- Ni elimu, afya, ajira na kilimo, wadau waponda, wahoji utekelezaji wake
Dar es Salaam. Zikiwa zimepita takribani siku 13 tangu kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na CCM, vinachuana vikali kujinadi kwa wananchi katika ajenda nne.
Mbali na vyama hivyo vikuu, ajenda hizo ambazo ni elimu, afya, ajira na kilimo, zinatumiwa pia na chama kipya cha ACT –Wazalendo ambacho kinajinadi kuwa kina tofauti kubwa na vyama vya upinzani pamoja na vingine vilivyokwishazindua kampeni zake, yaani Tanzania Labour (TLP) na Alliance for Democratic Change (ADC).
Kazi kubwa ni jinsi vyama hivyo vitakavyotekeleza ajenda hizo zinazohusu maisha ya kila siku ya Watanzania.
Elimu
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli anasema atasimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 kwa kuandaa mfumo, muundo na taratibu nyumbufu za kutoa elimu ya awali na ya msingi bila malipo.
Dk Magufuli amekuwa akiahidi elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne, ikiwa ni utekelezaji wa sera mpya ya elimu.
Lakini Chadema wamekwenda mbali zaidi. Mgombea urais wa chama hicho na Ukawa, Edward Lowassa, ambaye ajenda yake kuu ni elimu, ameahidi kutoa elimu bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu.
“Serikali ya Ukawa itasimamia ubora wa viwango vya elimu kote nchini, kuimarisha taaluma na mitalaa shuleni, kuondoa utoro darasani na kuboresha afya za wanafunzi,” alisema Lowassa katika moja ya mikutano ya kampeni.
Alisema ataboresha masilahi na vitendea kazi kwa walimu ikiwa ni pamoja na nyumba, posho ya kufundishia, usafiri na zana za teknolojia.
Kwa upande wake, mgombea urais wa ACT – Wazalendo, Anna Mghwira alisema chama chake kitaweka mfumo wa motisha kwa walimu utakaozingatia utendaji na mafanikio katika kuwawezesha wanafunzi kujifunza.
Vilevile, chama hicho kitaanzisha mfumo nyumbulisho wa usaili katika vyuo vikuu ili kuongeza idadi ya wahitimu wenye sifa za kujiunga navyo huku kikiongeza idadi ya shule za sekondari za juu kwa ajili ya kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu.
Afya
Katika sekta ya afya, vyama vinavyounda Ukawa vinasema afya na tiba ya kila Mtanzania itagharamiwa kupitia bima za gharama nafuu na mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuimarisha afya ya msingi na kupunguza gharama za tiba.
“Serikali itahakikisha kuna uwiano na upatikanaji wa watumishi wa afya katika kada mbalimbali ili kuleta tija na huduma stahiki. Itaimarisha miundombinu ya afya pamoja na kujenga hospitali za kisasa ili kusogeza huduma za afya karibu na jamii na pia kuepuka kupeleka wagonjwa nje ya nchi,” alisema Lowassa.
Waziri huyo mkuu wa zamani alisema Ukawa pia itadhibiti ongezeko la gharama za huduma za afya bila kuathiri uendeshaji wa watoaji wake, ikiwamo Serikali na hospitali binafsi.
CCM inaeleza katika ilani yake kuwa itajikita kuendeleza utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (MMAM) wenye lengo la kuimarisha na kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Chama hicho kikongwe kimesema kitahakikisha kuwa suala la kila kijiji kuwa na zahanati, kata kuwa na vituo vya afya na wilaya kuwa na hospitali, litaendelea kutekelezwa wakati hospitali za rufaa za mikoa, zikiimarishwa.
Pia, CCM imesema itagawa bure vyandarua zaidi ya 22,360,386 vyenye viwatilifu na kuajiri wataalamu wa afya wengi pamoja na kutoa motisha kwa watu wanaofanya kazi katika mazingira magumu.
ACT-Wazalendo inasema itachukua hatua za dharura kuimarisha huduma za mama na mtoto katika vituo vya afya ili kuzuia vifo vya watoto na mama wajawazito. Itafanya hivyo kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wahudumu wa afya katika vituo vya afya na hospitali zote.
“Katika siku 100 za mwanzo za utawala wa ACT, itaunda tume ya wataalamu katika sekta ya afya na uchumi kuainisha huduma za msingi za afya kwa mama na mtoto ambazo serikali itazigharamia. Hizi zitaleta tija katika kumaliza vifo visivyo vya lazima kwa watoto na mama wajawazito,” inasema ilani hiyo.
Ardhi na kilimo
Ukawa imesema itaimarisha mfumo wa umiliki wa ardhi kwa Watanzania na kudhibiti migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na kupima ardhi yote ya Tanzania, sambamba na kumilikisha vijiji kwa hati za Serikali ili kuipa ardhi thamani.
