dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, October 19, 2015

Magufuli: Asiyefanya kazi na asile!

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni wilayani Misungwi, Mwanza jana.
By Waandishi Wetu, Mwananchi
Magu/Misungwi. Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amewataka wananchi kujipanga kufanya kazi kwa sababu Serikali yake haitavumilia watu wavivu.
Akihutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Shule ya Msingi Misungwi jana, Dk Magufuli alisema hata vitabu vya dini vimeelekeza kwamba asiyefanya kazi na asile, hivyo wanaoahidi vitu vya bure wanawadanganya Watanzania.
“Tujipange kufanya kazi, hata maandiko ya vitabu vitakatifu yanasema, asiyefanya kazi asile… Misungwi nitaibeba kwa nguvu zangu zote nikichaguliwa,” alisema.
Pia alisema nyumba za tembe ambazo zinaahidiwa na wagombea wenzake kwamba zitaondolewa ndani ya siku 100 ni uongo hivyo wasisikilizwe, bali atakachofanya ni kuhakikisha bei ya vifaa vya ujenzi inapungua na ameanza na saruji.
Alisema anatambua kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na tatizo la maji na kuwaahidi wananchi kulishughulikia na wasimsumbue mbunge wao na kwamba anapoahidi kutoa Sh50 milioni kila kijiji nchini watu wanamshangaa lakini Serikali ina fedha, nyingine zilikuwa zinatafunwa na mafisadi.
“...Ndiyo maana baada ya kusikia nimetangazwa mengine yakakimbia… hivi sasa wanasema Serikali haijafanya chochote wakati wengine wamezeekea humu mpaka wakang’oka meno na kuwekewa ya bandia, mbona hawakuondoka muda wote?” alihoji Dk Magufuli.
Mgombea huyo huku akichomeka lugha ya Kisukuma kila mara, alisema ujenzi wa barabara ya Usagara – Kisema ukikamilika, malori yatakuwa hayaruhusiwi kuingia katikati ya mjini wa Mwanza. Aliahidi kufufua viwanda vya kuchambua pamba ili kuleta mabadiliko ya kweli.
Dk Magufuli aliahidi kufufua kilimo cha pamba kwa kuhakikisha mkulima anapata pembejeo na kunufaika na zao hilo na kwamba, haiwezekani pamba ilimwe Tanzania Ulaya wavae nguo mpya halafu Watanzania waletewe mitumba.
Hata hivyo, mgombea huyo akiendelea kutoa ahadi sauti za wanawake zilisikika zikimtaka kuzungumzia samaki kazi ambayo ndiyo wanayoitegemea kiuchumi, hivyo akalazimika kutamka kuwa atafuta ushuru unaoonekana kuwa kero.
“Nitafufua Chuo cha Kilimo Ukiriguru na kutumia wataalamu wake kuboresha kilimo cha pamba,” alisema.
Mgombea ubunge Jimbo la Misungwi, Charles Kitwanga alisema kuna sifa ya Dk Magufuli ambayo haijatajwa nayo ni ubunifu, kwani alianzisha mfuko wa kujenga barabara kwa fedha za ndani hali iliyowashangaza wafadhili.
“Hizi barabara tunazotaja kama siyo yeye zisingekuwapo, mnakumbuka wafadhili walikuwa wanakataa kutukopesha, akaanzisha mfuko wa kujenga barabara mpaka wafadhili wanauliza fedha zitakapopatikana, akawaambia tunazo,” alisema.
Kitwanga alimwomba mgombea huyo kuwajengea hospitali ya wilaya na kiwanda cha kusindika nyanya, zao linalolimwa kwa wingi.
Akiwa Magu, Dk Magufuli alisema endapo atachaguliwa, ataubadilisha mji huo kwa kutatua kero sugu ya maji na kujenga barabara zinazozunguka mji huo. Alisema atatumia uwezo wake wote kuhakikisha kilimo cha pamba kinakuwa bora ili bei ya zao hilo ipande na kuwanufaisha wakulima.
Akihutubia umati wa watu kwenye Viwanja vya Sabasaba jana, Dk Magufuli alisema: “Natambua kwamba Magu shida yenu kubwa ni maji, mmekuwa mkitaabika kwa muda mrefu, huku Ziwa Victoria likiwa limewazunguka.
“Kwa kutambua kwamba maji ni muhimu kwa binadamu, hapa Magu lazima mpate maji na tayari Kampuni ya Cowi inafanya upembuzi yakinifu kuhakikisha maji yanafika, wakikamilisha tu suala la maji kufika Magu niacheni mimi...”
Dk Magufuli alisema anataka kuona Magu inabadilika na kwamba ameahidi kujenga barabara zinazozunguka mji huo na kuunganisha wilaya jirani.
Alisema amezaliwa na kulima pamba pamoja na kufuga, hivyo ni mtoto wa mkulima na mfugaji na kwamba atatumia uzoefu wake kuhakikisha bei ya pamba inakuwa juu. “Nafahamu kwamba bei ya pamba kwa sasa imeshuka, lakini mimi ni mtoto wa mkulima na mfugaji, pamba naifahamu vizuri, nataka tutengeneze mazingira mazuri kwa wakulima wa pamba ili iwe bora,” alisema Dk Magufuli.
Aliwataka wakazi wa mji huo, kula fedha za watu wanaowahonga ili wawachague, akisema hizo ni fedha zao ambazo walizichuma kwa kutumia ufisadi.
“Nyie mkipewa fedha kuleni, kwani kula ni kwa mafisadi kulala kwa Magufuli,” alisema na kuongeza kuwa akichaguliwa, atakuwa rais wa watu wote, kwa kuwa maendeleo hayana chama.
Aliahidi kufuta ushuru ambao umekuwa ukiwasumbua wafanyabiashara ndogondogo sambamba na kupunguza kodi za vifaa vya ujenzi ili bei ya vifaa hivyo ipungue na kuwawezesha wananchi kununua na kujenga nyumba bora.

No comments :

Post a Comment