliko makubwa yatafanyika kwa sababu itakuwa ni msemo wa “msitu mpya na komba wapya.” Lakini jambo kubwa zaidi litakuwa ni lile linalohusu “Katiba ya Wananchi”.

Itakumbukwa kwamba zoezi la kuandika Katiba mpya liliendeshwa kwa njia ya kushangaza, na hatimaye halikufikia tamati yake. Hadi sasa wananchi hawajaambiwa ni hatua gani zoezi hilo limefikia, iwapo bado linaendelea, limekoma, limepumzika, limekwama au limekufa. Kwamba wakuu wetu wanaweza kutuingiza katika zoezi la mizungu kama walivyofanya ni jambo la kusikitisha kwa sababu ya hasara kubwa tuliyoingia na matokeo sifuri tuliyoyapata kutokana na fedha zote zilizoteketea.

Ni katika mvurugano uliotokea kutokana na mchakato wa uandishi wa Katiba kuvurugwa kwa njia za kushangaza ndiyo Ukawa ulizaliwa kama chombo cha kuunganisha nguvu za upinzani katika kudai kuandika katiba inayofanana na mapendekezo ya wananchi kama yalivyokusanywa na kuratibiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) chini ya mwenyekiti wake, Joseph Warioba.

Hivyo, ushindi kwa vyama vya Ukawa utakuwa umefungua milango kwa mjadala juu ya Katiba kuendelea na labda kufikia tamati yake kwa “Rasimu ya Warioba” kufikishwa mbele ya wananchi na kupigiwa kura. Hata katika sura ile niliyoiongelea hapo juu, ya kuwa na uwiano mzuri baina ya chama-tawala na upinzani bungeni, hilo linawezekana pia kwa sababu, kama nilivyosema, watawala watalazimika kutafuta mwafaka kwa masuala yote muhimu.

Kwa jinsi ninavyozifuatilia kampeni, napata mwelekeo wa uchaguzi mgumu kwa pande zote mbili, na pia naona ufinyu wa tofauti baina ya pande hizo. Sioni upande mmoja ukipata ushindi wa kishindo na upande mwingine ukionekana umepitwa “kama umesimama”. Matokeo hayatapishana sana.

Katika hali kama hii ni muhimu kujenga mazingira thabiti ya uwazi. Wakati tofauti kati ya mshindi na washindani wake inakuwa nyembamba, kunakuwa na umuhimu mkubwa wa kila kitu kufanywa waziwazi ili kuondoa wasiwasi unaoweza kutanda kwamba kura “zimechakachuliwa.”

Kwa bahati mbaya, sehemu nyingi za Bara la Afrika bado hazijafikia viwango vya uungwana wa kuandaa ushindani na kutendeana haki baina yetu kama washindani; tunaangaliana kama “maadui”, na neno hilo ndilo hutumika mara nyingi kuwaeleza wale tunaopingana nao.

Sababu ya uhasama huu ni kwamba, kwa kawaida katika nchi zetu, upande unaoshinda ndio unaochukua kila kitu. Peke yake, unaunda serikali, kutoka kuteua baraza la mawaziri hadi katibu kata, unajaza nafasi zote za utendaji, unagawa tenda na fadhila nyingine kwa kupendelea waliokuunga mkono, nk. Ushindi katika uchaguzi ni tiketi ya wale walioshinda kula. Kushindwa ni tiketi ya kufa njaa. Hii ina maana uchaguzi ni suala la kufa na kupona.

Hali iko tofauti kwa wenzetu walioendelea, kwani kwao nafasi ya uongozi ni nafasi unayopewa kwa sababu wenzako wamekuona una upeo, uwezo, maono na ari, na kwamba unaweza kuwafanyia kazi yao vizuri. Wanakupima na kukutathmini kwa muda maridhawa na kujua wewe ni mtu wa aina gani na nini unaweza kuwafanyia. Huna sababu ya kuuza nyumba yako na kuwafanya watoto wako wasile kwa sababu eti unagombea “uongozi” na unahitaji pesa za kununua kura.

Lakini kwa Waafrika hii ni tofauti. Mgombea anauza nyumba yake moja tu aliyonayo. Anauza shamba. Kama ana gari ataliuza, kila anachoweza kuuza atakiuza, na juu ya yote hayo atachukua mikopo ambayo kwa vyovyote vile hawezi kuirejesha. Anaposhindwa katika uchaguzi huo ni kama dunia yake yote imeteketea, na akipata watu wa kumchochea anaweza akaanzisha vurugu zitakazosababisha maangamizi ya watu wengi.

Kwa hiyo uchaguzi wetu unabeba hisia kali kwa sababu sisi hatujaelewa sawa sawa maana ya uongozi, na kwa sababu “uongozi” ni ajira na njia ya kupatia maisha ya mtu, tunakuwa wakali tunaposhindwa kwa namna ambayo inatufanya tuamini kwamba tumeonewa.

Hili ni jambo la kuangalia kwa umakini mkubwa na kuhakikisha kwamba tunatendeana haki. Wakati wenyewe wa kuhakikisha tunatendeana haki ni sasa. Kwa mfano nilianza kupata wasiwasi pale wakuu wa jiji walianza kuwaambia Ukawa hawawezi kufanya mkutano wao wa uzinduzi wa kampeni katika viwanja vya Jangwani wakati wenzao wa CCM walikwisha kufanyia uzinduzi wao papo hapo. Kwa bahati nzuri hilo lilitatuliwa kwa muda mwafaka.

Lakini hata kabla ya hapo, wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM yalisikika maneno ya kebehi na matusi kama “wapumbavu na malofa” yakitolewa na watu waandamizi ndani ya chama-tawala. Maneno kama hayo yameendelea kusikika kutoka sehemu kadhaa.

Ni vyema wakuu wa vyama na wapenzi wao wakajiepusha na maneno hayo. Ingefaa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) ianze mapema kutoa miongozo ili maneno yasiyo na murua na matendo mengine yanayoweza kuashiria uvunjaji wa amani yazuiliwe, na kama yakitolewa yakemewe ili tufike kwenye uchaguzi na tukivuke kipindi hiki kwa amani.
Itaendelea
- See more at: http://raiamwema.co.tz/uchaguzitutendeane-haki-na-tuonekane-tunatendeana-haki#sthash.x874ac5C.dpuf

No comments :

Post a Comment