Ilani ni kitabu cha mwongozo chenye jumla ya mambo yanayoaminika yametafakariwa kwa kina na waandaji wenye chama chao cha siasa na yanayopaswa kuelezwa na kueleweka kwa waandaliwa, kwa maana ya wapiga kura.
Kwa kifupi kabisa, Manifesto au Ilani ni mkataba baina ya wananchi na chama cha siasa na wagombea, wenye dhamira ya kutaka kushika dola kwa ridhaa ya wananchi hao wenye nchi yao.
Ndiyo maana kila chama cha siasa chenye dhamira ya kweli ya kutaka kushika dola, hulazimika kuandaa Manifesto au Ilani yake kwa ajili ya kuiuza na kuinadi vyema kwa wananchi ili kama wananchi hao wakiyakubali yote yaliyomo ndani ya Manifesto hiyo, basi wanafanya uamuzi wa kukichagua chama na mgombea wake wa urais.
Ni kupitia Manifesto hiyo wananchi wa taifa husika wanakuwa wanatambua ni wapi taifa lao ninataka kuelekea chini ya uongozi wa chama fulani na mgombea wake fulani wa urais.
Ni kupitia Manifesto hiyo, wananchi huweza kuifanyia tathimini serikali yao kama kweli imeyazingatia na kuyatimiza yale yote yaliyomo ndani, ambayo kimsingi ndiyo makubaliano hasa ya kimkataba baina ya serikali iliyoundwa na chama kilichopewa ridhaa ya kuongoza.
Kwa hiyo, chama cha siasa makini, kote duniani, hutoa umuhimu wa hali ya juu katika siku yake ya uzinduzi wa Ilani yake ya uchaguzi.
Umuhimu huo unakuja kutokana na ukweli kwamba kila mwananchi, kila mpigakura
katika taifa husika anakuwa na hamu ya kusikia na kujua Ilani za vyama vya siasa vinavyoshindana ili aweze kuziweka kwenye mizani Ilani hizo ni ipi yenye ubora na unafuu kwa maisha yake yajayo.
Kimsingi kabisa, siku ya Uzinduzi wa Ilani, ndiyo siku ambayo mkataba baina ya wananchi na chama cha siasa pamoja na mgombea wake, unafungwa. Chama cha siasa kikiboronga siku hiyo ya uzinduzi wa Ilani yake, maana yake kimeshindwa hata kabla ya kuanza kampeni.
Wananchi wanataka wasikie na waielewe Ilani ya mgombea urais na chama chake siku hiyo ya kwanza ya uzinduzi na huko mbele ya safari kwenye kampeni inabakia kuwa jukumu la mgombea na chama chake kujibu hoja zinazotokana na yaliyomo kwenye Ilani yao, hasa katika maeneo yenye utata na yale ambayo hayaeleweki vyema.
Taifa letu liko kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu. Kampeni hizo ndiyo kwanza zimeanza. Tayari vyama vya kadhaa vimefanya uzinduzi rasmi Ilani zao.
Kilianza Chama cha Mapinduzi (CCM) na mgombea wake wa urais, Dk John Magufuli, Agosti 23, mwaka huu, katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam. Kasha kilifuata Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mgombea wake wa urais, Edward Lowassa, Agosti 29,mwaka huu, katika Viwanja hivyo hivyo vya Jangwani.
Tumeshuhudia pia Ilani ya ACT-Wazalendo ikizinduliwa Agosti 30 katika Viwanja vya Zakhim Mbagala, Dar es Salaam.
Ni dhahiri kamati zote za uhamasishaji za vyama vyote vitatu zilifanya kazi nzuri ya kuhamasisha watu wengi kwa kadri walivyoweza kujitokeza kwenye mikutano hiyo ya uzinduzi wa Ilani. Vyote vilikuwa na watu wa kutosha kabisa.
Hoja yangu hata hivyo si ya wingi wa watu bali ni chama gani kilichoitumia vyema siku hiyo, na ni chama gani kilichoitumia vibaya!