“Tutakuza kilimo cha umwagiliaji kwa kuwapa wakulima elimu ya kuvuna maji na kujenga miundombinu husika na pia tutawapa mikopo ya riba nafuu,” alisema Lowassa.
Kuhusu kilimo na ardhi, ACT-Wazalendo inasema itajenga uchumi wa kilimo na ufugaji ikilenga kuwawezesha wakulima wadogo kugeuza kilimo kuwa mtaji wa biashara ili kukifanya kiwe chanzo cha chakula na mahitaji muhimu ya kiuchumi na kijamii. Chama hicho kinasema kitatoa elimu kwa wananchi kuhusu ufugaji bora na wa kisasa ili kuleta tija.
ACT- Wazalendo pia imekuja na vipaumbele vya kusimamia nishati ya gesi, kuboresha sekta ya utalii, kuimarisha uwekezaji kujenga viwanda, kujenga reli ya kati, kuboresha bandari na kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Kuhusu ardhi, ilani ya CCM inaeleza kuwa itawapa wananchi hatimiliki za kimila milioni 2.5 pamoja na kujenga masjala za ardhi 250 katika ngazi za wilaya. Pia, itatoa hatimiliki milioni mbili na kusajili nyaraka nyingine za kisheria.
“Ili kuhakikisha wananchi wasio na ardhi wanaipata, chama hicho kitafanya uhakiki wa mashamba pori yasiyoendelezwa kwa kipindi kirefu na kugawa upya kwa wananchi,” inaeleza ilani hiyo na kuongeza kuwa pia itaimarisha upatikanaji wa pembejeo za zana za kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Maoni ya wadau
Pamoja na vyama hivyo kujinadi katika maeneo hayo manne, wachambuzi wa siasa wanaona bado havijaeleza mikakati ya jinsi ya kutekeleza mipango hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa taasisi ya Haki Elimu, Godfrey Boniventura alisema ilani za vyama vya siasa zimegusia masuala ya elimu, lakini hakuna ambacho kimeeleza mikakati ya kupata fedha za kuigharimia.
Alisema mgombea urais anapaswa kusema namna atakavyosaidia kukuza elimu kuanzia ya awali mpaka chuo kikuu, huku akiainisha atakavyofanikisha upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.
Boniventura alisema kutokana na taaluma ya ualimu kupoteza hadhi katika jamii, mgombea urais awaeleze wananchi namna atakavyorejesha hadhi ya walimu ili kuhakikisha wanakuwa na ujuzi wa kutosha na kufundisha kwa ari na nguvu.
“Ukiwa na gari lazima uwe na dereva mzuri, la sivyo gari haliwezi kufika unakokwenda,” alisema.
Pia, alisema amesikiliza na kusoma baadhi ya ilani za vyama vya siasa na kugundua kuwa hakuna kinachozungumzia namna kitakavyoongeza bajeti ya elimu hadi kufikia asilimia 30 kwenye fedha za maendeleo tofauti na ilivyo sasa.
Kuhusu elimu bure, alisema iwapo hilo litafanikiwa Serikali italazimika kuvunja Bodi la Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na kuigeuza kuwa bodi ya kusaidia wanafunzi kifedha kusoma bure.
Katibu wa Umoja wa Wamiliki wa Shule na vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Kanda ya Dar es Salaam, Moses Kyando alipongeza baadhi ya vyama vya siasa ambavyo vimesema vitaunda tume ya walimu itakayoshughulikia masuala yote yanayohusu elimu nchini.
Hata hivyo, alisema ili mpango huo ufanikiwe ni lazima wadau wa sekta ya elimu wahusishwe katika mchakato wa kupatikana kwa chombo hicho kwa sababu Sheria ya Tume ya Walimu iliyopitishwa hivi karibuni ina baadhi ya mambo ambayo yatawabana walimu.
Kuhusu vyama kuahidi kutoa elimu bure, Kyando alisema jambo hilo linavutia kulisikiliza masikioni, lakini utekelezaji wake ni mgumu kwa kuwa watendaji serikalini ni walewale ambao kwa muda mrefu wameshindwa kusimamia sekta hiyo.
“Hata akiingia kiongozi mpya, mfumo bado ni uleule labda baada ya miaka mitano ndipo tutaanza kuona mabadiliko, bahati mbaya wananchi hatuna subira tunataka matokeo ya haraka,” alisema Kyando.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Nicholas Mgaya alisema serikali ijayo iweke msisitizo kwenye suala la ajira kwa kujenga mazingira mazuri yanayovutia wawekezaji.
Alisema Serikali haina budi kushirikiana na sekta binafsi kwa sababu ina mchango mkubwa katika kutoa ajira kwa wananchi wengi kupitia juhudi mbalimbali za uwekezaji walizozianzisha nchini.
No comments :
Post a Comment