Rais Jakaya Kikwete
Dar es Salaam. Tanzania imeahidi kuendelea kushiriki katika mazungumzo ya kulinda amani na kupeleka wanajeshi katika maeneo husika kuimarisha ulinzi.
Rais Jakaya Kikwete alisema hayo jana katika hafla ya kumuaga iliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Alisema Tanzania kushiriki katika mijadala na operesheni za kutunza amani kumeleta faida nyingi ikiwamo kudumisha uhusiano mzuri wa kidiplomasia na nchi zingine.
“Tutaendelea kushiriki kikamilifu katika operesheni za kutunza amani kwa sababu tumeona faida kubwa zilizopatikana,” alisema Rais Kikwete.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema wizara yake imeimarisha uhusiano kati ya Tanzania na nchi za nje jambo lililoleta faida.
“Urafiki wetu na nchi mbalimbali umeleta manufaa kwa Taifa, Marekani ilitoa Dola 698 milioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara, umeme na maji, huku China ikitoa Dola 1.9 bilioni za Marekani pamoja na kushiriki ujenzi wa bomba la gesi na Uwanja wa Ndege wa Zanzibar,” alisema Membe na kuongeza:
“Wizara pia imevutia wawekezaji, huku ikipanua wigo wa uwakilishi kwa kufungua balozi katika nchi za Brazil, Oman, Uturuki, Malaysia, The Hague-Uholanzi na Qatar.”
Balozi mstaafu Paul Rupia alimpongeza Rais Kikwete kwa kusimamia Sera ya Mambo ya Nje iliyoanzishwa mwaka 2014, huku kukiwa na ongezeko la watumishi katika wizara hiyo kutoka 250 wakati anaingia hadi 418 hivi sasa.
Wakati huohuo; Rais Kikwete ameridhia kuigawa Hifadhi ya Selous katika maeneo manane ya kiutawala ili kurahisisha ulinzi na kudhibiti ujangili. Alitoa tamko hilo juzi alipozindua Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (Tawa) baada ya kupokea hilo kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Akiwasilisha taarifa ya wizara yake kuhusu mchakato wa kuipata mamlaka hiyo, Nyalandu alisema hatua kadhaa zimechukuliwa ili kulinda wanyama na hifadhi za Taifa, lakini ujangili unaendelea kuwa changamoto kubwa.
Alisema imegundulika kuwa hata wale wenye vibali huwa wanakwenda kinyume na utaratibu waliopewa.
“Kuanzia sasa napiga marufuku utoaji wa vibali vya uwindaji. Hii ni kwa miaka miwili mfululizo. Ujangili umekithiri kwa kiasi kikubwa. Tumedhamiria kupambana na ujangili ili kuimarisha sekta ya utalii,” alisema Nyalandu.
Pia, aliwataka wajumbe wa bodi hiyo kuhakikisha wanaweka mikakati imara ya kuhifadhi na kulinda wanyamapori ili idadi yao iongezeke badala ya kupungua.
Hifadhi ya Selous ina eneo lenye kilomita za mraba 55 ikiwa imezunguka mikoa kadhaa.
No comments :
Post a Comment