Chadema na mgombea wake Lowassa, kama ni kutoa maksi za darasani,ningekipa maksi za chini kabisa. Chadema na mgombea wake Lowassa, walishindwa kukidhi matarajio ya Watanzania walio wengi, na kwa hakika kabisa, tukiacha ushabiki na unafiki, uzinduzi wao wa Ilani uliwakera wengi.
Pengine, inawezekana ni kwa sababu ya kutambua hilo la kushindwa kukidhi matarajio ya maana yenyewe ya siku hiyo, ndiyo maana mgombea
wake wa urais, Lowassa, siku hiyo hiyo aliamua kununua muda mwingine wa ziada saa tatu usiku kwenye Kituo cha Televisheni cha ITV ili
kufafanua Ilani yake.
Alikwishakuchelewa!
Ndugu zangu, chama cha siasa makini, kilichokaa na kuandaa Ilani yake ya uchaguzi kwa miaka yote mitano iliyopita, hakiwezi kuitisha umati wote ule tulioushuhudia pale Jangwani, halafu Ilani yake hiyo ikaelezwa na kufafanuliwa kwa chini ya dakika 15.
Ndugu zangu, chama cha siasa makini, kilichokaa na kuandaa Ilani yake ya uchaguzi kwa miaka yote mitano iliyopita, hakiwezi kuitisha umati wote ule tulioushuhudia pale Jangwani, halafu Ilani yake hiyo ikaelezwa na kufafanuliwa kwa chini ya dakika 15.
Naliona hilo kuwa ni mzaha na dosari kubwa kwa sababu maelfu yale ya
wakazi wa Dar es Salaam na Mikoa jirani, walioanza kufurika katika Viwanja vile vya Jangwani tangu saa moja asubuhi wakisubiri kusikia Ilani ya chama chao pendwa, hawawezi wakahutubiwa na mgombea wao wa urais, mwenye jukumu kubwa la kuelezea dira mpya ya serikali atakayoiunda kupitia Ilani yake kwa dakika 12 kwa kisingizio cha muda. Walipokuwa wakipanga ratiba hawakujua ukomo wa muda?
Lakini pia suala la Uzinduzi wa Ilani ya Uchaguzi, si jambo la dharura. Ni suala la kuandaliwa kwa miaka mitano kabla ya uchaguzi.
Siku ya Uzinduzi wa Ilani, ilipangwa muda mrefu na viongozi wa Chadema, kwa hiyo walipaswa kujua wana wazungumzaji wangapi na watachukua muda gani ili kumpa nafasi mwenye dhamana kuu ya kusimamia Ilani aweze kuielezea kwa umma wa Watanzania.Wamwone na wamsikie akiinadi ili wote waunganishwe na umahiri wa muwasilishaji, wamuamini kwamba ayasemayo yanatoka moyoni na kweli wakimpa ridhaa atatenda vivyo.
Walau, hata kama kuna upungufu, hivyo ndivyo wengi wetu tulivyoona katika siku za uzinduzi za CCM na ACT- Wazalendo.
Mgombea urais wa ACT-Wazalendo, Anna Mgwira, katika uzinduzi wa Ilani yao kwa mwaka 2015-2020, aliweza kutumia vyema siku hiyo kuinadi Ilani kwa takriban dakika 28 kutoka saa 11.37 hadi saa 12.05.
Alifafanua mambo muhimu yaliyomo ndani ya Ilani na yakaeleweka vyema. Vivyo hivyo kwa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli aliweza kutumia zaidi ya saa moja na zaidi kuelezea mambo muhimu ambayo yatasimamiwa na serikali yake atakayoiunda kama atapata ridhaa ya Watanzania pamoja na wapi anatarajia kuipeleka nchi yao.
Dk. Magufuli alitumia muda huo, ambao hata hivyo haukumtosha kuelezea
maeneo 32 ya msingi yanayobeba Ilani yake anayoendelea kuinadi kwa
wananchi mikoani yeye mwenyewe, mgombea mwenza wake Samia Suluhu Hassan na Kamati yake ya Kitaifa ya Kampeni za CCM 2015. Kama ni maksi darasani, kwangu ACT-Wazalendo na CCM, wangepata zaidi ya asilimia 80!
