Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, October 3, 2015

AHADI: Magufuli kufuta rushwa.

Mgombea wa Urais kupitia CCM, Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Ikungi kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu, uliofanyikakwenye viwanja vya Mnadani, Ikungi mkoani Singida jana. Picha: Adam Mzee
Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Magufuli ametangaza kiama kwa wala rushwa, mafisadi na viongozi wanaowaonea wanyonge, atakapochaguliwa kuwa rais. 
 
Aidha, amewataka watumishi wazembe na wala rushwa serikalini watubu na wajirekebishe mapema kama wanataka kufanya naye kazi atakapoingia Ikulu baada ya Oktoba 25, mwaka huu.
 
Alisema serikalini kumejaa mafisadi ambao wameitafuna nchi kwa muda mrefu hivyo ameamua kuomba urais ili awapandie huko huko juu waliko aweze kuwashughulikia kwa urahisi.
 
“Wanasema aliyejuu mngoje chini, mimi nimewasubiri kwa muda mrefu mafisadi washuke chini hawashuki sasa sitawasubiri chini nitawapandia huko huko juu niwashushe ndiyo sababu nataka mnipeleke Ikulu nikapambane nao,” alisema Dk. Magufuli.
 
Aliyasema hayo jana wilayani Manyoni mkoani Singida katika mkutano wake wa kampeni, ikiwa ni siku yake ya kwanza akitokea mkoani Dodoma.
 
Alisema amekuwa mtumishi mwadilifu hivyo kazi ya kuwaondoa mafisadi serikalini itakuwa rahisi kwake kwasababu anawajua walipo kutokana na kufanyakazi serikalini kwa muda wa miaka 20 mfululizo.Alisema sehemu yenye ufisadi maendeleo hayawezi kupatikana kwa sababu fedha zote zinazopatikana zinaishia mikononi mwa watu wachache wenye tamaa huku wananchi wa kawaida wakiteseka.
 
“Msimamo wangu ni kutumikia watanzania wanyonge ili wafaidi matunda ya nchi yao, sasa kuna mafisadi ambao ni wachache wanawatisha wafanyakazi kwamba Magufuli akishinda atawashughulikia, mimi sitakuwa na shida na mtumishi mwadilifu na mchapakazi, wale wanaoendekeza michakato na njoo kesho njoo kesho ndiyo siwataki” alisema.
 
Alisema kama angekuwa na tamaa ya mali angekuwa bilionea kwasababu Wizara ya Ujenzi ambayo ameiongoza kwa miaka mingi ndiyo inaongoza kwa kuwa na fedha nyingi za miradi ya ujenzi wa barabara.
 
Alisema ataendelea kuwa mwadilifu na amejipanga kuunda serikali ya watu waadilifu, wachapakazi na kwamba wale waliozoea kuwaambia wananchi njoo kesho na michakato inaendelea hawatakuwa na nafasi kwenye utawala wake.
 
Dk. Magufuli alisema anamwogopa Mungu na ataendelea kumweka mbele katika utendaji wake iwapo atachaguliwa kuingia Ikulu ili kuwaondolea Watanzania kero mbalimbali zikiwamo ushuru wa ovyo ovyo barabarani.
 
Alisema Watanzania wamekuwa wakitumia rasilimali zao kulima bidhaa bila msaada wowote lakini wanapovuna na kuanza kupeleka sokoni mazao yao, wamekuwa wakikumbana na vikwazo mbalimbali vya kodi ambazo nyingi huishia mikononi mwa watu.
 
“Nitakomesha vikodi vya ovyo ovyo ili watu waishi kwa raha, sitakubali serikali yangu iwe inakimbizana kimbizana na mamalishe na boda boda barabarani, kwasababu nitajenga viwanda, serikali itapata kodi huko kwenye viwanda vikubwa vikubwa,” alisema.
 
Aidha, Dk. Magufuli alisema kuwa anaposema serikali yake itaifanya Tanzania kuwa ya viwanda anamaanisha hivyo lakini kuna watu wamekuwa wakimwona kama mtu anayeota ndoto za mchana.
 
Alisema Tanzania ya viwanda inawezekana kwasababu wilaya nyingi nchini hivi sasa zina umeme na kwamba ugunduzi wa gesi nchini utachochea kwa kiwango kikubwa uanzishwaji na ukuaji wa viwanda vidogo vidogo na vikubwa.
 
Dk. Magufuli aliwahakikishia wakulima mazao watakayolima yataongezewa thamani vitakapojengwa viwanda vingi vya uzalishaji nchini ambavyo pia vitaongeza nafasi za ajira.
 
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Abdalah Bulembo alisema wanachama wa chama hicho waliohamia Ukawa wamekwenda kutafuta vyeo na wakikosa watarudi CCM hivyo aliwataka wananchi kumchagua Dk. Magufuli.
 
Bulembo aliwaambia wananchi hao kuwa Dk. Magufuli alipatikana kwa njia ya demokrasia ndani ya vikao mbalimbali vya chama hicho na ni msomi mwadilifu na mchapakazi asiye na makando kando ya ufisadi.
Akiwahutubia wananchi wa Singida, Dk. 
 
Magufuli alisema ana uhakika yeye ndiye rais wa awamu ya tano na wapinzani wanajua kuwa wanamsindikiza kwenda Ikulu ya Magogoni.
 
Amewataka wamachague kwa kishindo na kuwaacha mafisadi ambao alisema wakiingia Ikulu wanaweza kuuza nchi ili kurejesha fedha zao ambazo wamezitumia kwenye uchaguzi.
 
Alisema wapinzani wake wameshaanza kugawana rasilimali za kuuza kufidia gharama zao za kampeni wakidhani kwamba wanaweza kuingia Ikulu kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
 
Alisema yeye hana deni analopaswa kulipa atakapoingia Ikulu kwasababu hakutumia hata senti wakati wa mchakato wa kuwania kuteuliwa na CCM kuwania nafasi ya urais.
 
Aliwataka wananchi wa Singida Mashariki kumchagua mgombea ubunge wa CCM, Jonayhan Njau na kuachana na Mbunge wa Chadema, Tundu Lissu kwani kwa muda mrefu alilitelekeza jimbo hilo.
 
Alisema Njau ni mtu mchapakazi na mwadilifu ambaye licha ya kukosa ubunge mwaka 2010 aliendelea kukitumikia chama hicho kwa kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo.
 
Wakati huo huo, mbunge aliyekuwa swahiba wa mgombea wa Ukawa, Edward Lowassa, Diana Chilolo amemgeuka na kumrushia makombora kwamba ni mtu mwenye tamaa ya madaraka.
 
Chilolo aliyekuwa mbunge wa viti maalum Mkoa wa Singida, alisema Lowassa amekosa mshauri mzuri na kuhamia kwake Chadema ni mwisho wake wa kisiasa hapa nchini.
 
Alisema yeye alikuwa swahiba mkubwa wa Lowassa ambaye walikuwa wakikaa naye jirani ndani ya ukumbi wa Bunge lakini hakumfuata kama walivyofanya rafiki zake wengine ndani ya CCM.
 
Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu, alisema wakati jimbo lake likiendelea kustawi kwa huduma za jamii kama afya, maji, barabara na elimu, jimbo la Singida Mashariki limeendelea kurudi nyuma mwaka hadi mwaka.
 
Alisema baadhi ya kero kwenye jimbo hilo linaloongozwa na Chadema ni wanafunzi kukaa chini, kukosa maji na kukosa barabara za lami.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment