Manyoni/Mara. Mgombea urais kupitia tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesema Serikali imetenga Sh866bilioni, kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya barabara nchini.
Akizungumza na wakazi wa Manyoni mkoani Singida katika mkutano wake wa kampeni kwenye Viwanja vya Tambuka Reli, Dk Magufuli alisema: “Nikiwa Waziri wa Ujenzi, nilijenga barabara ya lami kutoka Manyoni hadi Itigi.
“Ziko barabara nyingi zimekamilika na zimesaidia nauli kushuka ikilinganishwa na kipindi cha nyuma, lakini bado Serikali imetenga Sh866bilioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa barabara zilizobaki”
Dk Magufuli aliyetokea mkoani Dodoma, aliahidi kujenga reli ya kutoka Manyoni kwenda Dar es Salaam hadi Tabora, lengo likiwa ni kuinua uchumi kwa Wana-Manyoni Mashariki na taifa kwa ujumla.
Mgombea huyo alirejea kauli yake kuwa Serikali ya awamu ya tano italeta umeme kwa kila kijiji ambao utaendesha viwanda na kuongeza wawekezaji wa ndani na nje.
“Awamu ya tano ya Dk Magufuli itakuwa ya viwanda vya kati na vikubwa ambavyo vitawanufaisha wakulima na wafugaji,” alisema Dk Magufuli.
Alisema kutokana na viwanda hivyo, wafanyabiashara wadogo hawatatozwa kodi yoyote, kodi zitatozwa kwa wenye viwanda na ataondoa ushuru kwa wananchi wa kipato cha chini.
Magufuli alisema ataboresha mishahara ya watumishi wote wa Serikali, kwani wamekuwa wakilipwa kidogo ikilinganishwa na kazi wanazofanya, huku wengine kutopewa malipo ya likizo.
Alisema elimu kwa shule za msingi hadi kidato cha nne itatolewa bure endapo ikiingia madarakani, lengo likiwa ni kumsaidia Mtanzania asiye na uwezo wa kupata elimu.
Serikali ya awamu ya tano itatoa Sh50milioni kwa vikundi vya akina mama na vijana kwa kila kitongoji; kijiji na kata ili kujikwamua kimaendeleo na kuepukana na janga la umaskini.
Lugola aibukia kwa Samia
Wakati huo huo mgombea ubunge wa Jimbo Mwibara, Kangi Lugola amedai wapiga debe wa mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa, walimshawishi kujiunga na safari ya matumaini iliyoishia njiani na ndipo akaamua kumuunga mkono Dk John Magufuli.
Lugola alisema hayo kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, uliofanyika Uwanja wa Mnadani Kisorya, katika Jimbo la Mwibara mkoani Mara.
“Ni kweli nilipanda basi la matumaini, nilivutiwa na wapiga debe wake si mnawajua walivyo? Walichukua hadi begi langu wakaliingiza huko, lakini gari lao liliharibikia njiani, nikaliona basi jipya la Magufuli sasa nimepanda tunaelekea Ikulu,” alisema Lugola na kushangiliwa na umati wa watu waliofurika kwenye mkutano huo.
Lugola alisema anamfahamu vizuri, Dk Magufuli kuwa ni mchapakazi kwa sababu alikuwa mwalimu wake wa somo la fizikia alipokuwa kidato cha nne.
Alitumia nafasi hiyo kuelezea njaa inavyowatesa wananchi wa jimbo hilo, hivyo kumwomba mgombea mwenza Samia awasaidie kuisisitiza Serikali, kupeleka chakula cha msaada jimboni na maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na njaa.
Alisema tatizo hilo ni kubwa kwa kuwa asilimia 70 ya wakazi hao wanakula mlo mmoja kwa siku badala ya milo mitatu.
“Pia hakuna hospitali ya Serikali katika jimbo hili, kuna hospitali ya misheni ambayo gharama za upasuaji ni kubwa wananchi wengi hawamudu, hakuna gari la wagonjwa na huwa ninabeba wagonjwa kwa gari yangu hivyo huwa natumia langu binafsi kuwasafirisha inapotokea hitaji hilo,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo, Samia aliahidi atahakikisha anafikisha taarifa hizo panapohusika, anajua Serikali imejipanga kukabiliana na janga hilo.
“Hakuna mwananchi atakayekufa njaa, ninajua Serikali imejipanga vilivyo, chakula kitaletwa mtauziwa kwa bei rahisi,” alisema.
Alisema pia changamoto ya kukosekana kwa hospitali itapatiwa ufumbuzi watakapofanikiwa kuingia madarakani, wataitatua kupitia Ilani ya uchaguzi kwa kuwa imebainishwa jinsi hospitali na vituo vya afya vitakavyojegwa.
Mama Samia alisema pamoja na mambo mengine, watakapoingia madarakani watahakikisha wanajipanga vyema kupambana na ujambazi ambao umekuwa ukifanywa kwenye maji katika Ziwa Victoria, ambapo ni tegemeo la kipato kwa wavuvi wa eneo hilo.
Aliwaomba wakazi wa jimbo hilo kumpigia kura, Lugola kwa kuwa ni miongoni mwa wabunge wanaowakilisha vyema, pia aliwaombea kura na wagombea udiwani wa kata za Bunda kupitia CCM.
No comments :
Post a Comment