Mwishoni mwa wiki hii iliyopita, ambayo Chadema walifanya uzinduzi wa Ilani yao, mgombea anayetafuta urais wa Marekani kupitia chama cha Republican, Donald Trump (69), alitumia zaidi ya saa moja, kwa maana ya dakika zaidi ya 60, kuelezea Ilani yake binafsi katika yale mambo ambayo vyombo vya habari vya nchi hiyo vimeyaita “The 10 best lines from Donald Trump's speech.”
Katika mambo yake hayo 10 ya kipaumbele, msaka urais huyo kwa tiketi ya Republican ameelezea mambo muhimu ya ndani ya nchi yake kisiasa, kijamii na kiuchumi, pamoja na sera yake ya mambo ya nje, hasa kuhusu Taifa la China na Wachina akisema:
“People say you don’t like China. No, I love them. I’m not saying they’re stupid. I like China. But their leaders are much smarter than
our leaders.” Kwa tafsiri yangu isiyo rasmi, msaka urais huyo wa Republican katika uchaguzi huo wa mwakani wa Marekani, anasema:
“Watu wanasema siwapendi Wachina. Hapana, nawapenda. Sisemi kwamba wao ni wapumbavu, naipenda China. Hata hivyo, viongozi wa China ni makini zaidi kuliko viongozi wetu!”
Trump ni msaka urais wa Marekani, Taifa kubwa na tajiri wa kila kitu na kila sekta, lakini aliweza kutumia zaidi ya saa moja katika uzinduzi wa Ilani yake binafsi mbele ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama chake hicho zaidi ya 800 waliokusanyika katika moja ya ukumbi wa jiji la Nashville, katika Jimbo la Tennessee.
Lakini hapa kwetu, tuna chama cha siasa kinachoitwa chama kikuu cha Upinzani nchini, chenye mgombea urais wake maarufu kisiasa, ambaye katika umati mkubwa wa watu ambao katika hali ya kawaida watu wote hao tungewahesabu kama ni kura, alisimama na kunadi Ilani yake kwa dakika 12 tu.
Tanzania, nchi masikini na yenye changamoto kibao zaidi ya mara 1000 ikilinganishwa Marekani, mgombea wake wa urais, Lowassa, amewatajia vipaumbele vyake vitano tu vya elimu, kilimo, afya, mawasiliano, nidhamu na utawala bora, basi.
Mgombea huyo haelezi hata mkakati mmoja wa kuboresha kipaumbele chake hata kimoja kati ya hivyo vitano, badala yake anawataka wananchi wale wampigie kura tu, na tena si kumpigia kura tu, bali wasaidie kumuombea na kwa wengine, kuanzia waume zao, wake zao, ndugu na jamaa zao.
Hao wote wataombwa kura kwa ushawishi wa Ilani ipi?
Kituko kikubwa zaidi, ambacho binafsi naweza kukiita dhihaka iliyopitiliza kwa Watanzania, ni pale alipowaambia maelfu kwa maelfu waliokuwa na hamu ya kumsikiliza pale Jangwani pamoja na mamilioni ya Watanzania, hasa wa vijijini waliokuwa wamejiandaa kusikiliza yaliyomo kwenye Ilani yake kutoka mdomoni kwake, kupitia radio zao na televisheni zao, akiwaambia wakaitafute hotuba yake ndani ya mtandao.
Yaani mama na baba yangu, babu na bibi yangu pamoja na wajomba na shangazi zangu kule kijijini, ambako ndiko kuna asilimia 80 ya wapigakura wote katika nchi hii, wajiandae kwa redio zao na televisheni zao kusikiliza sera za huyo anayetaka kuwa rais wao, halafu waambiwe hotuba haipo, kama wanaitaka waingie kwenye mitandao ya kompyuta na simu zao waitafute waisome wenyewe. Kama si dharau kwao ni nini hii?
Binafsi, nimefanikiwa kuingia kwenye mtandao wa Chadema uliotajwa na Lowassa. Huko nimeikuta hiyo inayoitwa hotuba yake iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya uzinduzi huo wa Ilani yao.
Katika vipengele vyote vikuu 18 vilivyoorodheshwa katika hotuba hiyo kama muhtasari wa mambo muhimu yaliyomo ndani ya Manifesto ya mgombea urais huyo na vyama vyake vya Ukawa, hakuna kipengele kinachozungumzia ufisadi, rushwa, wizi wala ubadhirifu wa mali za umma!
