Mwaka 1995 wakati akihutubia mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwalimu Julius Nyerere alisema mgombea urais kupitia chama hicho anatakiwa kukidhi matarajio ya Watazania na siyo anayekidhi matarajio ya wachache wenye fedha zao.
Siku hiyo alisema Watanzania wasipoyapata mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya chama hicho.
Mara kadhaa alisisitiza nchi kuwa na viongozi wanaochukia rushwa kutoka rohoni, watakaoweza kuitoa Tanzania kutoka ilipo kiuchumi na kuipelekea mbele zaidi. Pia alisisitiza Watanzania kuukataa udini na ukabila
Alichokisema Mwalimu Nyerere kwa kiwango kikubwa ndicho ambacho wagombea urais wanaochuana vikali, Edward Lowassa (Chadema) na Dk John Magufuli (CCM) wanakizungumza tangu kuanza kwa kampeni.
Leo ni siku ya 12 tangu Dk Magufuli kuanza kampeni zake na siku ya saba tangu Lowassa aanze safari ya kuelekea Ikulu.
Katika kipindi hicho kifupi wagombea hao wamekuwa wakizunguka mikoa mbalimbali nchini na kuwaeleza wananchi kile ambacho watawafanyia iwapo watawachagua.
Katika utekelezaji wa ilani ya CCM, Dk Magufuli amekuwa akiahidi baadhi ya vitu kama; elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, kuboresha huduma za afya kwa kujenga zahanati, hospitali kila kijiji, kata, wilaya na mkoa, kukuza soko la mazao ya kilimo na ujenzi wa barabara za lami nchini.
Lowassa naye ameahidi elimu bure mpaka chuo kikuu, kufuta ushuru na kodi kwa wakulima, kufuata misingi ya utawala bora, maisha bora kwa masikini, kufuta kodi zote katika vifaa vya michezo na muziki, kumaliza kero na matatizo yanayowakabili wakulima, wafugaji, wafanyabiashara, walimu, wanafunzi na kuboresha huduma ya maji.
Pamoja na ahadi nzuri za wagombea hawa kuna baadhi ya mambo binafsi naona bado hawajayatolea ufafanuzi wa kina licha ya kuwa na umuhimu mkubwa katika ustawi wa taifa letu.
Wagombea hawa wanazungumzia vitu vinavyogusa maisha ya watu na wanasisitiza zaidi kuhusu mambo ya ndani ya nchi kuliko nafasi ya Tanzania dhidi ya nchi nyingine kupitia diplomasia ya uchumi.
Ikumbukwe kuwa Tanzania si kisiwa hivyo kuna haja ya wagombea hawa kuweka msisitizo jinsi nchi itakavyoshirikiana kisiasa na kiuchumi na Jumuiya ya Afrika Mashariki na nyingine ulimwenguni.
Lowassa na Dk Magufuli kwa nyakati tofauti wamelizungumzia suala la kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lakini sidhani kama wametuliza kiu ya watanzania kuhusu suala la Katiba Mpya ambalo kwa sasa ni kama limeligawa taifa na wananchi.
Kimsingi, kati yao mmoja akiwa rais ni wazi kuwa kuna mambo yatampa changamoto hasa katika utekelezaji wake kutokana na nchi kuwa na Katiba iliyo nyuma ya muda na hata Katiba Inayopendekezwa nayo haikupatikana kwa maridhiano kati ya pande mbili zinazovutana.
Nimesikia suala la kuondoa umasikini likizungumzwa kwa kina kwelikweli na wagombea wetu wa urais, binafsi bado nina kiu kubwa ya kuwasikia wakieleza dira ya taifa ya maendeleo watakayoiandaa kuondoa umasikini nchini.
Wagombea wanasema wana mipango ya kuipeleka Tanzania katika uchumi imara huku wakitumia neno “mabadiliko”. Binafsi nina hamu ya kuwasikia wakisema dira jumuishi kwa Zanzibar na Tanzania bara itakayosaidia kutekeleza mikakati yao.
Vipi kuhusu utunzaji wa mazingira. Nchi nyingi duniani zinajilinda na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutunza mazingira.Mito inakauka, kina cha baadhi ya maziwa kinapungua wagombea wanatakiwa kutueleza watapambana vipi na suala hili.
Sekta ya afya imekuwa na matatizo kila uchwao, tunachokihitaji ni wagombea wetu kutueleza wamekuja na mwarobaini gani wa kumaliza manung’uniko ya watanzania katika hospitali zetu.
Si kuishia kusema akina mama hawatalala chini tena, kikubwa hapa ni kutueleza dawa ya kumaliza tatizo hilo, ikiwa ni pamoja na kuboresha dawa, vifaa tiba, kuweka mazingira mazuri ya kazi kwa watumishi wa sekta ya afya na kuboresha miundombinu.
Ukimwi bado ni tishio, tunahitaji kusikia wagombea wetu wa urais wakitueleza jinsi watakavyopabana na ugonjwa huu. Pia kuna malaria, saratani, shinikizo la damu, kifua kikuu, kisukari na mengine mengi.
Lowassa ameeleza jinsi ambavyo atawasaidia wanamichezo, ikiwa ni pamoja na kufuta kodi katika vifaa vya michezo jambo ambalo linaweza kusaidia kwa kiasi fulani.
Tanzania kwa muda mrefu imekuwa kichwa cha mwendawazimu katika michezo. Hakuna mchezo hata mmoja ambao taifa linafanya vyema hivyo ni wakati muafaka kwa wagombea wetu kuonyesha kwa vitendo jinsi watakavyoweza kulisaidia kundi hili kubwa.
Ninafuatilia mikutano ya kampeni ya mgombea urais wa Chadema chini ya mwamvuli wa Ukawa, nimezungumza na wananchi wachache na kunieleza kuwa wanahitaji mabadiliko.
Mabadiliko hayo pia Dk Magufuli amekuwa akiyasisitiza zaidi katika mikutano yake ya kampeni, hivyo ni wakati sasa wa wagombea hawa kutueleza watafanya nini kufanikisha jambo fulani ili kuwapa wananchi nafasi nzuri ya kuwatafakari na kuamua hiyo Oktoba 25, mwaka huu.
No comments :
Post a Comment