Hivi ni Mtanzania gani katika Taifa hili ambaye hafahamu wazi kwamba rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma, ndivyo kwa kiasi kikubwa vimechangia kurudisha nyuma maendeleo ya uchumi wa Taifa hili?
Je, Ilani hii ya Lowassa, ni yake mwenyewe, ni ya Chadema au Ukawa? Je, viongozi wanaounda vyama vya Ukawa hawafahamu kweli kama rushwa na ufisadi ndivyo vimechangia kudidimiza uchumi wa Taifa hili?
Kwa jinsi Ilani hiyo ilivyo, kwanini nisikubaliane na wanaodai kwamba Lowassa ni mgombea binafsi?
Jambo la mwisho la fedheha kwa Chadema na mgombea wake Lowassa, ni kuingiza mambo ya mizaha katika mambo na wakati muhimu. Ndugu zangu, sisi ni Waafrika. Tuna mila na desturi zetu zinazoheshimu ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki.
Daud Balali alikuwa Gavana wa Tanzania. Huyu ni marehemu. Ameacha ndugu, mjane, watoto na jamaa zake hapa duniani katika maeneo mbalimbali ya nchi hii na hata nje ya nchi.
Hivi linapotajwa jina la Balali kwenye mikutano ya hadhara ya kisiasa kwamba yuko hai na atarejeshwa nchini, familia yake hiyo pamoja na ndugu na jamaa zake wanatiwa uchungu na maumivu kiasi gani?
Inaingia akilini kweli kwa Lowassa kuidhihaki familia ya Balali kwa sababu yu ya kutaka urais?
Au anasema atawafungulia Babu Seya na wanawe kutoka jela. Hivi Mahakama inajisikiaje kwa tamko hili, tena baada ya Lawrence Masha kutuhumu taasisi hiyo ya utoaji haki? Au, wale watoto walionajisiwa na ushahidi ukatolewa mahakani, na wazazi wao wanajisikiaje wanaposikia Lowassa akirudiarudia mpango wa kumuachia huru Babu Seya? Kweli zigo la mwenzio ni kanda la sufi! Na hapa sikutaka kuzungumzia wenye tuhuma za ugaidi.
Nihitimishe kwa kusema kwamba uzinduzi wa Ilani ya Chadema ulifeli sana. Naamini baada ya mkutano ule wa Jangwani, upepo wa kisiasa dhidi ya Chadema na Ukawa, umepungua kwa zaidi ya asilimia 50.
Chadema na Ukawa kwa ujumla, wamejimaliza wenyewe kisiasa!
Hata hivyo, nafsi yangu inaamini kwamba kufeli huko kwa Chadema hakukuwa kwa bahati mbaya, bali kulipangwa kiufundi na viongozi wake ili kuwazuga na kuwahadaa Watanzania kwa ujumla wao.
Chadema kina dhamira ya kuwauzia Watanzania mbuzi kwenye gunia. Viongozi wa Chadema anatengeneza kwa ustadi mkubwa hadithi ile ya kula ugali kwa harufu ya samaki, ambayo inahusishwa na ndugu zetu jamii ya Wapare wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Chadema inataka kuwaaminisha Watanzania kwamba Lowassa yule aliyepata kuwa waziri na waziri mkuu katika Serikali ya CCM, aliyekuwa na sauti inayokata kama upanga, akikanyaga ardhi kwa kishindo, bado ni huyu huyu wa sasa anayegombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa.
Kwa hakika kabisa, huyu siye! Huyu wa sasa hafiki hata nusu ya yule wa zamani! Kwa mtindo
huu, kama baadhi ya Watanzania wenzetu hawa wataendelea kusukumwa naupepo huu wa Lowassa, siku yaja ambayo watajikuta wakilishwa ugali waokwa harufu ya samaki!
- See more at: http://raiamwema.co.tz/ya-chadema-lowassa-na-hadithi-ya-ugali-kwa-harufu-ya-samaki#sthash.ezvZK6zD.dpuf
No comments :
Post a Comment